Sunday, October 25, 2020

Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi jimbo la Masasi mjini wala viapo vya uadilifu



Na Hamisi Nasri,MASASI  

WASIMAMIZI wasaidizi wa uchaguzi 628 pamoja na makarani waongozaji wa wapiga kura 242 wa jimbo la Masasi mjini wamekula kiapo cha uadilifu pamoja na kuepuka kufungamana na itikadi ya vyama vya siasa watakapokuwa wakitimiza majukumu ya Msimamizi. 


Wasimamizi hao na Makarani wamekula kiapo hicho mwishoni mwa wiki wilayani Masasi mkoani Mtwara mbele ya Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Masasi mjini ambaye pia ni mkurugenzi wa halmashauri ya mji Masasi,Gimbana Ntavyo, sambamba na kupatiwa mafunzo maalumu kwa ajili ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majumu yao.


Akifungua mafumzo hayo,Msimamizi wa uchaguzi huyo alisema wasimamizi hao wanapaswa kutenda haki sawa katika kusimamia majukumu yao ya kuwahudumia wapiga kura wanaofika katika vituo vya kupiga kura kwa ajili ya kupiga kura kwa amani na utulivu.  


Alisema wasimamizi hao ni kiungo muhimu kinachounganisha mawasiliano kati ya mpiga kura na msimamizi msaidizi kwenye kituo hivyo iwapo wakitekeleza wajibu wao kikamilifu zoezi upigaji
litafanyika bila ya malalamiko yoyote.

Ntavyo alisema kuwa kazi ya usimamizi itahitaji unyenyekevu na busara hivyo wanapokwenda kusimamia upigaji kura kwenye vituo vya kupiga kura lazima busara iwe mbele zaidi.

" Leo mmekula kiapo cha uadilifu hapa hivyo tunaomba mkaifanyike kwa kuzingatia kiapo chetu mlichoapa," alisema Ntavyo 

Alisema kuwa ili uchaguzi uwe na utulivu unagusa wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo hivyo nafasi yenu ni muhimu katika uchaguzi.

Aidha,Msimamizi huyo wa jimbo la Masasi alisema kuwa tayari maandalizi ya kuelekea katika uchaguzi oktoba 28 na kwamba baadhi ya vifaa kwa ajili upigaji kura vimeshavika.

Alisema anatoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya upigaji kura kwa ajili ya kupiga kura na kwamba anawatoa hofu wananchi kuwa uchaguzi huo kufanyika kwa utulivu.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...