Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewahimiza wapiganaji wote wa kigeni na mamluki kuuondoka Libya ifikapo Jumamosi kama ilivyowekwa katika mpango wa kusitisha mapigano uliosainiwa Oktoba 23 na pande zinazohasimiana baada ya miaka mingi ya mapigano kuligawa mara mbili taifa hilo la Afrika Kaskazini.
Guterres pia ameihimiza serikali inayotambulika na Umoja wa Mataifa yenye makao yake katika mji mkuu Tripoli, magharibi mwa Libya, na wanajeshi wa kamanda Khalifa Hifter anayedhibiti mashariki na kusini mwa nchi, kuendeleza azma yao ya kupata suluhisho la kudumu la kisiasa kwa mgogoro huo, kutatua masuala ya kiuchumi na kupunguza hali ngumu ya kibinaadamu.
Katika ripoti iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Guterres ameukaribisha mpango uliofikiwa na Jukwaa la Mazungumzo ya Kisiasa la Libya, wa kuandaliwa uchaguzi wa rais na bunge Desemba 24 mwaka wa 2021.
