Friday, February 12, 2021

Wizara ya Mifugo na Uvuvi yawapika Wataalamu kutoka halmashauri za mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro


Na John Walter-Manyara

Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikishirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) imewakutanisha maafisa Ugani kutoka Halmashauri za mikoa ya kanda ya kaskazini,  Arusha,Manyara na Kilimanjaro katika kuwajengea uwezo wa kutekeleza Majukumu yao ya huduma za Ugani kwa Wafugaji.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati, Mkurugenzi wa utafiti, mafunzo na huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Angelo Mulawa,amesema lengo la kikao kazi hicho ni kuwawezesha wataalamu hao kujua teknolojia ambayo wizara na sera zinaweza kutumia katika  kuboresha  sekta ya Mifugo na Uvuvi ili  kuongeza uzalishaji kwa wingi.

Amesema wizara inatazamia wafugaji wafanye ufugaji kibiashara ili kuweza kupata kipato pamoja na kuzalisha malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda vya usindikaji wa Nyama,Maziwa ili kuhakikisha pato la taifa linaongezeka.

Mulawa amesema wamewapatia mafunzo hayo Maafisa ugani hao ili nao wakawasadie wafugaji kutambua namna ya kuhimilisha kwa kutumia mbegu za madume bora na majike sahihi kwa kupokea mbegu hizo.

Pamoja na hayo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kutoa dawa za kuogeshea mifugo kwa ruzuku kupitia Halmashauri ambazo na zinasimamiwa na maafisa ugavi na watendaji wengine wa serikali kuhakikisha inawafikia wafugaji katika Kata na vijiji vyote.

Amewataka wafugaji kuunda vikundi na mabaraza ya kuendesha majosho ya kuogeshea mifugo  ili dawa zinapowafikia wasimamie zoezi la uogeshaji wakisaidiwa na wataalamu katika uchanganyaji wa dawa kwa usahihi.

Mbali na mambo mengine, Kikao hicho pia kilizungumzia namna ya kutenga maeneo ya malisho na kuboresha nyanda za malisho na kudhibiti magonjwa ya mifugo.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...