KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amesema amewashangaa viongozi wa upinzani ambao walikuwa wakikosoa namna mbalimbali ambazo Rais Dk John Pombe Magufuli alizokuwa akizichukua kushughulikia tatizo la ugonjwa wa Covid-19.
Polepole ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM Lumumba jijini Dar kwa ajili ya kutoa shukrani mbalimbali kwa Watanzania na wahudumu ambao walikuwa mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Polepole amesema, viongozi hao wa upinzani hususan Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe walikuwa wakiitaka Serikali ifungie baadhi ya mikoa ambayo ina maambukizi makubwa bila kujua kufanya hivyo kungekwenda kuwaathiri Watanzania wengi zaidi wa kipato cha chini.
"Wako watu hapa Tanzania hasa kutoka vyama vya upinzani, walikwenda mbele wakasema, baadhi yao si wote. Wakasema tuufunge mkoa wa Dar es Salaam, tufunge Arusha…halafu tukifunga tutakula wapi? Hivi kweli Serikali ingeweza kutulipa mishahara?" alisema Polepole.
Alisema badala yake, Rais alielekeza zaidi watu kujilinda kwa kuchukua hatua zinazoelekezwa na wataalam wa afya pamoja na kutumia tiba mbadala.
"Rais wetu akasema msisahau mbona tuna mbinu nyingi tu hapa za asili wala si uganga? Kuna kujifukiza kula tangawizi, kula vyakula ambavyo vinaongeza kinga ya mwili, watu walipokea kwa muitikio mkubwa sana.
"Hivi Zitto anaposema tufungiwe yeye si ana mshahara. Vipi kuhusu mama lishe? Akatoka Mbowe, kiongozi wa kiimra kwelikweli, anamuambia kila mbunge wake kwamba mtakaa nyumbani siku 14 wao wakafanya kwa sababu wana mishahara, hawafikirii watu wa chini tena wanasahau hiyo mishahara yenyewe inatoka Serikalini," alisema.
Polepole aliwataka Watanzania kwa kuwa nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, wawapime na kutowachagua viongozi hao wa upinzani ambao walikwepa kukaa mstari wa mbele wakati wa mapambano dhidi ya Corona.
"Tunawapongeza wabunge wa CCM waliosimama imara katika mapambano ya Corona, na kwa vile tunaelekea kwenye uchaguzi basi hata wananchi watawapima. Viongozi waliokimbia vita wanyimwe kura," alisema Polepole.
Aidha, Polepole alisema CCM inatoa shukrani kwa kila mtu ambaye kwa namna moja au nyingine alihusika katika kuujenga uchumi wa nchi katika kipindi hiki cha Corona.
"Chama kinatoa shukrani kwa Watanzania wote, asante wakulima wa Tanzania. Mliendelea kulima malimao, maparachichi, tunawashukuru sana wafanyabiashara na wajasiriamali na wengineo…" alisema Polepole.
Aliitaka Wizara ya Afya Meandeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kuendelea kutoa elimu ya namna bora ya kutumia tiba mbadala ili watu waweze kujua vitu vya kuchanganya ili kuweza kutibu dalili za ugonjwa huo na ili kila Mtanzania akiwa nyumbani, akisikia koo linawasha ajue anatakiwa kuchanganya nini na nini kujitibu.
Polepole alimaliza kwa kuzungumzia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ambapo aliwataka wana-CCM mbalimbali wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali, kuacha kufanya hivyo kabla ya wakati.
"Kuhusu suala la uchaguzi Mkuu uliopo mbele yetu, chama kinaendelea kusisitiza tutumie muda huu kufuata katiba ya CCM na kanuni, wanaofanya vurugu kwenye majimbo, kata, walioanza kampeni kabla ya wakati hawatapewa nafasi ya uongozi," alisema Polepole na kuongeza.
"Umepewa kazi moja, hujaikamilisha unakwenda kuvuruga kabla ya muda. Wapo wanaosema wametumwa na viongozi wa juu, waongo. Hakuna aliyewatuma.
"Chama kimeandaa kituo. Nitawatangazia namba ya WhatsApp ambayo watu watatutumia taarifa. Tutazifanyia kazi tukikubaini umeanza kampeni kabla ya wakati tutakushughulikia na hata ukihama, bado tutakushinda hukohuko utakapohamia."