Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Wanawake wa kata ya Kizota Jijini Dodoma wamepatiwa mafunzo ya ujasiliamali mbalimbali ili kupanua biashara zao na kujipatia mahitaji ya muhimu pasipo kutegemea wanaume zao.
Akizungumza wakati wa semina hiyo afisa habari wa jukwa la uwezeshaji Wanawake kiuchumi Mkoa wa Dodoma, bi Merry Mabhaya, amesema lengo la semina hiyo kuwajengea uwezo wajasiliamali wadogo ili waweze kufanikiwa katika biashara na kuunda vikundi kulingana na biashara zao.
Amewataka wanawake kuacha kuwa akina mama wa nyumbani bali wachangamkie fulsa zilizopo katika kuboresha biashara zao za ujasiliamali hasa baada ya Serikali kuhamia Dodoma na kufungua fulsa nyingi za kiuchumi.
" Baada ya Serikali kuhamia Dodoma fulsa nyingi zimefunguka ndugu zanguni muache kuwa wamama wa nyumbani ujio wa watu kunahitaji vyakula kwa wingi, hata saluni tu watu watakuja kusuka" amesema Merry.
Amesema kupitia jukwaa hilo watawezesha vikundi mbalimbali kuundwa kisha kupata elimu ya namna ya kuendesha vikundi hivyo yote ni katika kumuinua mwanamke kiuchumi ili nao wasibaki nyuma.
"Tunataka wanawake wamiliki uchumi wao ili wafanikiwe lazima tusimamie na tuhakikishe wamepata elimu ya biashara na kuwa katika vikundi ili kupata mikopo" amesema.
Amewataka wanawake kila changamoto inapotokea wachukulie kama fulsa ili wanufaike kwa kubuni njia mbalimbali ili kujipatia kipato na kutaka kutengwa kwa siku maalumu ya kuuza na kuonyesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wanawake au wajasiliamali wa Kizota.
"Nitamshauri Diwani itengwe siku na eneo maalumu la wazi kwa wanawake wa Kizota kuonyesha bidhaa zao na kuuza ili watu watambue kuwa hii bidhaa inatengenezwa Kizota" amesema.
Kwa upande wake afisa uendelezaji biashara kutoka SIDO bwana Crispini Kapinga wakati wa uwasilishaji wa maada wakati wa semina hiyo amesema mjasiliamali lazima awe mgunduzi na mfumbuzi wa fulsa mbali mbali zinazopatikana eneo husika.
Aidha amewakata kujitofautisha na wengine katika biashara na sio kufanya biashara ya aina moja sehemu moja pasipokujitofautisha na wengine, na kusisitiza kabla ya kuanza biashara uwe na taarifa muhimu ya biashara hiyo.
Nae Diwani msitaafu na ambae pia ni Mgombea udiwani kata ya Kizota (CCM) bwana Jamal Ngalya, amewataka wanawake hao kutokuwa na woga katika kuomba mikopo ili waweze kuendesha biashara zao.
" Nduguzanguni msiwe waoga kukopa hakuna tajiri mkubwa hapa nchini ambaye hana mkopo na hakukopa na ninyi jitokezeni kuomba mikopo muwezeshwe katika ujasiliamali wenu" amesema Ngalya.
Amesema endapo atafanikiwa kuibuka na ushindi katika kinyang'anyilo hicho mapema atakutana na wanawake na wajasiliamali kwa ujumla na kuunda vikundi sambamba na elimu ya biashara kutoka kwa wawezeshaji pamoja na benki ili kutengeneza mtandao mkubwa kwa wajasiliamali kunufaika.