Saturday, June 6, 2020

Uchaguzi Mkuu 2020: Rungwe atangaza ‘kutembeza bakuri’

KAMATI Kuu ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) nchini Tanzania, kimetangaza kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, huku kikitoa wito kwa vyama vyengine vitakavyohitaji kushirikiana nacho, kufanya majadiliano.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi  tarehe  6 Juni 2020, na Hashim Rungwe, Mwenyekiti wa Chaumma, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kutoa maazimio ya kikao cha kamati kuu.

Rungwe amesema, hivi karibuni Chaumma itatoa ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu za wanachama wake watakaohitaji kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo.

"Muda si mrefu tutatoa ratiba ya kuchukua na kurudisha fomu katika nafasi yoyote," amesema Rungwe.

Wakati huo huo, Rungwe amesema Chaumma imekamilisha kuandaa ilani yake ya uchaguzi na kwamba kiko katika mchakato wa kuiwasilisha katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

"Ilani ya uchaguzi imekamilika, iko katika mchakato wa kwenda kwa msajili wa chama. Muda ukifika tutainadi kwa wananchi na itapatikana kwa mdau yeyote," amesema Rungwe.

https://youtu.be/Js7K96Q9bgM

Aidha, Rungwe ameomba wananchi wenye mapenzi mema na chama hicho, kuchangia fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kampeni.

"Chama kinaendelea kutafuta wafadhili ili kiweze kupata fedha za kampeni. Milango iko wazi kwa mtu kukichangia kiasi chochote cha fedha, tunahitaji fedha za kutosha kufanya kampeni," amesema Rungwe
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...