Friday, August 3, 2018

kibali cha DPP chasubiriwa Kesi ya kina Aveva

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kugushi na utakatishaji wa fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na wenzake umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wameshafanyia marekebisho hati ya mashtaka ya kesi hiyo na kwa sasa wanasubiria kibali cha DPP ili iweze kuendelea.

Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro, ameeleza hayo leo, Agosti 3.2018 Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba kesi hiyo ilipokuja  kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (PH).

Wakili Kimalo ameeleza kuwa, tayari wameshatimiza amri ya mahakama ya kubadilisha hati ya mashtaka na kuwaondoa watuhumiwa wawili waliotakiwa kuondolewa ili kesi ya msingi iweze kuendelea.

Aliongeza kuwa, kwa kuwa hati hiyo mpya ya mashtaka inatakiwa kupata kibali cha DPP ili Mahakama ya Kisutu iweze kuendelea wameirudisha kwake kwa ajili ya kupata kibali hicho na kuongeza kuwa kwa sasa DPP hayupo hivyo wanaiomba mahakama itoe ahirisho fupi kwa ajili ya kusubiria kibali hicho.

Naye Wakili wa Utetezi Nehemiah Nkoko amedai kuwa ni kweli amefuatilia na kubaini kuwa PH ipo tayari lakini kinasubiriwa kibali hicho ili washtakiwa hao wasomewe mashtaka mapya.

Aidha ameunga mkono ombi la kuahirisha kesi hiyo lililotolewa na upande wa mashtaka kutokana na kukosekana kwa kibali hicho.

Hakimu Simba amemtaka upande wa mashtaka kufuatilia kibali hicho kwa DPP kipatikane haraka kwani kesi hiyo imekwisha kaa muda mrefu.

Kesi hiyo sasa itatajwa Agosti 10.2018

Aveva anashtakiwa pamoja na Makamu wake Godfrey Nyange Kaburu. 

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi,  kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji fedha haramu.  

Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...