Sunday, March 24, 2019

Taarifa kwa Umma kutoka kwa SUMAJKT


Wabia wa Kampuni ya SUMAJKT Skyzone jana wamekagua eneo la Kiwanda cha taa za LED (Light Emitting Diode) kinachoendelea kujengwa chenye thamani ya zaidi shilingi za kitanzania bilioni 12 kinachojengwa katika Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa Mlalakuwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea kuona hatua za utekelezaji wa Ujenzi wa Kiwanda hicho, Makamu wa Rais wa kampuni ya Everlight Skyzone ya nchini China, Bw. Hassan Baalbaki ambaye ni mmoja wa wabia wa SUMAJKT Skyzone amesema kiwanda hicho kinachojengwa kitatumia teknolojia mpya ambayo bado haijaenea nchi nyingi za Afrika.
 
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Kanali Rajabu Mabele ambae ni mmoja wa wabia wa SUMAJKT Skyzone, amefafanua faida za kuwepo kwa kampuni hiyo hapa nchini, kuwa itasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa taa hizo ambazo kwa sasa zinaagizwa toka nje ya nchi. 
Kampuni hiyo ya ubia imeanzisha kiwanda hicho ambacho kitasaidia utekelezaji wa kauli mbiu ya Mh. Rais ya Tanzania ya viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Everlight Skyzone Tanzania Bw. Victor Madata amesema katika kuunga mkono juhudi za Mh. Rais Dkt John Magufuli juu ya adhma yake ya Tanzania ya Viwanda, watafanya mafunzo kwa watanzania ili kutoa fursa za ajira na ujuzi wa jinsi yakutengeneza taa hizo na kuziuza nje ya nchi.

Kuanzishwa kwa kiwanda hicho kitaendelea kutekeleza kifungu cha 7 cha sheria ya uratibu wa Ajira kwa wageni kinachomtaka kila mwajiri kuandaa mpango wa urithishaji wa ujuzi kwa wafanyakazi Watanzania kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wananufaika na ujuzi huo.

SUMAJKT Skyzone ni kampuni ya ubia kati ya SUMAJKT inayomiliki 49% na Everlight Skyzone inayomiliki 51% iliyoanzishwa mwezi Octoba 2018, Inatarajia kumaliza ujenzi huo  mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu na kuanza uzalishaji wa taa hizo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...