Wafanyakazi watano wa benki ya NMB wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Tanga wakituhumiwa kuiibia benki hiyo Sh1.2 bilioni.
Washtakiwa Erick Olomi, Christopher Kilemera, Joakim Carls, Edward Laswai na Beatrice Mathew wanadaiwa kuwa kila walipotakiwa kuweka fedha katika mashine za kutolea fedha (ATM), waliweka kiasi na nyingine waligawana.
Wamesomewa mashtaka yao leo Jumatano Januari 20, 2021 mbele ya hakimu mwandamizi, Kassim Matembele
Akiwasomea maelezo ya mashtaka yao mwendesha mashtaka wa Serikali, Pius Hilla amedai washtakiwa walishirikiana kwa pamoja kumwibia mwaajiri wao katika tawi la Mkwakwani mkoani Tanga.
Amesema walipanga na kutekeleza hujuma yao kati ya Septemba 1, 2013 na Februari 28, 2014.
Akieleza namna walivyoiba, mwendesha mashtaka huyo amesema walikuwa wakipunguza kiasi cha fedha kinachowekwa katika ATM.
"Mathalani ilitakiwa kila siku ATM ziwekwe Sh80 milioni lakini wao walikuwa wanaweka Sh60 milioni zilizobaki yaani Sh20 milioni walikuwa wanagawana wote watano," amesema.
Amesema kwa kuwa walikuwa wakiiba fedha hizo mara kwa mara wamekutwa na mali na utajiri usioendana na vipato vyao, kumtaja Erick kuwa alikutwa na magari, nyumba pamoja na viwanja.
Washtakiwa wote wameweka mawakili wa kuwatetea. Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Alhamisi Januari 21, 2021 na washtakiwa wamerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana.
