Na John Walter-Babati.
Wananchi wa Jimbo la Babati Vijijini wanamatarajio ya kutatuliwa kero ya miundombinu ya barabara na maji kutokana na ahadi ya mgombea ubunge wa jimbo hilo alipokuwa akiowaombea kura diwani wa kata ya Galapo Michael Naasi na Dk. John Magufuli mgombea Urais Ccm.
Akijinadi mbele ya wananchi waliojitokeza katika mkutano huo wa hadhara wa kufunga kampeni za Kunadi sera na ilani ya Chama Chama Mapinduzi uliofanyika katika kijiji cha Galapo kata ya Galapo, Mgombea Ubunge Jimbo hilo anaesubiri kuapishwa baada ya kupita bila kupingwa Daniel Sillo, alisema kuwa ilani ya Chama hicho imesheheni mambo mengi ikiwemo miundombinu ya barabara, Elimu, Maji na Afya.
Alisema kuwa miundombinu ikiwa bora inasaidia kukuza uchumi wa wananchi kutokana na shughuli za kimaendeleo ambazo zinakuwa zinafanyika katika maeneo ya vijiji au miji ya kibiashara hasa usafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali.
Amesema ilani ya Chama cha Mapinduzi imeendelea kutekelezwa kwa vitendo ambapo katika jimbo la Babati Vijijini lenye vijiji 102, Vijiji 84 tayari vinawaka Umeme na kubaki vijiji 18 pekee na kazi bado inaendelea ambapo lengo ni kufikisha umeme hadi kwenye vitongoji.
Sillo alisema kuwa jimbo hilo linakabiliwa na changamoto ya maji hivyo atahakikisha maeneo yote yenye changamoto hiyo na nyingine, anatafuta njia ya kuzitatua.
Amewataka wananchi kutochezea amani ya Nchi na Badala yake wawe Mabalozi Wazuri wa kutunza na kuenzi amani hiyo kwa kumchagua tena Dr. John Pombe Magufuli kuiongoza nchi ya Tanzania kwa miaka mingine Mitano.
Mgombea Udiwani kata ya Galapo Michael Naasi ameahidi kushirikiana na Mbunge kuwasemea wananchi katika vikao vya Baraza la Madiwani ili changamoto zilizopo zitatuliwe.