SALVATORY NTANDU
Katika jitihada za kudhibiti uvunaji holela wa Misitu kwaajili ya Matumizi ya Mkaa wilayani Kahama Mkoani Shinyanga,Wakala wa huduma za Misitu (TFS) imeamua kujenga kiwanda Maalumu ili kuzalisha Nishati mbadala ya Mkaa unaotokana na pumba za Mpunga ambazo ni rafiki kwa mazingira.
Hayo yalibainishwa Jana na Meneja wa TFS wilaya ya Kahama, Ally Juma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Mradi wa utengenezaji wa Mkaa mbadala unaotarajia kuanza kuuzwa Mjini Kahama hivi karibuni.
Juma alisema kuwa Ujenzi wa kiwanda hicho umegharimu zaidi ya shilingi milioni 15 na kitakuwa kikizalisha tani tatu za Mkaa kwa siku ambazo zitakuwa na ubora wa hali ya juu kutokana na utengenezaji wake utakuwa wakitaalam zaidi ilikinganishwa na unaotokana na miti.
"Tutatumia pumba za mpunga, maranda ya mbao, magunzi ya mahindi,matenga ya miti yaliyoacha kutumika ambayo yanapatikana kwa wingi katika maeneo yetu ya Kahama hivyo tunaimani wakazi wa kahama watatuunga mkono pindi tutakapo anza kuuza mkaa huu"alisema Juma.
Aliongeza kuwa kiwanda hicho kitatumika kama chuo cha mafunzo ya wanachi kujifunza bure namna ya kutengeneza mkaa huo mbadala ambao ni rafiki wa Mazingira na kuwataka wawekezaji wilayani humu kuchangamkia fursa hiyo Muhimu.
"Nitoe rai kwa wafanyabiashara wa Kahama kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kutengeneza mkaa mbadala kwani Soko lipo na la uhakika,msiwe na hofu tumejipanga kuhakikisha wananchi wanachana na matumizi ya mkaa unaotokana na miti ambapo mpaka sasa tunaendelea na udhibiti wa watu wanaofanya biashara hiyo,"alisema Juma.
Sambamba na hilo Juma alifafanua kuwa katika Kanda ya Magharibi ya (TFS) serikali imesitisha shughuli zote za Uvunaji wa misitu ili kuwadhibiti watu wanaojihusisha na biashara ya mazao ya misitu kama vile mkaa,mbao na magogo ambao hapo awali zilikuwa zimeshamiri.