Friday, May 29, 2020

Mahakama ya Kisutu yamkuta Mdee na kesi ya kujibu




MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamuhuri, imejitosheleza kwamba Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ana kesi ya kujibu. 

Uamuzi huo ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kupitia hoja za pande zote mbili. 

Akisoma uamuzi huo jana, Hakimu Simba alisema mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais John Magufuli. 

Inadaiwa Julai 3 mwaka 2017 maneno ya Makao Makuu ya Chadema, Mdee alitumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Magufuli akisema 'anaongea hovyo hovyo anatakiwa afungwe breki'. 

Alisema Februari 20 mwaka huu upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ya uchochezi walifunga ushahidi wakiwa na mashahidi watatu. 

Hakimu Simba alisema upande wa utetezi waliwasilisha hoja wakiishawishi mahakama imuone mshtakiwa kwamba hana kesi ya kujibu. 

"Mahakama imepitia kwa makini ushahidi, hoja zilizowasilishwa na msimamo wa kisheria nimejitosheleza kwamba mshtakiwa ana kesi ya kujibu,"alisema. 

 Baada ya kusema hayo Hakimu Simba alitaka kujua mshtakiwa atajitetea kwa mfumo upi na atakuw na mashahidi wangapi kama ambavyo sheria inataka. 

Akijibu Wakili wa utetezi, Hekima Mwasipo alisema mtuhumiwa atajitetea kwa kiapo na atakuwa na mashahidi watano. 

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni 25 na 26 kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kujitetea. 

Katika kesi hiyo, inadaiwa Julai 3,2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mtaa wa Ufipa Wilaya ya Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa "anaongea hovyohovyo , anatakiwa afungwe breki" na kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani. 

Mdee alifikishwa mahakamani hapo Julai 10, 2017 na yupo nje kwa dhamana. 



Source

Zitto Kabwe kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kutoa matamshi ya uchochezi



Kiongozi wa chama cha upinzani ACT-Wazalendo nchini Tanzania ametiwa hatiani na mahakama jijini Dar es Salaam na kuhukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa sharti la kutotoa kauli za kichochezi. 

Chama chake cha ACT tayari kimetoa taarifa ya kuwa bwana Kabwe anapanga kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo. 

Mahakama hiyo imemtia hatiani Zitto kwa makosa yote matatu ya uchocheji yaliyokuwa yanamkabili. 

Hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi imekuja baada ya kipindi cha zaidi ya mwaka mzima wa kesi kuunguruma, kwa mara ya kwanza bwana Zitto kufikishwa mahakamani kusikiliza kesi zake ilikuwa Novemba 2, mwaka 2018.

Zitto anadaiwa kutenda makosa hayo ya uchochezi Oktoba 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari. 

Chama cha ACT kupitia makamu mwenyekiti wake Dorothy Semu kimetoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa hukumu dhidi ya kiongozi wao haikubaliki na wataipinga mahakamani. 

"Hukumu hii ni sawa na kumzuia Zitto kusema chochote cha kuikosoa serikali na rais katika mwaka wa uchaguzi," inaeleza sehemu ya taarifa ya Bi Semu. 

"Hukumu hii haiwezi kukubalika. Inaweza kuwa mfano wa kuminya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza Tanzania."

Bi Semu ameituhumu serikali ya chama tawala nchini Tanzania CCM kwa kile alichokiita "kutumia mashtaka ya uchochezi kuwanyamazisha wale wanaongea ukweli dhidi ya serikali.

Trump Awaita ' VIBAKA ' Waandamanaji Wanaopinga Mauaji ya Mmarekani Mweusi Yaliyofanywa na Polisi

Rais Donald Trump wa Marekani  amewaita waandamanaji wanaopinga mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd katika mji wa Minneapolis kuwa ni "vibaka" na kuonya kwamba watafyatuliwa risasi iwapo wataanza kupora. 

Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter baada ya waandamanaji hao walioghadhabishwa na kifo cha Floyd chini ya mikono ya polisi, kuchoma kituo cha polisi. 

Mapema, Trump alielezea kusikitishwa na kifo hicho akisema lilikuwa ni tukio la kushtusha mno. 

Hata hivyo, alibadilika baada ya machafuko hayo ya jana usiku na kusema kuwa vibaka hao wanachafua kumbukumbu ya Floyd na hatakubali hali hiyo kutokea.

 Alisema amezungumza na gavana Tim Walz na kumueleza kwamba jeshi liko upande wake, na iwapo wataanza uporaji wafyatuliwe risasi.


Masharti ya kukabiliana na virusi vya corona kulegezwa Afrika Kusini




Serikali ya Afrika Kusini imesema kuanzia Jumatatu itawaruhusu watu kununua pombe na kuhudhuria makanisani ikiwa ni sehemu yake ya kulegeza masharti ya kukabiliana na janga la corona. Lakini hatua hizo zitakwenda sambamba na kanuni za kujikinga katika taifa hilo lenye visa vingi vya maambukizi barani Afrika. 

 Uuzaji wa vileo, ambao ulipigwa marufuku tangu Machi 27, utaruhusiwa kwa siku nne kwa wiki. Lakini hakuna pombe ambayo itakayoruhusiwa kununuliwa Ijumaa na katika siku za mapumziko ya nyuma, na baa pia zitaendelea kufungwa. 

 Na pombe hizo zitanywiwa nyumbani tu. Makanisa yatafunguliwa lakini kusiwe na mkusanyiko wa watu wanaozidi 50. Vitakasa mikono, barakoa na kujitenga baina ya mtu na mtu ni mambo ya lazima kanisani. Afrika ya Kusini ina maambukizi 25, 937 huku vifo vikiwa 552.

“Anga Liko Wazi Tanzania, Watalii Karibuni”- Dkt.Kigwangala

Na Paschal Dotto-MAELEZO
Serikali kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), leo imezindua rasmi filamu inayoitambulisha Tanzania ndani na nje ya nchi katika maeneo mbalimbali ya utalii ambayo inaendana na kauli mbiu ya Tanzania Isiyosahaulika "Tanzania Unforgettable" yenye kuitambulisha Tanzania duniani kote.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala amesema kuwa Tanzania imeendelea kutangaza utalii pamoja na kuwepo kwa ugonjwa wa Covid-19, kwani, Rais Dkt.John Pombe Magufuli ameiongoza vyema nchi katika mapambano bila kuathiri sekta za kiuchumi ikiwemo Utalii.

"Namshukuru Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuongoza vyema katika mapambano ya covid-19 bila kuathiri sekta za kiuchumi ikiwemo hii ya utalii, kwani kwa  sasa tumefungua sekta hii, kama mnavyojua biashara ni ushindani atakeyewahi kufungua na kuweka misingi mizuri ya kuwahudumia wageni na wahudumu sekta ya utalii ndiye atakayepata faida zaidi, tumeamua kufungua utalii wetu na sasa anga letu lipo wazi kwa watalii", Dkt.Kigwangala.

Amefafanua kuwa Tanzania imejipanga kuwahudumia vyema watalii watakao watawasili nchini na kuhakikisha kuwa wanaondoka salama ili wakifika katika nchi zao wapeleke habari njema kwamba Tanzania ni salama na watalii ambao walisita kuja waje bila woga.

Amebainisha kuwa Serikali imeamua kufungua sekta ya utalii kwa kufuata tahadhari zote zinazotolewa na mamlaka husika ikiwemo Wizara ya Afya ya Tanzania na Shirika la Afya Duniani (WHO), na kuwakaribisha watalii.

Katika uzinduzi huo, Waziri Kigwangala ametoa rai kwa Watanzania kuisambaza  filamu hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter, Instgram, telegram na mitandao mingine, ili iweze kuwafikia walengwa kwa lengo la kutangaza Tanzania kiutalii katika soko la utalii la kimataifa.

"Hii ni video rasmi au filamu fupi kwa lengo la kuitambulisha nchi yetu kiutalii katika soko la utalii kimataifa, na hii imeendana sawa kabisa na kauli mbiu ya Tanzania Unforgettable kwa hiyo ninaomba Watanzania wenzangu tuisambaze kwenye mitandao yetu ya kijamii kwa maana imetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili, Kingereza, Kifaransa, Kihispania, Kiisrael na Kichina", Dkt. Kigwangala.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi.Devotha Mdachi alisema kuwa Tanzania kwa sasa imejikita zaidi kutangaza vivutio vya utalii kupitia mitandao ya kijamii, kwa hiyo kuzinduliwa kwa filamu hiyo fupi kutawasaidia kuteka soko la ndani na nje ya nchi.

"Sisi Kama Bodi ya Utalii tumejikita zaidi kutangaza utalii kwa kutumia mitandao ya kijamii, kwani mpaka sasa tuna vipindi vinavyoruka mubashara kupitia mitandao yetu kwa mfano kipindi cha Serengeti safari show na kile kinachorushwa na Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro, hizi ni moja ya njia za  kutangaza utalii ndani na nje ya nchi", Bi. Mdachi.

Ameongeza kuwa kupitia filamu hiyo fupi watalii watapata fursa ya kuona utamaduni na maeneo mbalimbali ya kuvutia na kuweza kuchagua sehemu sahihi ya kwenda kutembelea, amewataka Watanzania hasa watu maarufu kusambaza filamu hizo za dakika moja, dakika tatu, dakika saba na dakika 10 kwenye kurasa zao ili ziweze kufika mbali zaidi.

Mwisho.



Source

Kuwa Makini Sana Na Mambo Haya Yanaweza Kukuzia Kufanikiwa Kwako.


Kuna wakati unaweza ukawa unashangaa kwa nini ndoto zako hazitimii?  Utakuta umejiwekea malengo yako vizuri, lakini unashangaa ni malengo machache sana yanayotimia au wakati mwingine hakuna kabisa.

Sina shaka yoyote umeshawahi kukutana na hali kama hii wakati fulani katika maisha yako. Kiuhalisia, yapo mambo mawili ambayo kitaalamu hupelekea ndoto zako kushindwa kutimia ikiwa hutayajua vizuri.

Jambo la kwanza, ni kutokujua kile unachokitaka vizuri. Hili ni jambo ambalo hupelekea wengi kushindwa kufanikisha ndoto zao kabisa. Kama hujui kile unachokitaka vizuri, suala la kufanikisha ndoto zako litakuwa gumu kidogo.

Katika akili yako ili uweze kufanikisha ndoto yako au jambo unalolitaka kwa urahisi, ni lazima kile kitu unachokitaka uweze kukijua vizuri. Tambua njia utakazotumia hadi kukipata kitu hicho pia tambua kitu hicho changamoto zake ni zipi.

Acha kufanya kosa la kuuchanganya ubongo wako kwa kuupa vitu vingi. Kuwa maalumu kwa kujua vizuri kile unachokitaka. Usipojua kile unachokitaka kwa uhakika na kukifanyia kazi, ni wazi hutaweza kufanikiwa na hilo halina ubishi.

Jambo la pili, ni kukosa hamasa ya kutosha kwa kitu hicho unachokitaka. Hamasa ni kitu cha muhimu sana ili kufikia ndoto zako. Ukishakijua kitu hicho vizuri, hamasa itakusaidia kufanya kila jitihada hata kama umechoka.

Wengi ni watu wa kutaka kufikia lengo fulani katika maisha yao, lakini kwa bahati mbaya hujikuta ni watu wa kukosa hamasa ya kuwasukuma kuweza kukamilisha malengo yao.

Ili kufanikiwa, fanya kila ufanyalo kuhakikisha una hamasa ya kufanya hicho unachotaka kukifanya katika maisha yako. Inapotokea hamasa hiyo umeikosa acha kusimama eti kwa sababu ya kukosa hamasa.

Maisha hayasimami eti kwa sababu wewe hujisikii kufanya kitu fulani au umekosa hamasa. Endelea kusonga mbele, huku ukitafuta hamasa ya kufanikiwa kwako kila siku. Ukifanya hivyo utafika mbali kimafanikio.

Katika hali ya kawaida, kama kila wakati unakosa mambo haya mawili suala la kufanikiwa kwako linakuwa ni gumu sana. Hivyo, ni lazima sana kwako kujua vizuri kile unachokitaka na kuwa na hamasa kubwa yaani 'burning desire' ya kuhakikisha kitu hicho ni lazima unaweza kukipata.
Ukichunguza watu wengi ambao hawajafanikiwa wanashindwa kufanikiwa kwa sababu hizi mbili tu na si vinginevyo. Kama unafikiri natania anza kufatilia, huku lakini ukianza na wewe.

Kama unajiona hujafanikiwa vya kutosha jiulize binafsi je, unakijua vizuri kile unachokitaka na huna tamaa ya kutaka  hiki mara kile na mwisho wa siku kuwa na malengo mengi yasiyotekelezwa?

Usiishie hapo tu, tena kama unaona hujafanikiwa vya kutosha jiulize, je, una hamasa kubwa ya kuona ndoto zako zinatumia? Je, unakosa usingizi na kuamua kujituma usiku na mchana hadi kufanikiwa?

Ukipata majibu ya maswali hayo yatakusaidia sana kuweza kufanikiwa na kuwa mtu mwingine tofauti na hatimaye kuweza kufanikisha zoezi zima la kutimiza ndoto zako. Jitoe kikamilifu kuona ndoto zako zinatimia kwa kuyajua mambo hayo mawili.
Ni wako rafiki katika mafanikio,

BASI LA PREMIER LA MWANZA - MBEYA LAPATA AJALI USANDA SHINYANGA..KUNA MAJERUHI




Watu 59 waliokuwa wakisafiri kutoka Jijini Mwanza kwenda Mbeya wamenusurika na kifo mara baada ya basi walilokuwa wakisafiria Premier lenye namba za usajili T, 629 AET, linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Mbeya kupata ajali katika kijiji cha Ngaganulwa Usanda wilayani Shinyanga na kusababisha majeruhi Saba.



Akisimulia, mashuhuda wa ajali hiyo Robart Samwel aMEsema tukio hilo limetokea leo Ijumaa Mei 29,2020 majira ya saa 3 asubuhi katika eneo hilo, ambapo kulikuwa na mabasi mawili yamesimama ndipo basi hilo likiwa katika mwendokasi lilishindwa kusimama na hatimaye dereva kulikwepesha na kuanguka.

Alisema katika eneo hilo kulikuwa na basi la Abood limesimama upande wa kushoto na jingine la Ally's Bus upande wa kulia, ambapo basi hilo la Premier lilianza kufunga breki na baada ya dereva kuona limemshinda ndipo akalikwepesha vichakani na kuanguka chini.

"Nimeishuhudia ajali ya basi hili la Premier kwa macho yangu kabisa, ambapo pembeni ya barabara kulikuwa na basi la Abood limesimama na upande mwingine kulikuwa na basi la Allys, ndipo basi hili likiwa katika mwendo kasi lilishindwa kusimama na kusababisha ajali," alisema Samweli.

Nao baadhi ya abiria akiwemo Justice Alyoce ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha Sita ,alisema wakati akitokea jijini Mwanza basi hilo la Premier pamoja na Abood yalikuwa yakifukuzana ndipo walipofika eneo hilo na kukuta mabasi la Abood na Allys yamesimama likamshinda ndipo ikatokea ajali.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP Debora Magiligimba ambaye alikuwa eneo la tukio, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi, ambapo dereva wa basi la Premier alipofika eneo hilo na kukuta mabasi mawili yamesimama pande zote basi lilimshinda na hatimaye kuanguka.

Aidha alisema basi hilo lilikuwa limebeba abiria 59 wakiwamo wanafunzi, huku akiwataja majeruhi saba wa ajali hiyo kuwa ni Thabiti Abdul, Swaumu Kisandu, Mohamed Nyerere, Betha Minami, Mohamed Ahmed, Ilham Yahya, pamoja na Haida Hassani.

Alisema majeruhi hao wote wamepata majeraha katika maeneo mbalimbali ya viungo vyao vya miili yao, ambapo walikimbizwa kupatiwa matibabu katika kituo cha afya Tinde kilichopo karibu na eneo la ajali,na kwamba hakuna kifo, na kubainisha wanamtafuta dereva wa basi hilo ambaye amekimbia kusikojulikana.


TAZAMA PICHA HAPA CHINI



Basi la Premier lenye namba za usajili T, 629 AET linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Mbeya likiwa limepata ajali katika eneo la Ngaganulwa- Usanda wilayani Shinyanga na kusababisha majeruhi saba. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga  ACP Debora Magiligimba akiwa eneo la tukio na kuzungumzia chanzo cha ajali hiyo.

Abiria Justice Aloyce ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha Sita Jijijni Mbeya akielezea namna ajali ilivyoanza kutokea sababu ya uzembe wa dereva. kutokea Jijini Mwanza.

Muonekano wa basi la Premier likiwa limeanguka chini mara baada ya kupata ajali.

Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Thursday, May 28, 2020

Uongezaji wa makalio ni hatari isiyozungumzwa



Mwanamke wa miaka mitatu amefariki baada ya kuripotiwa kuelekea Uturuki kwa aina ya upasuaji kwa jina Brazilian Butt Lift [uongezaji wa makalio}.

Ni kwa nini upasuaji huu ni maarufu mbali na kwamba ni hatari kufanyiwa upasuaji huo ughaibuni.

Leah Cambridge kutoka Leeds alipatikana na mishtuko mitatu ya moyo baada ya kudungwa sindano ya ganzi katika kliniki moja katika mji wa Izmir, mwenzake Scott Franks aliambia gazeti la the sun.

Anaeleweka kufanyiwa BBL ama upasuaji wa kuongeza makalio ambapo mafuta kutoka katika tumbo hutiwa katika makalio.

'Mrembo huyo alikubali kufanya upasuaji ughaibuni ambapo ni bei nafuu ikilinganishwa na Uingereza baada ya kukerwa na mafuta mengi katika sehemu yake ya tumbo baada ya kupata watoto', alisema bwana Frank.

Majirani wake wamemtaja kuwa mtu anayevutia, wakiongezea kuwa wanaamini alielekea kufanyiwa upasuaji huo mwezi uliopita bila kumshauri mpenziwe.

Na bi Cambridge sio mwanamke wa kwanza Muingereza ambaye hamu yake ya kuwa na makalio ya kuvutia yalimwangamiza akiwa ughaibuni.

Joy Williams alifanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio yake mjini Bangkon nchini Thailand mnamo mwezi Octoba 2014.

Vidonda vyake vilipata maambukizi na mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 24 kutoka mjini London , alifariki akidungwa sindano ya ganzi.

Miaka mitatu kabla , Claudia Aderotimi mwenye umri wa miaka 20 , kutoka Hackney , mashariki mwa London alifariki kutokana na matibabu ya kujiongeza makalio yake katika hoteli moja nchini Marekani.

Upasuaji wa kuongeza makalio hauonekani kuwa hatari zaidi ya aina nyengine zozote za upasuaji, kulingana na daktari wa upasuaji wa urembo Bryan Mayou.

'Hatari yake ni upasuaji huo kufanywa na madaktari ambao hawajahitimu, nje ya kliniki bila kuwa na maelezo ya jinsi ya kujichunga baada ya matibabu hayo kufanywa', anasema bwana Mayou, mwanachama wa muungano wa madaktari wa upasuaji nchini Uingereza.

Iwapo mafuta yataingizwa katika tishu ya sehemu ya makalio kuna hatari ya kuingiza mafuta hayo katika mishipa mikubwa ya damu.

Mafuta hayo yanaweza kupita katika mishipa ya damu , kuingia katika mapafu kabla ya kusababisha kifo.

Bwana Frank aliambia gazeti la The sun : Leah alikuwa amedungwa sindano ya ganzi akakumbwa na matatizo baada ya mafuta kuingia katika mishipa yake ya damu hatua iliofanya viwango vyake vya oxygen katika damu kushuka .

Hali yake iliimarishwa lakini alikumbwa na mishtuko mitatu ya moyo na hawakuwa na la kufanya.

'Madaktari wa upasuaji kutoka jamii za kimataifa wameunda jopo kuchunguza kuripoti kuhusu utaratibu huo'', anasema Mayou.

'Viwango vya vifo vinavyotokana na utaratibu huo ni kisa kimoja kati ya 3000 huku vifo vyote vilivyochunguzwa vikihusisha mafuta yaliopatikana ndani ya mishipa ya misuli ya makalio', anasema.


Ni mtindo wa kisasa, miaka kadhaa iliopita kila mtu alipendelea kuwa mwembamba na walikuwa wakisema kuwa wanataka kufanyiwa upasuji ili kufanya makalio yao kuwa madogo.

'Na hiyo ndio mbinu ambayo inaweza kutumika iwapo mtindo mpya wa kuongeza makalio utakwisha na mwathiriwa anataka makalio yake kurudishwa yalivyokuwa', anasema.

Kwa nini watu wanapendelea sana kuwa na makalio makubwa ? ni kutokana na utamaduni maarufu wa kushabikia maungo yanayovutia.

Watu maarufu kama vile Kim Kardashian , Kylie Jenner na Cardi B wana umaarufu mkubwa katika mitandao ya kijmaii ambapo huchapisha picha zao wakionyesha makalio yao yalio mviringo.

Jenner alichapisha katika blogi yake ambapo alisifu maumbile yake na uzani ulioongezeka.

''Sijaongezewa makalio. Unajua, nilikuwa na uzani wa 120 [lbs]. Nilikuwa mwembamba sana. Sasa nianelekea 136Ibs , lakini ni sawa napendelea uzani nilionao''.

Hatahivyo, Cardi B amefichua kwamba kabla ya kuingia katika fani ya muziki aliongezewa makalio huko mjini New York na kifaa alichowekewa ndani kilivuja kwa siku tano baadaye.

Katika mahojiano alisema kuwa alilipa takriban $800 (£564) kwa upasuaji huo baada ya kuwaona wachezaji densi wanzake walio uchi katika vilabu vya burudani walio na makalio makubwa wakipata fedha nyingi kumliko.

Chloe Simms, ambaye ni nyota wa kipindi cha runinga cha The Only Way Is Essex, amekuwa wazi kuhusu makalio yake aliyoongezewa baada ya kulalamika katika kipindi hicho kwamba alikuwa hana makalio.

Prof. Kabudi akutana na kuzungumza na mabalozi wa Ufaransa, Uturuki nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Pamalagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Clavier ameipongeza Tanzania kwa hatua ilizochukua kupambana na janga a virusi vya corona nchini.


Balozi Clavier pia amemhakikishia Mhe. Waziri kuwa Ufaransa inaiunga mkono Tanzania kwa asilimia 100 kwa hatua ilizochukua kupambana na janga la virusi vya corona na kusema Ufaransa itaipatia Tanzania Euro milioni 30 ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu na riba ndogo kwa ajili ya kupambana na janga la virusi vya Corona pamoja na kusaidia kuinua uchumi.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Waziri Kabudi amemuelezea Balozi wa Ufaransa jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na Janga la Corona nchini na kumhakikishia utayari wa Tanzania katika kupambana na janga hilo na kuongeza kuwa Serikali ya Tanzania ilichukua hatua hizo kulingana na hali halisi ya maisha ya watanzania.

Prof. Kabudi amesema hatua zilizochukuliwa na Tanzania zililenga kuwafanya watanzania kuendelea na maisha yao bila ya kuathiriwa kiuchumi huku wakijilinda na kuchukua tahadhari ambazo zilikuwa zikitolewa na wataalamu wa afya nchini na duniani.


Balozi Clavier amemuambia Mhe. Waziri Kabudi kuwa Ufaransa pia imetoa msaada wa Dola 500,000 ambazo watapewa wakulima wadogowadogo 6,000 nchini kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha kilimo chao na maghala ya kuhifadhia mazao yao.

Ameongeza kuwa Rais wa Ufaransa ameziandikia nchi za G20 na Paris Club kuzishawishi kuahirisha ulipaji wa madeni na riba zake na pia kufuta kabisa madeni hayo ili kuimarisha uchumi ambao umeathiriwa na janga la corona katika nchi zinazoendelea.

Katika hatua nyingine Waziri Kabudi amekutana na kuagana na Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Ali Davutaglu ambaye amemaliza muda wake wa utumishi na amemtakia maisha mema na kumwambia kuwa ni matarajio yake kuwa atakuwa Balozi wa hiari wa Tanzania nchini uturuki na kwingineko duniani.


Naye balozi Davotaglu ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa ikimpatia alipokuwa akitekeleza majukumu yake nchini na kuahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa. 
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...