Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona akizungumza wakati wa kufunga warsha ya MAMA RIKA mkoa wa Mwanza Aprili 25,2019.
*****
Tunataka Taifa la Tanzania liwe na watoto wanaozaliwa bila kuwa na Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU)!
Haya ni maneno ya Cecilia Yona ambaye ni Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii wa asasi ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) inayojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI na UKIMWI, wakati akifunga warsha kwa MAMA RIKA mkoa wa Mwanza iliyolenga kuwajengea uwezo kuhusu masuala mbalimbali ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI.
MAMA RIKA ni Waelimishaji wa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanaoishi na VVU ambao wanapata huduma za tiba na matunzo katika kliniki ya mama,baba na mtoto (RCH) ili kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Warsha hiyo ya siku mbili imemalizika Alhamis Aprili 25,2019 jijini Mwanza na kuhudhuriwa na MAMA RIKA 70,wauguzi, waratibu wa huduma ya afya ya uzazi,waratibu wa huduma za VVU na UKIMWI katika jamii mkoa wa Mwanza.
Afisa Miradi huyo wa Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona alisema ili kuwa na watoto wanaozaliwa bila maambukizi ya VVU katika taifa la Tanzania ni lazima akina mama wanaoishi na VVU wapewe elimu ya kutosha kuhusu namna ya kuzuia maambukizi wakati wa ujauzito, kujifungua na wakati wa kunyonyesha.
"Hatuwezi kupata watoto ambao ni Free From HIV (watoto wasio na HIV),bila akina mama kuwa na elimu,ndiyo maana AGPAHI tumewakutanisha MAMA RIKA ili tuwajengee uwezo juu ya masuala ya VVU na UKIMWI na namna ya kusaidiana kupitia uzoefu kutoka ujauzito mpaka watoto wanapopata kipimo cha mwisho cha uhakiki",alieleza Yona.
"Lengo la kuwa na MAMA RIKA kwenye vikundi ni kusaidia kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,hivyo tunaamini mama akielewa vizuri,akipata elimu ya kutosha na akafuatilia yale aliyoelekezwa mtoto hatapata maambukizi ya VVU",alisema.
"AGPAHI iko bega kwa bega kufanya kazi na MAMA RIKA,tunaamini kwamba huyu mama akijengewa uwezo vizuri kwa njia ya wataalamu na kufundishana wao kwa wao,wanapata nafasi kubwa ya kujifunza wenyewe kwa wenyewe kwa kutumia uzoefu walionao,yule ambaye ameshajifungua atamfundisha mjamzito, yule amemaliza kunyonyesha atamfundisha anayeanza kunyonyesha, kwa hiyo wanafundishana kwa njia ya uzoefu na elimu hiyo inakuwa sehemu ya maisha yao na kuwasaidia akina mama wengine",aliongeza Yona.
Yona alitoa wito kwa washiriki wa warsha hiyo kuwa mabalozi na wasimamizi kwa akina mama wengine ili watakaporudi wakawasaidie akina mama waliopo katika kitengo cha kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Hata hivyo MAMA RIKA walioshiriki warsha hiyo walisema hivi sasa suala la ubaguzi na unyanyapaa limepungua kutokana na watu wengi kupata elimu kuhusu VVU na UKIMWI na wengi kujiweka wazi wakibainisha kuwa kupata maambukizi siyo mwisho wa maisha.
Aidha walishauri elimu iendelee kutolewa zaidi kwa akina mama wajawazito wahudhurie kwenye vituo vya afya wafundishwe mambo muhimu badala ya kufuata maneno mtaani na kujinyanyapaa matokeo yake wanajifungua watoto wenye maambukizi.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Afisa Miradi huyo wa Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona akifunga warsha ya siku mbili ya MAMA RIKA mkoa wa Mwanza iliyofanyika katika ukumbi wa Gold Crest Hotel jijini Mwanza -Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Cecilia Yona akiwasisitiza washiriki wa warsha hiyo kuwa mabalozi kwa akina mama wengine wawape elimu ya kutosha kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI ili wazaliwe watoto wasio na maambukizi ya VVU.
Washiriki wa warsha wakiwa ukumbini.
Cecilia Yona akionesha kitabu cha mwongozo wa kuendesha vikundi vya akina mama wanaoishi na VVU wenye ujauzito na wanaonyonyesha kutoka kitengo cha kuzuia maambukizi ya toka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT).
MAMA RIKA,wauguzi, waratibu wa huduma ya afya ya uzazi na waratibu wa huduma za VVU na UKIMWI katika jamii wakionesha vitabu vya mwongozo wa kuendesha vikundi vya akina mama (PMTCT) baada ya kugawiwa wakati wa warsha hiyo. Kushoto ni Mwezeshaji wa kitaifa wa masuala ya Vijana,VVU na UKIMWI, Dkt. Happiness Wimile Mbeyela.
Washiriki wa warsha hiyo wakiwa ukumbini.
Awali,Mwezeshaji wa kitaifa wa masuala ya Vijana,VVU na UKIMWI, Dkt. Happiness Wimile Mbeyela akitoa mada kuhusu unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU.
Dkt. Happiness Wimile Mbeyela akisikiliza swali kutoka mmoja wa washiriki wa warsha hiyo.
Dkt. Happiness Wimile Mbeyela akisikiliza swali kutoka mmoja wa washiriki wa warsha hiyo.
Mwezeshaji katika warsha hiyo, Edwiga Zumba akitoa mada ukumbini.
Mwezeshaji katika warsha hiyo,Yahaya Isangula akiwasisitiza akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wenye maambukizi ya VVU kuendelea kuwa wafuasi wazuri wa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs).
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo akiuliza swali.
Mratibu wa huduma ya afya ya uzazi halmashauri ya wilaya ya Ilemela,Grace Kusaya akiwahamasisha MAMA RIKA kuwapa elimu akina wajawazito na wanaonyesha ili watoto wasipate maambukizi ya VVU.
Mratibu wa huduma ya afya ya uzazi halmashauri ya wilaya ya Misungwi, Flora Kuzenza akichangia hoja.
Kaimu mratibu wa huduma ya afya ya uzazi halmashauri ya wilaya ya Ukerewe, Laurencia Damas akizungumza ukumbini.
Picha ya pamoja washiriki wa warsha.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Soma pia : AGPAHI YAENDESHA WARSHA KWA MAMA RIKA MKOA WA MWANZA
Soma pia : AGPAHI YAENDESHA WARSHA KWA MAMA RIKA MKOA WA MWANZA