MTU anayedaiwa kuwa ni kinara wa usafirishaji wa wahamiaji haramu, David Kapangala (31) na wenzake watatu wamekamatwa jijini hapa kwa kosa la kuwahifadhi na kuwasafirisha wahamiaji haramu kutoka nchi mbalimbali.
Akizungumza juzi jijini hapa Kamishina wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mwanza, Bahati Mwaifuge alisema watu waliokamatwa ni wahamiaji haramu 25, mmoja akiwa ni raia wa Kenya, 13 ni wanawake ambao ni raia wa Burundi, watu wengine 11 ni raia wa Ethiopia wakiwemo watanzania wanne.
Alisema wahamiaji hao haramu wakiwemo wa Ethiopia walikutwa wamehifadhiwa kwenye nyumba katika mtaa wa Majengo Mapya katika Kata ya Mkolani na watanzania hao.
"David na wenzake hawa watatu tulikuwa tunawatafuta siku nyingi, baada ya kufika anapoishi na kufanya upekuzi tuliwakuta watu wengine 11 wakiwa juu ya dari ambao ni raia wa Ethiopia," alisema.
Akizungumza mara baada ya kukamatwa kwa watu hao, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella aliwataka wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya kuhifadhi na kuwasafirisha wahamiaji haramu kwa madai kuwa ni kinyume na Sheria za nchi na za kimataifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Mapya iliyoko katika Kata ya Mkolani Ramadhani Musabi aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la polisi wanapoona kuna watu ambao sio watanzania.