MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, atahakikisha anaendeleza sekta ya michezo ili kuona wanamichezo wanaimarika pamoja na kuikuza sekta hiyo kuwa imara zaidi.
Alisema serikali inawajibu mkubwa kuisaidia sekta hiyo, na atahakikisha anaisaidia kwa kila hali.
Akizungumza katika Mahojiano katika kipindi maalim cha Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), alisema sekta ya michezo sio burudani peke bali sekta hiyo inaweza kumuwezesha msanii kupata ajira.
Aidha alisema katika serikali ya awamu ya nane itakayoingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu kumalizika atahakikisha anaiangalia sekta ya michezo ili viwango vya michezo vizidi kuimarika zaidi.
Aidha alisema kuwa katika uongozi wake pia katika suala michezo atawahamasisha wafanyabiashara wakubwa wa Zanzibar kudhamini michezo nchini.
Alisema kumekuwepo kwa migogoro mbalimbali katika Vyama vya michezo jambo ambalo linaweza kuzoretesha michezo Zanzibar na kuahidi kutatua migogoro hiyo endapo akipewa ridhaa ya kuongoza Zanzibar.
"Nitahakikisha nawasirikisha wafanyabiashara wakubwa kwa kudhamini ligi kuu zote za Zanzibar na sio mpira wa miguu peke yake" alisema.
Pamoja na hayo, Dk.Mwinyi alisema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar atahakikisha serikali atakayoiongoza itahakikisha inatenga fungu maalum kwa ajili ya kukuza michezo, ili maendeleo ya michezo yaonekanwe Zanzibar.
Akizungumzia viwanda vya mpira alisema kuwa ataendeleza viwanja vyote vilivyoachwa na serikali ya awamu ya saba ikiwemo cha kitogani kwa kukikamilisha ili wananchi waweze kutumia kwa michezo mbalimbali.
"Nafahamu viwanja vipo na vimeimarika chini ya uongozi wa Dk. Shein, nami wananchi mukinipa ridhaa nitahakikisha kuwa viwanja navimalizia ili musipate shida ya kutafuta viwanja kwa ajili ya michezo" alisema.
Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alisema endapo kila mmoja atatimiza majukumu yake kwa kuona changamoto zote zinazoikabili sekta ya michezo kwa viwango cha hali ya juu.
Dk.Mwinyi alisema lazima kuwe na viwanja vya michezo katika maeneo yote ambayo wananchi wanaishi ukianzia shehia, wilaya na mikoa.
"Tusipokuwa na viwanja vya michezo huwezi kuibua vipaji kwa hivyo hilo ni jukumu la serikali zote kuanzia chini mpaka juu kuhakikisha kwamba viwanja vinakuwepk vyenye kiwango ili kuendeleza michezo tulokuwa nayo," alisema.