Wednesday, February 3, 2021

TAKUKURU yaokoa mamilioni ya NHIF

 


TAKUKURU mkoa wa Kagera imekabidhi zaidi ya shilingi milioni 10.3 kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), zilizolipwa kwa udanganyifu kwenye maduka mawili ya dawa za binadamu ambayo ni MK Pharmacy na EJU Pharmacy, baada ya kuwasilisha nyaraka za madeni wakidai kutoa huduma kwa wagonjwa.


Akikabidhi fedha hizo mbele ya mkuu wa mkoa wa Kagera, mkuu wa TAKUKURU wa mkoa huo John Joseph, amesema kuwa fedha zilizokabidhiwa ni sehemu ya shilingi milioni 304, ambazo taasisi hiyo imeziokoa kama madeni hewa, kutokana na nyaraka zilizotumika kubainika kuwa zimeghushiwa.


Joseph amesema kuwa ufuatiliaji umebaini kuwa madai hayo yalikuwa ni ya uongo, kwa kuwa fomu za NHIF zilizowasilishwa ziliandikwa na mtu aliyeitwa Dk. Frida Samwel, ambaye sio daktari na wala hakuwahi kuajiriwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa na hatambuliki.


Akizungumzia tukio hilo mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amesema kuwa serikali haitavumilia vitendo vyovyote vya ubadhirifu, na kwamba uchunguzi dhidi ya tukio hilo unaendelea na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...