Samia Suluhu Hassan sasa ndiye Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini yapo mambo tisa yanayomsubiri ayapatie ufumbuzi katika siku 1,691 atakazohudumu madarakani kutoka sasa hadi mwaka 2025 utakapofanyika uchaguzi mkuu.
Samia ameapishwa jana asubuhi kushika wadhifa huo kwa mujibu wa Ibara ya 37(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 baada ya Rais aliyekuwapo, John Magufuli kufariki dunia kwa ugonjwa wa moyo Machi 17, 2021.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi wanaona Rais Samia atakabiliwa na mambo tisa mbele yake na moja ni kupanga safu ya watakaomsaidia ili kutimiza ndoto na maono yake kama walivyofanya watangulizi wake.
Jambo jingine ni kuenzi miradi, mipango na mikakati mizuri ya kimaendeleo iliyoanzishwa na hayati Magufuli. Miongoni mwa mambo anayotazamiwa kuyaendeleza kwa kasi ni ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme la Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Jambo la tatu ni kujenga umoja wa kitaifa na mshikamano vinavyoelezwa vimetetereka kutokana na tofauti za kisiasa, kidini na kimaeneo.
Mengine ni masuala ya kuzingatiwa misingi ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari, mchakato wa Katiba mpya na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao hawajaongezewa mishahara tangu awamu ya tano ilipoingia madarakani 2015.
Jambo jingine litakalomkabili ni kuimarisha misingi ya utawala bora uliotikiswa na mfano ni baadhi vitendo vya viongozi kutoa amri za kukamatwa na kuswekwa ndani watu bila sababu za msingi.
Pia atakabiliana na mtihani mgumu wa kurejesha imani kwa wafanyabiashara wanaolalamikia mfumo wa kodi kuwa unaua biashara.
Rais Samia mara baada ya kuapishwa jana alilihutubia taifa na kuwataka Watanzania kuzika tofauti zao na kuwa wamoja, kudumisha amani kwakuwa si wakati wa kutizama yaliyopita, bali ni wakati wa kutazama yajayo.
"Si wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele. Ni wakati wa kufutana machozi na kufarijiana. Ni wakati wa kuweka nguvu za pamoja ili kujenga Tanzania mpya…" alisema Rais Samia.
Wachambuzi wabainisha changamoto
Rwezaura Kaijage ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Ruaha (Rucu), alisema Rais Samia anakabiliwa na changamoto mbili kubwa ambazo ni kuunda safu ya uongozi itakayozungumza lugha moja.
"Jambo la kwanza linalomkabili ni utekelezaji sahihi na hapa naomba nieleweke, utelekezaji sahihi wa majukumu aliyoyaacha mwenzake. Kuvaa viatu unaweza kuvaa viatu vya mtu mwingine lakini kukutosha hilo ni jambo lingine," alisema.
"Lazima atafute safu ya uongozi atakayoshabihiana nayo. Katika nchi yetu yeye ni mtu wa juu kabisa mwenye uamuzi. Dhamira yake na mwelekeo wake unategemea safu hii. Jambo hili (kifo) limetokea ghafla si rahisi kupata haraka," aliongeza.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kisiasa ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema Rais Samia amepokea uongozi kutoka kwa mtu aliyefanya mageuzi makubwa nchini.
"Changamoto atakayoipata ni namna gani ataendeleza moto huo wa kimageuzi. Lakini Rais Magufuli alikuwa binadamu na kama binadamu anakuwa na upungufu wake.
"Kuna upungufu wa kiutawala ambao labda pengine sasa Rais Samia anatakiwa akae chini na kutathmini na kuboresha ili utawala wake uwe bora zaidi, hasa katika utawala bora na mambo ya demokrasia."
Mchambuzi mwingine, Basil Lema alisema Rais Samia atakabiliwa na kufufua utawala wa sheria na kidemokrasia, kufuta sheria kandamizi ili kuruhusu uhuru wa habari na kuboresha mazingira rafiki ya biashara na ulipaji kodi.