Friday, August 24, 2018

MWANDISHI WA HABARI MATATANI KWA KUPOST FACEBOOK "PICHA YA POLISI" AKILEWA NA SARE SIMIYU


Mkuu wa jeshi la polisi nchini Simon Sirro.

Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linamshikilia mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru mkoani Simiyu, Constantine Mathias kwa kosa la kimtandao (cyber-crime).

Constantine anadaiwa kuweka picha ya askari polisi aliyekuwa akinywa pombe huku akiwa na sare za jeshi hilo kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Picha anazodaiwa kusambaza ni za askari polisi PC Neto Mahenge wa kituo cha polisi Mwamapalala.

Kwa mujibu wa Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu, Samwel Mwanga, mwandishi huyo alikamatwa jana akishutumiwa kwa kosa la kimtandao.

''Ni kweli mwandishi wa gazeti la Uhuru anashikiliwa na Jeshi la Polisi na wamemfungulia jalada la makosa ya kimtandao kwa kosa la kuzisambaza picha za askari polisi aliyekuwa anakunywa pombe akiwa na sare za jeshi hilo wa kituo cha Mwamapalala wilayani Itilima katika mitandao ya kijamii," alisema Mwanga.

Mwanga aliongeza kuwa kwa sasa uongozi wa klabu ya waandishi wa habari Simiyu unafanya utaratibu wa kumdhamini na taratibu zingine zitafuata baada ya mwandishi huyo kumtoa nje.

Kwa mujibu wa waandishi waliokuwapo eneo la tukio, mtuhumiwa yuko mikononi mwa polisi na tayari amechukuliwa maelezo yanayosubiri kusainiwa na Mwenyekiti au Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Simiyu ili aweze kupatiwa dhamana.

Waandishi hao wanaliomba Jeshi la Polisi kumwachia mwandishi huyo kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ni haki ya mtuhumiwa kupewa dhamana.

Akizungumza jana Agosti 23 Kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu, Deusdedit Nsimeki alisema Mathias alikamatwa, akahojiwa kisha akaachiwa.

"Anahojiwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na madai ya kujihusisha na vitendo vya rushwa. Nimeagiza achukuliwe maelezo na kuachiwa kwa dhamana akikamilisha taratibu na mahitaji ya kisheria," alisema Kamanda Nsimeki.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...