Tuesday, April 7, 2020

Waziri Wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga Amtembelea Waziri Mkuu Msaafu Mhe Mizengo Pinda, Nyumbani Kwake Jijini Dodoma

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 7 Aprili 2020 amemtembelea Waziri Mkuu Mstaafu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa Mhe Mizengo Peter Pinda nyumbani kwake eneo la Zuzu Jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo Waziri Hasunga amempongeza Mzee Pinda kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya kilimo hususani katika kilimo cha mbogamboga na matunda kupitia kitalu nyumba (Green Houses) ambapo amesisitiza umuhimu wa uwekezaji huo kwa wakulima wa maeneo jirani kujifunza mbinu bora za kilimo kupitia yeye.

Pamoja na kutembelea ujenzi wa Vitalu nyumba kadhalika Waziri Hasunga amejionea uwekezaji mkubwa wa ufugaji wa kisasa wa samaki.

Akizungumza shambani hapo Waziri Mkuu mstaafu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mhe Mizengo Peter Pinda amepongeza juhudi za Wizara ya Kilimo kuanzisha mchakato wa kuanzishwa kwa Sheria ya Kilimo itakayotoa suluhisho la changamoto zinazomkabili Mkulima na Sekta hiyo kwa ujumla itakayopelekea kuunganisha Bodi za mazao ili kuwa na mamlaka za mazao.

Kadhalika Mhe Pinda amesema kuwa kuna ulazima wa kuendelea kusimamia kwa weledi sekta ya Ushirika nchini kwani huo ndio umoja pekee unaowaunganisha wakulima na kuwa na nguvu ya pamoja hususani katika kupanga bei ya mazao yao kadhalika kuimarisha masoko ya mazao.

Kuhusu sekta ya Umwagiliaji Mhe Pinda amesema kuwa serikali inapaswa kuendelea kutilia mkazo zaidi kwani ndio njia pekee itakayomnusuru mkulima katika sekta hiyo ili kuondokana na kutegemea kilimo cha msimu wa mvua pekee.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...