India na China zimekubaliana kuondoa wanajeshi wa kila upande kutoka eneo la mpaka wa pamoja uliopo magharibi ya safu za milima ya Himalaya hatua inayomaliza miezi kadhaa ya mvutano na makabiliano kuhusu eneo hilo linalozozaniwa.
Waziri wa Ulinzi wa India, Rajnath Singh ameliambia Bunge la nchi yake kuwa mkataba huo kuhusu eneo la ziwa Pangong Tso umefikiwa baada ya duru kadhaa za mazungumza baina ya makamanda wa jeshi na wanadiplomasia wa mataifa hayo jirani.
Wiraza ya Ulinzi ya China tayari ilitangaza jana Jumatano kuwa wanajeshi wa mataifa hayo mawili yenye silaha za nyuklia wameanza kuondoka kutoka mwambao wa ziwa Pangong jana Jumatano.
Mvutano baina ya mataifa hayo mawili ambao wakati fulani ulishuhudia makabiliano ya kijeshi ulianza mapema Aprili mwaka uliopita baada ya India kusema wanajeshi wa China walivuka mpaka na kuingia kwenye eneo la Ladakh ambalo ni sehemu ya himaya yake.
Source