Mkuu wa Wilaya ya Geita, Fadhili Juma (katikati) akionesha kipeperushi chenye maelezo ya namna ya kutoa taarifa za ulinzi na usalama kwa kampuni ya GGML. Kulia ni Meneja wa Ulinzi kutoka GGML, George Kaijunga na Meneja wa masuala ya kijamii- GGML, Joseph Mangilima.
NA MWANDISHI WETU
Katika jitihada za kushirikiana zaidi na jamii inayouzunguka mgodi, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), imezindua rasmi mfumo wa kutoa taarifa mbalimbali za ulinzi, usalama na za kijamii ambapo raia wema wamepatiwa fursa ya kupiga simu ya bure bila malipo yoyote.
Katika mfumo huo wa kidigitali, raia wema wanaozunguka eneo la mgodi wataweza kupiga simu namba 0800 750 145 bila malipo yoyote wanapobaini vitendo vya uhalifu vikiwemo kula njama, uharibifu wa mali za kampuni, vitendo vya rushwa kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi au wakandarasi wanaofanya kazi na kampuni ya GGML, vitendo vya kiusalama ikiwemo uendeshaji wa magari usio salama, na taarifa nyinginezo zote zinazoihusu kampuni.
Akizindua mfumo huo mkoani Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Fadhili Juma alisema teknolojia ya habari na mawasiliano ni muhimu katika kipindi hiki ili kujibu changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ikiwemo uhalifu na hujuma ya miundombinu mbalimbali ikiwemo umeme au mabomba ya maji ambayo huigharimu serikali fedha nyingi.
"Naipongeza sana Kampuni ya GGML kwa kuja na ubunifu huu kwa kuwa lengo lake litaisaidia pia serikali kupata taarifa mbalimbali za kiuhalifu. Jukumu la serikali ni kuweka mazingira bora ya kumlinda mwekezaji ili afanye shughuli zake kwa usalama na ufanisi, akitoa ajira na kuchangia pato la taifa kupitia kodi na tozo mbalimbali," alisema.
Akizungumzia mfumo huo, Meneja Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya ulinzi kutoka Kampuni ya GGML, Suleiman Machira alisema mfumo huo umekuja kipindi muafaka wakati kampuni ya GGML na wakazi wanaouzunguka mgodi huo wakiwa wameimarisha mahusiano mema ya kindugu na kufanya shughuli zao kwa ushirikiano mkubwa.
"Tumekuwa na raia wema ambao wamekua tayari kutoa taarifa mbalimbali ambazo zingeisaidia kampuni lakini wanashindwa kutoa taarifa kwa sababu ya kukosekana kwa mfumo rahisi usio na gharama wa kutoa taarifa," alisema Machira.
Machira aliongeza kuwa mwekezaji anapofanya shughuli zake kwa usalama bila kuhujumiwa au kufanyiwa vitendo vya kihalifu maana yake ataweza kufanya shughuli zake za uwekezaji kwa amani na kuchangia pato la uchumi wa mkoa wa Geita na Tanzania kwa ujumla.
Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, GGML imefadhili miradi mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 30 katika kipindi cha miaka 3 katika mkoa wa Geita.
Hivi karibuni GGML pia imeibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini lakini ilichukua tuzo pia katika vipengele vya mazingira, usalama, mlipaji bora wa kodi, uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) na uwezeshaji bora wa raia wa ndani ya nchi kwa mwaka 2019/2020.