Sunday, February 3, 2019

Kipigo cha Simba Chamuibua Afande Sele


Kipigo cha pili mfululizo cha Simba katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika kimeendelea kuwachanganya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo huku hatma ya nafasi katika kundi lao ikiendelea kuwa mashakani.


Simba imefungwa mabao 5-0 na Al Ahly jana Jumapili na kufanya kuwa ni kipigo cha pili mfululizo katika michuano hiyo, baada ya kufungwa na AS Vita Club ya DR Congo, Januari 19.

Msanii mkongwe wa muziki wa Hip Hop nchini, Afande Sele ametoa maoni yake katika ukurasa wake wa Instagram kufuatia kipigo hicho, ambapo amesema kuwa sababu ya Simba kufaya vibaya licha kuwa na uwekezaji mkubwa ni kuendeshwa kienyeji.

"Wakati ule wanasimba wanafurahia ujio wa Mo wakiamini kwamba timu itakua bora kwa sababu itakua na mahela ya udhamini, sisi wengine tulikaa kimya tukisubiri kuona hayo mabadiliko ya uendeshaji wa timu atakaokuja nayo Mo ambayo tulitegemea angeitoa Simba katika uendeshwaji wa kikariakoo uliozoeleka na kuiendesha kitaalamu kama inavyotakiwa lakini kumbe Mweh", amesema.

"Chini ya udhamini mnono wa Mo, Simba imeendelea kuwatumia madalali wapiga dili walewale katika usajili wa wachezaji hadi benchi la ufundi. Simba pamoja na udhamini wa Mo lakini bado inasajili wachezaji magarasa kutoka nje ya nchi ambao hata timu zao za taifa haziwajui kabisaa na matokeo yake wanachukua wachezaji wa kuja kujaribiwa badala ya kuja kucheza, mfano katika hao 'mapro' wa Simba ukimtoa Kagere na Chama ni nani mwingine anaechezea timu yake ya taifa?", ameendelea kusema Afande sele katika maoni yake.

"Nakumbuka baada ya Simba kufungwa na Kagera sugar mbele ya Rais JPM, huyu mzee aliongea kiroho safi tu kwamba kwa wachezaji na uchezaji ule Simba inakwenda kutia aibu katika mashindano ya kimataifa labda ifanye usajili mkubwa wenye tija kitu ambacho bila shaka viongozi wa Simba na mdhamini wao walichukulia poa tu".

Kwa matokeo hayo, Simba imeendelea kusalia katika nafasi yake ya tatu ikiwa na alama tatu, huku kundi hilo likongozwa na Al Ahly yenye pointi 7, nafasi ya pili ikishikiliwa na AS Vita Club ikiwa na alama nne na JS Saoura ikiburuza mkia kwa alama 2.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...