Monday, January 4, 2021

Manara Afunguka ya Mkude "Hatujamfukuza Bado ni Mchezaji Wetu Anapitia Changamoto"




MSEMAJI wa klabu ya Simba, Haji Manara, leo Januari 04, 2021, amezungumza na wanahabari kuelekea mechi yao kubwa iliyobeba hatma yao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe, itakayochezwa Januari 06, mwaka huu katika dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Manara amesema suala la mchezaji mwandamizi wa klabu hiyo, Jonas Mkude, bado lipo kwenye kamati ya nidhamu ya klabu, lakini ijulikane tu kuwa mpaka sasa ni sehemu ya Simba SC hajafukuzwa kazi, amepitia changamoto kama mfanyakazi mwingine kokote.

"Mkude ni mchezaji wa Simba SC. Jambo lake lipo kamati ya maadili. Mkude hajafukuzwa Simba SC. Bila shaka yoyote baada ya kamati atarejea klabuni. Huyu ndiye mchezaji mwandamizi ndani ya Simba kwa miaka 10," alisema.


Kuhusu maandalizi na mikakati ya Simba kuelekea kwenye mchezo wao na FC Platinum, Manara amesema yanakwenda vizuri, mechi yao iko palepale baada ya kupokea barua kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambao wameridhia mchezo ubakie muda uleule saa 11:00 jioni huku akibainisha viingilio kuwa ni Tsh 7,000.



"Tuliposema WIDA (War In Dar) hatukuwa na maana hasi, ni mapambano ya uwanjani kuhakikisha tunashinda na kuvuka kwenda hatua ya makundi na jana nimepokea simu kutoka kwa kiongozi wa timu moja pinzani anaulizia hii WIDA, nikasema yes ujumbe umefika.


"Hakuna namna Simba itakosa ubingwa wa #VPL mwaka huu, kwa hiyo watu wanapotaka itolewe tutachukua tena ubingwa na tutashiriki sisi wao watabaki hapa, kama huwezi kutushangilia baki nyumbani acha kupitapita sijui unashangilia Wazimbabwe.


"Katika kila Watanzania kumi kati yao saba wanashabikia Simba na unaweza kuona kupitia idadi ya mashabiki uwanjani ni takribani miaka kumi sasa Simba ndiyo timu inayojaza zaidi, hivyo tunaomba mashabiki mwendelee kuja kuwapa nguvu wachezaji.


"Simba siyo timu ya wananchi wala wazalendo wala yeyote yule, ni timu ya watu, nguvu yetu ipo katika watu na tumekuwa tukishinda mechi zote mashabiki wanapojitokeza, tulishinda dhidi ya Al Ahly, AS Vita na wengine, hivyo Jumatano Wazimbabwe hawatoki," amesema.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...