Siku chache baada ya Rais John Magufuli kuonesha kukwazwa na kiwango kidogo cha makusanyo ya mapato ya jiji la Dar es Salaamambayo alieleza kuwa yanazidiwa karibu mara mbili na ya jiji jipya la Dodoma, Meya waHalmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob ameibuka na kueleza kuwa Rais alipewa taarifa zisizo sahihi.
Rais Magufuli alieleza kuwa jiji la Dar es Salaam lenye watu zaidi ya milioni 5 lilikusanya Sh15 bilioni huku jiji la Dodoma lenye watu takribani milioni 2 likikusanya Sh24 bilioni na kuongoza.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Jacob alisema kuwa jiji la Dar es Salaam lilikusanya zaidi ya Sh 139 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 91.95 ya malengo iliyowekewa ambayo ni Sh 151 bilioni.
"Halmashauri zote za DSM walipanga kukusanya billioni 151,290,075,441 na wakafanikiwa kukusanya kiasi cha Billioni 139,118,756,519,90 sawa na asilimia 91.95. Swali ni Je, Billioni 139.118,756,519.90 ni ndogo kuliko billioni 24.4," alisema Jacob na kusisitiza kuwa kiasi hiki ndicho kilichochangiwa na watu milioni 5 wa mkoa wa Dar es Salaam waliotajwa.
Akizichambua baadhi ya halmashauri za mkoa huo, alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pekee ilipanga kukusanya sh16.4 bilioni lakini ilikusanya 16.8 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 102, hivyo ilivuka lengo.
Aliongeza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni katika mwaka jana wa fedha ilipanga kukusanya 31.6 bilioni na ilikusanya 29.7 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 94 ya malengo. Temeke ilipanga kukusanya Sh30.9 bilioni lakini ilikusanya Sh29.03 bilioni sawa na asilimia 94.
Halmashauri ya Ubungo ambayo anaiongoza, amesema ilikusanya Sh16 bilioni lakini ilikusanya Sh13.5 ambayo ni sawa na asilimia 81.8.
Akiendelea kumkosoa aliyempa taarifa hizo Rais, Meya huyo alisifu utaratibu aliouanzisha Rais Magufuli wa kushindanisha mapato ya Halmashauri zote nchini kwani utachagiza usimamiaji mzuri wa makusanyo ya mapato.
Boniface alikiri kuwa kuna mikono ya upigaji kwenye halmashauri za Dar es Salaam kama ilivyo kwa halhamashauri nyingine lakini akaeleza kuwa hata Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo anafahamu juhudi zinazofanywa na halmashauri hizo ambazo nyingi zinaongozwa na upinzani ikiwa ni pamoja na Jiji la Dar es Salaam likiwa chini ya Meya Isaya Mwita wa Chadema.