Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) imefanikiwa kuwadhibiti makundi ya nzige yaliyovamia wilaya za Longido na Simanjiro kwa kuwaua kwa kutumia ndege maalum iliyonyunyizia kiuatilifu kwenye maeneo ya mapori walipovamia.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa katika kijiji cha Kimokouwa wilaya ya Longido wakati Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliopotembelea kukagua maeneo ambayo yalikuwa makazi ya nzige wa jangwani mara baada ya kazi ya upulizaji sumu uliofanywa na ndege maalum.
"Leo tumefanikiwa kuua makundi makubwa ya nzige wa jangwani kwenye wilaya za Simanjiro na Longido ambapo ndege maalum imefanya kazi hiyo asubuhi na hapa tunashuhudia tayari nzige wameanza kufa na hakuna nzige aliyepo angani hadi muda huu (saa 6 mchana) ninapozungumza nanyi waandishi wa habari hapa Longido" Bashe.
Bashe alibainisha kuwa serikali mara baada ya kupata taarifa toka kwa wananchi kuwa eneo la wilaya ya Mwanga hapo mwezi Januari waliona nzige ilituma wataalam wa udhibiti wa visumbufu vya mimea toka TPRI kufuatilia nyendo zao na pia tarehe 16 Februari nzige wa jangwani waliingia Longido kupitia mpaka wa Namanga wakitokea Kenya hatua za mapema zilichukuliwa ili wasilete madhara.
Aliongeza kusema hadi nzige hawa wanaangamizwa leo hakuna eneo la kilimo ambalo mazao yake yameathirika na wadudu hao kutokana na hatua ambazo serikali kupitia wataalam wa wizara ya Kilimo imechukua.
"Hakuna eneo la kilimo ambalo limeathiriwa na nzige wa jangwani tangu waliporipotiwa kuingia nchini kwetu, hivyo wakulima na pia wafugaji wasiwe na hofu serikali ya awamu ya tano ipo madhubuti kuwakabiri ili nchi yetu iendelee kuwa na uhakika wa chakula" alisisitiza Naibu Waziri Bashe.