Sunday, August 19, 2018

KIGOGO WA CHADEMA AITAKA CHADEMA KUSUSIA CHAGUZI ZOTE


Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Profesa Abdallah Safari amekishauri chama hicho kususia chaguzi zote nchini na kudai kwanza tume huru ya uchaguzi.


Kauli ya Profesa Safari imekuja wakati Chadema ikiugulia maumivu ya kupoteza Jimbo la Buyungu ilililokuwa ikilishikilia kutokana na kifo cha Kasuku Bilago baada ya kuchukuliwa na CCM katika uchaguzi uliofanyika Agosti 12 na Christopher Chiza kuibuka mshindi.


Mbali na kupoteza jimbo hilo, Chadema na vyama vingine vya upinzani wamepoteza kata zote 77 za udiwani zilizonyakuliwa na CCM.


Uchaguzi huo umeibua hisia tofauti na hivi karibuni, Ubalozi wa Marekani nchini ulitoa ukisema uligubikwa na vurugu, ukiukwaji wa sheria za uchaguzi ikiwa ni pamoja na baadhi ya watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukataa kuwasajili wagombea kutoka vyama vya upinzani.


Marekani pia imelalamikia vitisho vya polisi dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani, watu kukamatwa kiholela bila kuwapo vibali vya ukamataji na kukandamizwa kwa uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni katika kipindi chote kuelekea chaguzi hizo.


Aidha, Chadema na ACT Wazalendo pia vikiilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) vikidai haikuvitendea haki.


Baada ya tamko hilo la Ubalozi wa marekani, NEC ilijibu ikisema uchaguzi huo haukua na waangalizi wa kimataifa na kuhoji ubalozi huo umetoa wapi taarifa hizo na hayo uliodai kuyaona ni kwa kutumia sheria ipi?


Kuhusu madai ya vurugu NEC ilisema kilichotokea Arusha ni vurugu mitaani mbali na maeneo ya vituo vya kupigia kura na kwa kuwa vurugu hizo zilisababisha jinai kufanyika, vyombo husika vinashughulikia.


Mbali ya NEC, CCM nayo iliijibu Marekani kupitia kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally ambaye aliitaka nchi hiyo kuzingatia uhuru wa Tanzania na kwamba uchaguzi huo ulizingatia sheria.


Pia Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakaluka alijibu madai hayo ya marekani akisema, "Polisi inamkamata mtu kwa kuzingatia sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai... sisi tunapokamata mtu hatuangalii kama anapiga kura au anafanya nini ilimradi tunashuku kuwapo kosa la jinai."


Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Profesa Safari aliyewahi kuandika kitabu kiitwacho 'Haja ya kuwa na Tume Huru ya uchaguzi ya Taifa Tanzania' alisema hata Chadema wakienda mahakamani na kushinda kesi, wataishia kupoteza katika uchaguzi. Hata hivyo, alisema mawazo yake bado hayajakubalika ndani ya chama hicho.


"Nimewashauri sana wenzangu Chadema, tupambane kudai tume huru, lakini imeshindikana. Kwa sababu hata hizi kesi tukishinda, tutaishia kudhulumiwa ushindi, sasa unafanya nini?" alisema.


Profesa Safari aliyewahi kuwa kiongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) alisema, "Tangu nilipokuwa CUF nimegombana na Profesa Ibrahim Lipumba kwa sababu hiyohiyo. Nilimwambia tususie chaguzi zote, yeye akasema tutakuwa tumemwachia nguruwe shamba la muhogo. leo CUF iko wapi?"


Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema Dk Vincent Mashinji alipoulizwa kwa siku kuhusu madai hayo alisema hajawahi kusikia kitu hicho, "Tuko viongozi wengi kwenye chama, sijui amemwambia nani… Kwa sababu yule ni kiongozi mkuu wa chama na ni mtoa maamuzi."


Maulid Kambaya, ambaye ni mkurugenzi wa habari wa CUF upande wa Profesa Lipumba alisema hawana mpango wa kujitoa kwenye uchaguzi akisema unawasaidia kukusanya ushahidi wa malalamiko yao kuhusu unyanyaswaji.


"Tuliwahi kufanya hivyo Januari 21, 2001 yaliyojitokea kila mtu anajua. Kwa sasa haiwezekani kususia. Kwanza tumezuiwa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, kwa hiyo zikitokea chaguzi ndiyo tunapata nafasi ya kuhutubia wafuasi wetu," alisema.


"Siyo sisi tu, hata Chadema na ACT waliwahi kususia lakini sasa wamerudi. Lengo ni kupata ushahidi wa jinsi tunavyonyanyaswa. Malalamiko yetu makubwa ni kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo imebaki kama bodi tu, lakini injibi yote iko kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya."


Mbali na uchaguzi wa Agosti 12, Chadema na vyama vingine vya upinzani vililalamikia uchaguzi wa Februari 17 katika majimbo ya Kinondoni na Siha.


Katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM jimbo la Kinondoni aliyejitoa CUF, Maulid Mtulya alishinda huku mgombea wa CCM aliyejitoa Chadema katika jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel akishinda.


Kabla ya chaguzi hizo, Chadema ilisusia chaguzi za marudio katika majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea uliofantyika Januari 13, 2018.

Na Elias Msuya, Mwananchi.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...