Tuesday, July 29, 2025

Airtel Africa Yatangaza Matokeo Mazuri ya Robo ya Kwanza 2025


Airtel Africa imetangaza matokeo bora kwa robo ya kwanza iliyoishia Juni 30, 2025, ikionesha ongezeko la wateja wanaotumia huduma za intaneti na Airtel Money katika nchi mbalimbali za Afrika.

Afisa Mtendaji Mkuu, Sunil Taldar, amesisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya utekelezaji wa mkakati thabiti unaolenga kuboresha huduma kwa wateja na kuwekeza katika teknolojia mpya kama vile Airtel Spam Alert ili kuhakikisha usalama na kuimarisha imani ya mtandao.

"Tunaendelea kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuunganisha jamii nyingi zaidi barani Afrika," amesema.

Airtel Africa imeshukuru wafanyakazi na wadau wote kwa mchango wao katika kuhakikisha ukuaji endelevu na huduma bora kwa wateja nchini Tanzania na kwingineko.

 

Sunday, July 27, 2025

RC Manyara awapiga marufuku viongozi kujilimbikizia mali


Na John Walter-Babati

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amepiga marufuku viongozi na watumishi wa umma mkoani humo kujilimbikizia mali ambazo wanashindwa kuziendeleza, akieleza kuwa hali hiyo inaziba fursa kwa wananchi wengine kupata maendeleo.

Sendiga alitoa agizo hilo Julai 24, 2025, wakati wa hafla ya kumkabidhi mkandarasi eneo la ujenzi wa stendi ya mabasi, barabara za lami na mitaro katika stendi ya muda ya Makatanini, mjini Babati.

Amesema baadhi ya viongozi wamekuwa wakijipatia mali nyingi – zikiwemo vibanda – lakini wanashindwa kuviendeleza, hali inayokwamisha matumizi bora ya rasilimali zilizopo kwa manufaa ya jamii.

"Marufuku kujilimbikizia vibanda vitakavyojengwa katika stendi hii mpya. Kila mmoja apate kibanda kimoja ili kutoa nafasi kwa wengine, wale waliopo sasa kwenye stendi ya muda wapewe kipaumbele kwa gharama nafuu," alisisitiza.

Aidha, alibainisha kuwa kukamilika kwa stendi hiyo kutachangia kukuza uchumi wa wananchi wa Babati na kuondoa kero ya vumbi ambalo limekuwa likisababisha maradhi kwa watumiaji wa stendi hiyo kwa muda mrefu.

Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa Mkoa alimwagiza mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni ya Wesons Engineers, kuhakikisha hakuna visingizio vya kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo na kwamba kazi ifanyike kwa ubora na ikamilike kwa wakati.

"Tunataka kuona thamani ya fedha kwenye kila senti, hakuna sababu ya kuchelewa au kutoa visingizio. Ujenzi uende kwa kasi na ubora unaotakiwa," alisema Sendiga.

Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 15 kwa gharama ya shilingi bilioni 19.996, na unahusisha ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 4.7 pamoja na mitaro ya kupitisha maji yenye urefu wa kilomita 8.15.

Ujenzi wa stendi hiyo mpya unatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa sekta ya usafirishaji mjini Babati na kuchochea biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Wednesday, July 16, 2025

‎Mwenge wazindua daraja la watembea kwa miguu Tipri Mbulu. ‎


Na John Walter -Mbulu

Mradi wa ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu Tipri lililoko kata ya Gehandu, halmashauri ya mji wa Mbulu, umeleta afueni kubwa kwa wananchi takribani 3,995, wakiwemo wanafunzi ambao sasa wanaweza kuhudhuria masomo bila usumbufu wakati wote wa mwaka.

‎Akisoma taarifa ya mradi huo wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, Meneja wa TARURA wilayani Mbulu, Mhandisi Nuru Hondo, amesema kabla ya kujengwa kwa daraja hili, wanafunzi walikuwa wanakwamishwa na mvua kwa takribani miezi saba kila mwaka, jambo lililoathiri mahudhurio na maendeleo yao kielimu.

‎Ameeleza kuwa daraja hilo kutokana na uimara wake linaweza kudumu kwa miaka 70.

‎Mwenge wa Uhuru umepokelewa wilayani Mbulu kwa ziara ya kukagua, kutembelea, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali yenye thamani ya Shilingi bilioni 44, ikiwemo miradi ya afya, miundombinu ya barabara na miradi mingine ya maendeleo.

‎Miongoni mwa miradi hiyo ni daraja hili la Tipri, ambalo linaunganisha vijiji vya Tsawa na Tipri.

‎Kukosekana kwa daraja hilo kwa muda mrefu kulisababisha wananchi kupata changamoto kubwa katika kupata huduma muhimu, hasa wakati wa mvua ambapo mto huo ulikuwa unakuwa kikwazo kikubwa. Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 158.9.

‎Akizungumza kwenye eneo la mradi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, ameipongeza halmashauri ya mji wa Mbulu kwa ubunifu na utekelezaji wa mradi huu muhimu.

‎Vilevile, ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama kwa usimamizi mzuri wa fedha za mradi.

‎Mwenge wa Uhuru mwaka huu unaendelea na kaulimbiu isemayo: ‎"Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu."

Mwenge wa uhuru wazindua Mradi wa nishati mbadala Manyara Girls Sekondari



Na John Walter -Babati

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ali Ussi, amezindua mradi wa nishati mbadala katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Manyara wenye thamani ya shilingi milioni 21.9.

‎Mradi huo unalenga kurahisisha upikaji wa chakula kwa wanafunzi pamoja na kutunza mazingira kwa kupunguza ukataji miti ovyo.

‎Kiongozi huyo amesema ni jitihada za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya nchi na kulinda afya za Wananchi.

‎Akisoma taarifa kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa, Mkuu wa shule ya Manyara Girls, Bi. Gisella Msofe, amesema mradi huo wa gesi safi ya kupikia utapunguza muda wa kuandaa chakula na kuchangia jitihada za shule katika uhifadhi wa mazingira.

‎Baadhi ya wanafunzi akiwemo Sabrina Msangi, Faith Flavian na Sharon Msangi, wameishukuru serikali kwa mradi huo, wakieleza kuwa sasa watakuwa na muda zaidi wa kusoma badala ya kutumia muda mwingi kutafuta kuni, pamoja na kulinda afya zao kutokana na kupunguza moshi unaotokana na kuni na mkaa.

‎Mradi huo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya mkaa na kuni ili kulinda mazingira, ambapo serikali imeanza na taasisi zinazolisha watu kuanzia 100 na imekuwa ikitoa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500.


Source

Gwajima: CCM Sihami, Tunabanana Mpaka Kieleweke



"Mimi bado ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi na nitaendelea kuwepo. Mimi sihami, CCM nipo sana, tunabanana humu humu ndani mpaka paeleweke pakae vizuri. CCM ni chama cha kidemokrasia kama ilivyo madhumuni ya katiba yake." - Askofu Josephat Gwajima


Tuesday, July 15, 2025

Mchambuzi Hans Rafael Amchana MO Dewji Vibaya: Asitufanye Sisi Watoto

 

Mchambuzi Hans Rafael Amchana MO Dewji Vibaya: Asitufanye Sisi Watoto


Binafsi nimemsikiliza Tajiri ila sıjaona utofauti wa kile alichoongea msimu uliopita na leo.

1. Mo anasema ametoa zaidi ya Tsh 80b,inawezekana ni kweli Ila atwambie na Yeye Simba imemtengenezea kiasi gani?….maana kila mwaka anatumia Brand ya Simba kutangaza bidhaa zake.


2. Mo amesema kila mwaka anatoa hela ya usajili ila mambo yamezidi kuwa yale yale kila mwaka Simba wanasajili Wachezaji 17 na mwisho wa Msimu wanakata 14 je Mo haoni pale Simba kuna shida ya utendaji? Kwani asiwaondoe viongozi wote wanaosajili…..? na kuajiri watu wapya wa mpira kama (Technical Director na Drector of football) ili wasimamie vizuri project na Pesa zake? Kwanini ameendelea kuwakumbatia viongozi wale wale ambao kila msimu wanafuja pesa zake kwa kusajili Wachezaji wa kawaida?


Binafsi nadhani hakuna tajiri mjinga ambae kila mwaka atakubali kupoteza hela Yake Kama hapati faida……Mo amekomaa na Simba coz anapata faida,biashara zake zinaenda,Simba ni Brand kubwa ambayo kila tajiri nchini anatamani kuitumia leo asitufanye sisi kama watoto😄


Ifike Muda matamko yakome,vitendo viongee,Simba kabla ya kupata hela ya Mo wanahitaji mfumo mpya wa katiba na viongozi Ila hawa wa Sasa sioni wakifanya Jambo

Mo Dewji : Toka Mwaka 2018 Hadi Leo Nimetumia Bilioni 87 Kwa Ajili ya Simba



"Kuanzia mwaka 2018 hadi leo nimewekeza shilingi Bilioni 45 kwa ajili ya mishahara, usajili, maandalizi ya Timu na mahitaji mengine ya uendeshaji, pia nimechangia shilingi Bilioni 20 kama sehemu ya ununuzi wa hisa asilimia 49 ndani ya Simba Sports Club na mara nyingi nimekuwa nikitoa msaada nje ya mfumo rasmi, kila palipojitokeza uhitaji wa dharura kuanzia mwaka 2017 hadi 2024 nimetumia takribani Bilioni 22 katika misaada ya dharura hivyo kufanya jumla ya mchango wangu kwa Simba kufikia shilingi Bilioni 87 hivyo kusema Mo hatoe hela ni kauli ya kupotosha yenye mwelekeo wa chuki, tuachane na fitna zisizo na msingi, tujenge palipotoboka, tuzibe ufa panapovuja na tusonge mbele bila kuonyeshana vidole" 

——— 
Mohammed Dewji, Mwekezaji na Rais wa heshima wa Simba Sports Club.

Monday, July 14, 2025

‎Mwenge wa Uhuru Waweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Ghala la Kuhifadhi Mazao Kiteto. ‎


Na John Walter -Kiteto 

Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhi mazao katika Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara.

‎Taatifa ya mkuu wa wilaya ya Kiteto Remidius Mwema kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, Ismail Ussi, imesema lengo la mradi huo ni kutoa huduma za kiutawala kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala, kuinua uchumi wa wananchi na kutoa hifadhi salama ya mazao.

‎Mradi huo unagharimu shilingi milioni 149,680,000 ambazo ni mapato ya ndani ya Halmashauri.

‎Hadi sasa mradi umefikia asilimia 70 ya utekelezaji na unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi mahitaji ya tani kati ya 437.6 hadi 600 za mazao.

‎Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru na timu yake wameridhishwa na mradi huo na hatimaye wameweka jiwe la msingi kama ishara ya kuunga mkono jitihada hizo za maendeleo.

‎Kiongozi huyo wa Mwenge ameupongeza uongozi wa Wilaya kwa kuchukua hatua hiyo muhimu ya kuwakumbuka wakulima, akieleza kuwa kupitia ghala hilo wakulima watanufaika kwa kuhifadhi mazao yao kwa usalama na kupata fursa ya kuuza kwa bei bora kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala.

‎Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 ni:

‎"Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025 kwa amani na utulivu."

Friday, July 11, 2025

Mkoa wa Manyara Wazindua Mpango wa Usambazaji Nishati Safi ya Kupikia kwa Bei ya Ruzuku


Na John Walter -Hanang'

Katika juhudi za kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi, leo julai 11,2025 mkoa wa Manyara umezindua rasmi mpango maalum wa usambazaji wa nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu kupitia ruzuku ya serikali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika wilayani Hanang', Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amewataka Wakuu wa wilaya zote tano za mkoa huo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha unafikia malengo yaliyokusudiwa. 

Ameongeza kuwa mawakala wanaosambaza mitungi hiyo ya gesi wanapaswa kuwa waaminifu kwa kuuza kwa bei iliyoelekezwa na serikali.

Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Matumizi ya nishati safi kwa kizazi cha sasa na kijacho, ambao umeanza tangu mwaka 2020 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2034, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mradi huo, Abdulrazack Mkomi, serikali imetoa ruzuku kwenye mitungi ya gesi ya kilo sita, ambapo kila wilaya imepokea mitungi 3,255. 

Wananchi wataweza kununua mtungi mmoja kwa shilingi 17,500 pekee, kwa sharti la kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA).

Mradi huu una lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia, kulinda afya za wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na moshi wa mkaa na kuni, kuboresha uchumi wa kaya na pia kuhifadhi mazingira kutokana na kupungua kwa ukataji wa miti.

Kwa mujibu wa takwimu, jumla ya mitungi 16,275 itasambazwa kwenye wilaya zote tano za Mkoa wa Manyara, huku zaidi ya shilingi milioni 284.8 zikitumika kugharamia mradi huo.

Kwa hatua hii, serikali inatarajia kuona mabadiliko makubwa katika mtindo wa maisha ya wananchi, kupungua kwa uharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa matumizi ya nishati salama na rafiki kwa mazingira.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...