Monday, June 28, 2021

LISSU: Miezi 3 ya Samia kuna uhuru, watu wanapumua



MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Tundu Lissu, amesema kwa kipindi cha miezi mitatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, kuna uhuru, watu wanapumua na vyombo vya habari vinaandika vitu ambavyo vilikuwa haviwezi kuandika.

Lissu alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa na televisheni moja nchini Kenya.

"Ni kweli kuna mabadiliko, tuna rais mpya, Samia Suluhu Hassan. Katika miezi mitatu ambayo amekuwa rais, ni kweli kuna mambo yamefanyika ambayo yako tofauti na miaka mitano iliyopita. Kuna uhuru, watu wameweza kupumua, sasa hivi kila mtu anapumua, magazeti na vyombo vyetu vya habari sasa hivi vinaandika vitu ambavyo vilikuwa havidiriki kuandika,"alisema Lissu.

Akijibu swali aliloulizwa kuhusu uzuri wa marais wastaafu, Lissu alisema kwa kuanza na awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, yapo aliyoyafanya.

"Kizuri cha Mwalimu Nyerere, alijenga na alikuwa rais muda mrefu kuliko kiongozi mwingine yeyote, alikaa madarakani miaka 24, lakini pamoja na kukaa muda mrefu madarakani, aliachia kwa hiari na bila kuhusishwa na wizi au ufisadi au uchafuzi wa mali za umma," alisema na kuendelea:


 
"Aliondoka madarakani akiwa na mikono misafi, akiwa msafi kwenye masuala ya matumizi ya madaraka na mali za umma, huwezi kumtuhumu Mwalimu Nyerere kwamba alituibia, hakutuibia."

Kuhusu Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Lissu alisema aliirudisha nchi katika msingi mzuri uliosaidia kuokoa uchumi na pia ndiye aliyeleta mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Kuhus Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, Lissu alisema hakuvuruga mfumo wa vyama vingi na alidhibiti Idara ya Usalama wa Taifa kwa kuitungia sheria ya kudhibiti mamlaka yake.


Kuhusu Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Lissu alisema miaka 10 ya Kikwete itakumbukwa kwa kuimarisha Bunge, kuweka bunge hilo kuwa mubashara na alipanua demokrasia.

"Na katika kipindi hiki ndipo tuliona jinsi ambavyo bunge linaweza kuwa, lakini ni rais ambaye chini yake demokrasia ilipanuka, vyama vya upinzani kama CHADEMA vilipata nguvu kubwa sana," alisema Lissu.

KATIBA MPYA

Akizungumzia kuhusu vuguvugu lakudai Katiba mpya linalofanywa na chama chake, Lissu alisema hakuna namna yoyote ambayo chama kikuu cha upinzani kitaenda kwenye uchaguzi na Tume ya Taifa ya Uchagu (NEC) kama ilivyo kwa sasa.

WANACHAMA 19

Akizungumzia waliokuwa wanachama chake wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama chake (BAWACHA), Halima Mdee na wenzake 18, Lisssu alisema anashangaa sababu za watu hao kuendelea kuwapo bungeni wakati chama chao kilishawafukuza uanachama.

"Hawa 19 wanaoitwa wabunge, tumewafukuza uanachama, wako bungeni kwa nini, ili uwe mbunge au diwani au hata mwenyekiti wa kijiji au mtaa, lazima uwe mwanachama wa chama cha siasa na ukipoteza uanachama kwa mujibu Katiba,
unapopoteza ubunge au udiwani  automatic, hawa tumewafukuza kwenye chama, wako bungeni kwa  nini?" alihoji Lissu.

"Na hili ni suala muhimu sana, kuna makosa makubwa ya jinai yamefanyika, kuna watu wamegushi nyaraka za kuwafanya hawa watu wawe wabunge, sheria ya uchaguzi ya  Tanzania inasema hivi, ili mtu awe mbunge wa viti maalum anayewakilisha wanawake, lazima kwanza chama chake kipeleke majina ya hao walioteuliwa kuwa wabunge kwa NEC," alieleza na kuongeza:

"Sisi hatujawahi kupeleka jina hata moja kwa sababu tulijadiliana kwenye kamati kuu ya chama, tukasema kwamba hatukubaliani na uchaguzi, na hatutapeleka majina ya wabunge na hatutachukua pesa ya ruzuku ."

Tanzania Kunufaika Soko Eneo Huru La Biashara Afrika


Na Mwandishi wetu, Dar
Serikali ya Tanzania inategemea kunufaika na soko la bidhaa zake katika masoko ya nje baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa ushiriki katika Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA).

Akiongea na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCTA) Mhe. Wamkele Mene, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho kusaini Mkataba wa AfCTA.

"Lengo la ziara ya Mhe. Mene hapa nchini pamoja na mambo mengine ni kukutana na viongozi na wadau wengine muhimu kujadiliana na masuala mbalimbali yanayohusu Mkataba wa AfCTA ikiwa ni pamoja na umuhimu wa Tanzania kuridhia Mkataba huo," Amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, uanzishwaji wa AfCTA ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa ambapo pamoja na mambo mengine, utekelezaji wake unatarajiwa kuongeza wigo wa fursa nafuu za biashara nchini kwa kuwavutia wawekezaji na kuongeza mauzo hasa ya bidhaa za kilimo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Sekretariati ya Eneuo Huru la Biashara Afrika (AfCTA) Mhe. Wamkele Mene ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano ambao imempatia tangu wakati wa uchaguzi hadi sasa na kuahidi kuwa utekelezaji wa Mkataba huo utanufaisha kila Nchi Mwanachama.

"……….Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwani tangu ilipoingia Madarakani imetumia muda mfupi katika kushiriki kwa ukamilifu katika majadiliano ya kusaini mkataba huu na Tanzania imeshiriki vizuri sana kwenye majadiliano haya muhimu," Amesema Mhe. Wene

Ameongeza kuwa kwa sasa Eneo Huru la Biashara Afrika lina Nchi wanachama 38 ambazo zimekubaliana na Mkataba huo na kwamba kwa sasa Sekretariati hiyo inaendelea kuimarika katika kukuza biashara na sekta binafsi katika nchi wanachama wa AfCTA.

Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika umesainiwa na Nchi 54 kati ya nchi 55 za Umoja wa Afrika ikiwemo Tanzania. mkataba huo ulipata nguvu ya Kisheria Julai, 2019 baada ya nchi 28 kuridhia Mkataba huo. Mkataba wa AfCTA unahusisha maeneno ya ushirikiano katika bishara ya bidhaa, biashara ya huduma, uwekezaji, hakimiliki na ubunifu pamoja na Sera za ushindani.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameshiriki uzinduzi wa Kongamano la Usawa wa Kijinsia ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula kongamano hili litakuwa mahsusi kuangalia masuala ya uswa wa jinsia kwa kizazi hiki na kizazi kijacho na kwamba wakuu wa Nchi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa watakuatana Ufaransa katika kongamano hilo kuanzia tarehe 30 Juni hadi 2 Julai 2021.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, Tanzania itashiriki katika kongamano hilo ambapo Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan atawakilishwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango

Uzinduzi wa Kongamano la Usawa wa Kijinsia uliofanyika leo jijini Dar es Salaam umehudhuriwa na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Fredric Clavie pamoja na Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) Bibi Hodan Addou.


TGNP YAJIVUNIA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA... LIUNDI ASEMA ' ANA MWENDO WA TOFAUTI USAWA WA KIJINSIA'

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi amepongeza mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akisema inazingatia masuala ya usawa wa kijinsia hali itakayosababisha maendeleo yaende kwa haraka.

Liundi ameyasema hayo leo Jumatatu Juni 28,2021 akizungumzia Siku 100 za uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakati akifungua mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga (Kiloleli – Kishapu) na Dar es salaam (Mabwepande, Saranga, Kivule na Majohe) yanayofanyika katika ukumbi wa TGNP Mabibo jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi huyo wa TGNP amesema katika siku 100, serikali ya awamu ya sita imeonesha mwelekeo mzuri katika kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia.

"Suala la jinsia ni suala la maendeleo,ni suala la uchumi, ni suala la kila kitu, hivyo ni lazima tutoe kipaumbele. Uchumi umekuwa ukiyumba kutokana na masuala ya kijinsia kutopewa uzito. Tunatarajia kwa mwelekeo huu tunaokwenda nao katika awamu ya sita pia hata maendeleo yatakwenda kwa haraka",amesema Liundi.

"Tumeona masuala ya usawa wa kijinsia kwenye uongozi ,ni kitu ambacho tumekizungumza kwa muda mrefu tangu mkutano wa Beijing na utekelezaji wa azimio la Beijing, awamu zilizopita zilifanya juhudi zake lakini awamu hii ya sita imekuja na juhudi ambazo ni tofauti, ambazo zinatusogeza mbele zaidi.

Kwa hiyo tukiona Kiongozi wa nchi anazungumza wazi wazi kwamba kwenye masuala ya uongozi atatoa kipaumbele pia kwa wanawake wenye uwezo. Na tumeona anachofanya, kwa upande wa Makatibu Tawala ameteua wanawake asilimia 48, hii inakuwa ni kwa mara ya kwanza. Hiki ni kitu cha kujivunia",ameeleza Liundi.

"Hizi siku 100 ni za kusherehekea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wetu Mpendwa Mhe. Samia Suluhu Hassan amelipa kipaumbele suala la usawa wa kijinsia. Tumeona pia majaji ameteua wanawake asilimia 42.8, mabalozi asilimia 33.3 lakini pia wakuu wa wilaya asilimia 31",amesema Liundi.

Amesema kutokana na hali hiyo hivi sasa kwamba mwendo uliopo ni wa tofauti, mambo yanaenda vizuri kinachotakiwa ni kutoa ushirikiano, wale waliochaguliwa na kuteuliwa waendelee kujitoa, wafanye kazi vizuri, kwa uaminifu, uadilifu ili kuonesha kwa vitendo kuwa wanawake wana uwezo wa ziada.

Aidha amefafanua kuwa serikali ya awamu ya sita imeanza kuonesha mabadiliko kwa kuangalia tunu za kuongoza taifa mfano masuala ya haki, kilimo chenye tija, demokrasia, usawa na uhuru wa vyombo vya habari, kuondoa umaskini na rushwa ikiwemo ubadhirifu wa mali za umma na ukusanyaji kodi usio na bughudha.

Kuhusu mageuzi ya kilimo ambapo mkulima mdogo, mwanamke ndiyo amebeba taifa katika uhakika wa chakula , Liundi ameshauri mwanamke asije akatupwa pembeni, kuwe na mikakati mahsusi ili kuhakikisha kuna ushiriki wa wakulima wadogo wadogo hususani wanawake waliopo kwenye maeneo ya pembezoni ambao wamekuwa wakiteseka kila siku huku akishauri wanawake wapewe kipaumbele zaidi kwenye elimu ya ujuzi kwenye vyuo vya ufundi.

"Lakini pia tumeona katika masuala ya madini,maji, elimu,afya uchumi, utalii, viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano vinatiliwa uzito wa kipekee kama vipaumbele vya maendeleo ya taifa, tunachotaka mwanamke asiachwe nyuma na serikali imeshaonesha nia watu wote watanufaika",amesema Liundi.

Amesema madhumuni ya mafunzo hayo kwa waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa ni kuongeza na kuimarisha uelewa wa washiriki juu ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa sababu suala la kijinsia ni suala la maendeleo.

"Kwa hiyo tunapokuwa na utengwaji wa rasilimali ambazo zinaangalia mtazamo wa jinsia, makundi yote katika jamii yatafaidika na rasilimali za taifa na ndiyo maana tunatia msisitizo",amesema Liundi.

"Tunajua kuwa Bajeti yetu ya taifa imepitishwa na Bajeti ikipitishwa tujue kuwa mwaka mzima tutatembea katika huo mgawanyo wa bajeti. Hivyo kama wananchi ni vizuri kufahamu ni kitu gani kimepita, vipaumbele gani vimepitishwa hali itakayosaidia kufuatilia hizo rasilimali zinatumikaje kwa kuzingatia makundi yote katika jamii",ameeleza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi akizungumza  wakati akifungua mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga (Kiloleli – Kishapu) na Dar es salaam (Mabwepande, Saranga, Kivule na Majohe) leo Jumatatu Juni 28,2021 katika ukumbi wa TGNP Mabibo jijini Dar es salaam. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Lilian Liundi akizungumza  wakati akifungua mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam 
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Lilian Liundi akizungumza  wakati akifungua mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam 
Mwezeshaji katika mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam, Deogratius Temba akitoa mada kuhusu Bajeti ya Mrengo wa Kijinsia.
Afisa Habari wa TGNP, Monica John akizungumza wakati mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam 
Washiriki wa mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia ambao ni waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia ambao ni waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia ambao ni waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia ambao ni waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia ambao ni waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia ambao ni waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam wakipiga picha ya kumbukumbu.
Washiriki wa mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia ambao ni waandishi wa habari na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa ya Shinyanga  na Dar es salaam wakipiga picha ya kumbukumbu.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Dc Busega aanza na kwa kusimamia ushuru wa ndani


Mkuu wa wilaya ya Busega mkoani Simiyu Gabriel Zakaria  amesema atahakikisha anasimamia  makusanyo (ushuru) ndani ya Wilaya hiyo ikiwa ni moja kati ya vipaumbele vyake atakavyovitekeleza akiwa Wilayani hapo.

 Mkuu huyo alisema hayo jana wakati wa kikao chake na wananchi wa kijiji cha Bukabile kata ya Nyashimo ,kilichofanyika katika viwanja vya standi Wilayani hapo.

Alisema bila kusimamia makusanyo ya ushuru,wilaya hiyo haiwezi kuwa na miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo ataanza na usimamizi madhubuti wa ushuru kwa kuunda kikosi kazi cha ufuatiliaji na ukusanyaji.

"Suala la ushuru( mapato) kwangu mimi ni kipaumbele cha kwanza na nitahakikisha tunakusanya zaidi ili asilimia 40 ya miradi iweze kubaki kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za jamii" alisema.

Aliongeza kuwa Wilaya ya Busega ina vyanzo vingi vya makusanyo na kwa kutumia vyanzo  hivyo wataweza kukusanya fedha zaidi na wananchi watapata huduma za afya,miundombinu na elimu .

Aidha amewataka wananchi kulipa kodi wanazostahili na kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kwa pamoja waweze kuibadilisha wilaya hiyo na kwa Wilaya ya mfano.

Tanzania kuanzisha utalii wa lugha ya Kiswahili


Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kuwa inampango mkakati wa kuanzisha utalii wa lugha ya Kiswahili kwenye maeneo yote yenye kumbukumbu kama Butiama kwa lengo la kuwawezesha watalii kujifunza Kiswahili pamoja na kusimuliwa historia na kumbukumbu za waasisi wa Taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 28, 2021, na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Mary Masanja wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Esther Matiko, aliyehoji mpango wa serikali wa kuyaboresha maeneo aliyozaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ili pawe historical site kama ilivyo Afrika Kusini kwa Hayati Nelson Mandela.

"Serikali ina mpango wa kuanzisha utalii wa Kiswahili kwenye maeneo hayo yenye kumbukumbu ili mtalii anapofika katika maeneo hayo ajifunze lugha ya Kiswahili, lakini pia atasimuliwa historia na kumbukumbu ya waasisi wetu walikuwaje na walifanya nini na ukizingatia Mwalimu Nyerere alikuwa ni Muasisi wa kuboresha lugha yetu hii," amejibu Naibu Waziri Mh. Mary Masanja.

MANGE KIMAMBI amshauri HARMONIZE ‘Mashabiki wako karibia wote ni wa ALIKIBA, usishindane naye’


MANGE KIMAMBI amshauri HARMONIZE 'Mashabiki wako karibia wote ni wa ALIKIBA, usishindane naye'

Mange Kimambi Amenadika haya:

 
Mdogo angu upande wa mama huyu….

Fans wako karibia wote ni fans wa Kiba sasa jaribu usiwe unashindana nae unakuwa una kosa support. Kama mi dadako Kiba angekuwa hayuko hewani sasa hivi ningesimana na wewe tuwashinde wale 🤣🤣🤣 ila sasa ona hata nyimbo yako nimeposti ili nikupe hii meseji. Yani the only way na wewe ungeshine kipimdi hiki ilibidi fans wa Kiba wamwache Kiba waje kwako kitu ambacho ni kigumu.

Inabidi uwe very strategic kwenye ku-release kazi zako. Hapa marekani wasaniii hawaachii kazi hovyo wanatumia akili kubwa mnoooooo katika kuachia ngoma. Timing ya kuachia kazi is almost as important as uzuri wa nyimbo. Kwa mfano Rihanna aachie ngoma kali hutokaaa usikue after 2 days Beyonce nae anaachia ngoma. The problem ni kwamba wote wanataka Ngoma zao ziwe#1 kwenye billboard charts sasa mkiachia wote same time lazma mmoja awe 2. Na wasanii wakubwa kutokuwa #1 ni big deal mnoo. So inabidi uachie kazi muda ambao hakuna hit kubwaaaa ili uwe namba 1. Hata kama only for 1 week ila angalau uiguse number 1.

Ona hata Jide kaachia ngoma kali ila watu kama hatujaiona sababu tupo busy na watu wawili. Jide angetulia akaachia ngoma baada ya wiki 3 hivi ange hit kinoma noma. Ila muda hakuuchagua vizuri. Timing is crucial.

Alafu huku wasaniii wanatangaza hadharani tarehe gani ataachia ngoma. Kwahiyo kila mtu anakuwa anasubiria. Drake hawezi kutangaza anaachia ngoma tarehe flani alafu Chris Brown akamvizia ile kaachia tu na yeye kesho akaachia. Mmoja wao ana risk kuwa namba 2 kwenye billboard charts. Mara chache mnoooooooo msaniii mkubwa anaachia ngoma by surprise. Na hata akichia kwa surprise ana hakikisha hakuna ngoma iliyoshika attention za watu.

Kuna kazi ngumu sana inabidi ifanyike ya kuua team Dai na Team Kiba hizi team zinauwa wasaniii wengine. Inabidi tusapoti wasanii woteNa hiyo Kazi inabidi ianzie kwetu sisi vigagula. Ila na wasanii nao wapeane muda wakuachia kazi ili wote wapate attention kubwa, wasigawe mashabiki kwa wote kuachia kazi same time.

Majina ya waliopitishwa kugombea TFF kuwekwa hadharani leo


 MCHAKATO wa uchaguzi kwa sasa bado unaendelea ambapo leo majina ya waliopenya hatua ya kugombea nafasi ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF) inatarajiwa kuwa hadharani

Kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya uchaguzi wa TFF Juni 25-27 ni siku za kufanya usaili wa wagombea ambao walipita kwenye mchujo wa awali na zoezi hilo lilifanywa na Kamati ya Uchaguzi na wagombea wenyewe.

Jana Juni 27 ilikuwa siku ya mwisho kukamilisha mchakato huo na leo Juni 28 itakuwa ni siku ya kutangaza na kubandika kwenye mbao za matangazo matokeo ya awali ya usaili na itafanywa na Kamati ya Uchaguzi TFF.

Uchaguzi unatarajiwa kufanyika Agosti 8 ikiwa chini ya Kimoni Kibamba ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi.

Kwa upande wa nafasi ya Urais ni wagombea watatu walipitishwa kwenye mchujo wa awali ambao ni Evans G Mgeusa, Hawa Mniga na Wallace Karia ambaye anatetea kiti chake. Huku kwa upande wa wajumbe wakiwa ni 17 katika kanda 6.

Makamu Mwenyekiti wa Uchaguzi wa TFF, Benjamin Kalume alisema kuwa watasimamia haki katika uchaguzi huo kwa mujibu wa kanuni.


Source

Burna Boy Ashinda Tuzo Ya BET 2021 katika kipengele cha Best International Act


Msanii Burna Boy kutokea nchini Nigeria leo Juni 28, 2021 amefanikiwa kushinda tuzo ya BET kupitia kipengele cha BEST INTERNATIONAL ACT 2021.

Ushindi wa msanii huyo kutoka Nigeria, unamfanya awabwage washindani wake waliokuwa wakichuna katika kipengele hicho akiwemo Diamond Platnumz na Wizkid kutoka nchini Nigeria.

Wengine waliokuwa katika kipengele hicho ni Aya Nakamura (Ufaransa),Emicida (Brazili), Headie One (Marekani) Young T & Bugsey (Marekani) na Youssoupha (Ufaransa)



MSANII BURNA BOY KUTOKA NIGERIA ASHINDA TUZO YA BET 2021.. DIAMOND PLATNUMZ AKOSA



Msanii Nassib Abdul maarufu Diamond Platnumz amekosa tuzo ya BET ambazo zimefanyika usiku wa kuamkia leo Juni 28, Mkali huyo anayetamba na kibao cha Kamata, alikuwa kwenye kipengele cha Best International Act, tuzo hiyo imeeenda kwa msanii wa Nigeria Burna Boy.

Msanii Burna Boy kutokea nchini Nigeria amefanikiwa kushinda tuzo ya BET kupitia kipengele cha BEST INTERNATIONAL ACT 2021.

Burna Boy alikuwa anashindana na wakali wengine;- Diamond Platnumz (Tanzania), Aya Nakamuraa (Ufaransa), Emicida (Brazil), Headie One (Uingereza), Wizkidayo (Nigeria), YoungTand Bugsey (Uingereza) na Youssouphamusik (Ufaransa).



Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...