Benki ya NMB imepata ongezeko la asilimia 76 la faida kabla ya kodi kwa kipindi kilichoishia Septemba 30, 2020. Kwa miaka mitano sasa, Tanzania imeshuhudia ukuaji imara wa uchumi uliowezeshwa na sera thabiti za kiuchumi
za Serikali ya awamu ya Tano.
Maendeleo haya ya kiuchumi, mazingira rafiki ya kibiashara, pamoja na utekelezaji mzuri wa mikakati ya benki ya NMB ni sababu kuu zilizopelekea ongezeko hili la faida katika robo ya tatu ya mwaka 2020.
Katika kipindi hiki faida kabla ya kodi ya Benki ya NMB imepanda kwa 76% kutoka Shilingi bilioni 118 katika robo ya tatu ya mwaka 2019 hadi shilingi bilioni 208 mwaka huu, wakati faida baada ya kodi ikipanda kutoka shilingi bilioni 82 hadi shilingi bilioni 145 ambayo ni sawa na ongezeko la 77%.
Pia katika kipindi hiki, mkakati wa Benki ya NMB wa kukuza vyanzo vya mapato umejidhihirisha kwa ongezeko la
mapato yatokanayo na uendeshaji kwa 14% kutoka bilioni 527 katika robo ya tatu mwaka 2019 hadi bilioni 600
katika robo ya tatu ya mwaka huu (2020).
Katika kipindi hiki pia programu za Benki za kudhibiti gharama za uendeshaji na matumizi ziliimarishwa na kusababisha uwiano mzuri wa gharama na mapato kwa 52%. Vile vile, Benki ya NMB kama mwezeshaji mkubwa wa maendeleo na uchumi nchini, imeweza kukuza rasilimali zake kwa 15% kutoka shilingi trilioni 6.1 kipindi kama hiki mwaka jana hadi trilioni 7 katika robo ya tatu ya mwaka 2020; hili limesababishwa na ongezeko la amana za wateja kwa 15% na ongezeko la mikopo kwa wateja la 16%.
Benki yetu pia imepata mafanikio makubwa katika eneo la ukopeshaji kwa kupunguza tengo la mikopo chechefu
kwa asilimia 22 ukilinganisha na kipindi husika mwaka 2019. Kwa matokeo haya ya utekelezaji kwa kipindi hiki, Benki ya NMB imeendelea kuimarisha mtaji wake juu ya kiwango kilichowekwa kisheria na Benki Kuu ya Tanzania cha asilimia 12.5.
Hiki ni kiashiria muhimu sana kuthibitisha afya ya Benki ya NMB kuendelea na biashara yake kwa miaka mingi ijayo. Akitangaza matokeo ya robo ya tatu ya mwaka 2020 ya Benki hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alisema kuwa matokeo haya yamesababishwa na kukua kwa haraka kwa uchumi wa Tanzania, sera
wezeshi na mwendelezo wa ukuaji wa pato la taifa kwa miaka ya hivi karibuni kama ilivyodhihirishwa kwa nchi
yetu kuingia kwenye uchumi wa kati mwezi Julai mwaka 2020. Haya yote yamesababisha sekta ya kibenki kufanya
vizuri, ikiwemo Benki ya NMB.
Bi. Zaipuna alisema kuwa "utendaji mzuri wa kifedha wa Benki ya NMB mwaka wote wa 2020 ni kielelezo kizuri
cha ufanisi wa utekelezaji wa mikakati ya Benki, ubora wa wafanyakazi wetu na imani ya wateja wetu kuendelea kutumia huduma zetu za kibenki. Tunaendelea kuwashukuru wateja wetu, wanahisa wote na wafanyakazi wetu wote kwa matokeo haya chanya".
Ni katika muktadha huo, wiki iliyopita, benki ya NMB ilipata tuzo ya Benki Salama zaidi Tanzania kwa mwaka 2020
itolewayo na jarida la kimataifa la Global Finance la New York, nchini Marekani. Ushindi huu umepatikana miezi
kadhaa tangu jarida la Euromoney la London liitangaze Benki ya NMB kuwa Benki Bora Tanzania kwa miaka nane
mfululizo.