Rais wa Iran Hassan Rouhani amesifu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki - ICJ kuwa inaweza kuisikiliza kesi ya Iran dhidi ya Marekani inayolenga kuondoa vikwazo, na kuutaja kuwa ni ushindi mkubwa kwa Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Shirika la habari la Iran - IRNA limemnukuu rais huyo wa Iran akiwapongeza watu wa Iran akisema huo ni mojawapo ya maamuzi kadhaa ya ushindi ambayo serikali imepata dhidi ya Marekani katika mahakama hiyo.
Mahakama hiyo ya juu kabisa ya Umoja wa Mataifa ilisema jana kuwa inaweza kusikiliza malakamiko ya Iran ya kutaka iondolewe vikwazo ilivyowekewa tena na Marekani wakati wa utawala wa Donald Trump.
Mawakili walioiwakilisha Marekani katika vikao vya mwaka jana walisema kesi hiyo inapaswa kutupiliwa mbali kwa sababu mahakama hiyo ya The Hague haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo, madai ambayo yamekataliwa.