Na Abby Nkungu - Manyoni
Imeelezwa kuwa moja ya sababu ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kukumbwa na utapiamlo ni kutokana na baadhi ya wanaume kutokuwa na tabia ya kwenda kliniki na wenzi wao pindi wanapokuwa wajawazito ili wakapatiwe elimu na ushauri wa Lishe bora kwa Mama na Mtoto.
Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Muhalala katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida walisema kutokana na mfumo dume katika jamii nyingi ambapo baba ndiye mtoa uamuzi na mmiliki wa kipato katika familia,wengi wa wajawazito hushindwa kupata lishe bora kwa kukosa fedha za kununua mahitaji muhimu kulingana na ushauri wa kitaalamu.
Walisema kuwa hali hiyo husababisha lishe duni isiyokuwa na virutubisho muhimu kwa mtoto aliye tumboni na hata baada ya kuzaliwa hali ambayo walidai huendelea kutokana na wanawake wengi kuishi kwa kuwategemea waume zao ambao hawajui umuhimu wa lishe bora.
"Hebu fikiria kwa baba ambaye ni mlevi kupindukia, utoke kliniki eti ukamueleze unatakiwa upate lishe bora kwa afya yako na mtoto aliye tumboni, hawezi kukuelewa katu", alisema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mariam Bunku mkazi wa Muhalala Wilayani Manyoni.
Alieleza kuwa tatizo hilo ni moja ya sababu ya baadhi ya watoto kupata utapiamlo kutokana na lishe duni inayochangiwa na baadhi ya wazazi wa kiume kutojua umuhimu wala kuwa na elimu ya lishe bora.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanawake wanasema kuna haja kwa Serikali kutunga Sheria itakayowalazimisha wanaume kwenda na wenzi wao kliniki kabla na baada ya kujifungua.
Walidai kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza tatizo la utapiamlo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano iwapo akinababa, ambao ndio watoa uamuzi, watapata elimu na kujua umuhimu wa lishe bora kwa mama na mtoto.
Ofisa Lishe mkoa wa Singida, Teda Sinde anasema ukosefu wa lishe bora kwa mjamzito husababisha udumavu kwa mtoto aliye tumboni na hata baada ya kuzaliwa huathiri ukuaji wa ubongo na maungo ya mwili wake; hivyo kudumaza maendeleo ya ukuaji wake kwa ujumla.
Takwimu za utafiti wa kitaifa za mwaka 2018 juu ya hali ya lishe mkoani Singida zinaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia 5 ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo.
Kadhalika, utafiti huo unabainisha kuwa asilimia 27.9 tu ya watoto hao ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na asilimia 3 tu ya watoto walio chini ya miaka miwili ndio angalau hupata mlo unaokubalika katika tafsiri ya lishe bora.