Sunday, December 29, 2019

Diamond Platnumz Apokelewa Kishujaa Kigoma

Mwanamuziki Diamond Platnumz amepokewa na mabango wakati akiwasili stesheni ya Nguruka Mkoani Kigoma katika kuadhimisha miaka yake kumi katika muziki.

Umati wa watu umejitokeza katika stesheni ya Nguruka Mkoani Kigoma wakiwa na mabango yaliyobeba jumbe mbalimbali kwa mwanamuziki huyo.

Moja ya mabango hayo lilikuwa limeandikwa "Karibu Diamond kwenu Kigoma tuijenge Kigoma, Sisi Nguruka tulishaanza ujenzi wa madarasa saba na vyoo 12. Tunaomba tuunge mkono, watoto 494 hawana pakusoma."

Diamond aliyeanza safari ya kuelekea Kigoma jana Desemba 28, 2019 akiwa na mashabiki wake katika treni lengo lake kubwa ni kujumuika na watu wa mkoa huo kusheherekea miaka kumi tangu kuanza muziki.

Nguruka ikiwa ndio stesheni ya kwanza unapoingia Mkoa wa Kigoma, Diamond alikutana na umati wa watu ukimsubiri.

Baada ya kuwasili eneo hilo Diamond alipanda jukwaani na kuanza kuwaimbisha wakazi hao wimbo wa Baba lao .
Hata hivyo ilifika mahali mzuka ukampanda kweli kama moja ya kibwagizo kilichopo katika wimbo huo kinachosema 'mzuka ukipanda hata nguo nitavua, nivue muone'walipoitikia mashabiki akavua fulana yake aliyokuwa ameivaa ambapo watu wake waliichukia na baadaye kumrudishia



Source

Monday, December 23, 2019

WAJAWAZITO WAIDAI SERIKALI - "TWENDE NA WAUME ZETU KLINIKI"

Na Abby Nkungu - Manyoni
Imeelezwa kuwa moja ya sababu ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kukumbwa na utapiamlo ni kutokana na baadhi ya wanaume kutokuwa na tabia ya kwenda kliniki na wenzi wao pindi wanapokuwa wajawazito ili wakapatiwe elimu na ushauri wa Lishe bora kwa Mama na Mtoto.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Muhalala katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida walisema kutokana na mfumo dume katika jamii nyingi ambapo baba ndiye mtoa uamuzi na mmiliki wa kipato katika familia,wengi wa wajawazito hushindwa kupata lishe bora kwa kukosa fedha za kununua mahitaji muhimu kulingana na ushauri wa kitaalamu.

Walisema kuwa hali hiyo husababisha lishe duni isiyokuwa na virutubisho muhimu kwa mtoto aliye tumboni na hata baada ya kuzaliwa hali ambayo walidai huendelea kutokana na wanawake wengi kuishi kwa kuwategemea waume zao ambao hawajui umuhimu wa lishe bora.

"Hebu fikiria kwa baba ambaye ni mlevi kupindukia, utoke kliniki eti ukamueleze unatakiwa upate lishe bora kwa afya yako na mtoto aliye tumboni, hawezi kukuelewa katu", alisema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mariam Bunku mkazi wa Muhalala Wilayani Manyoni.

Alieleza kuwa tatizo hilo ni moja ya sababu ya baadhi ya watoto kupata utapiamlo kutokana na lishe duni inayochangiwa na baadhi ya wazazi wa kiume kutojua umuhimu wala kuwa na elimu ya lishe bora.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanawake wanasema kuna haja kwa Serikali kutunga Sheria itakayowalazimisha wanaume kwenda na wenzi wao kliniki kabla na baada ya kujifungua.

Walidai kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza tatizo la utapiamlo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano iwapo akinababa, ambao ndio watoa uamuzi, watapata elimu na kujua umuhimu wa lishe bora kwa mama na mtoto.

Ofisa Lishe mkoa wa Singida, Teda Sinde anasema ukosefu wa lishe bora kwa mjamzito husababisha udumavu kwa mtoto aliye tumboni na hata baada ya kuzaliwa huathiri ukuaji wa ubongo na maungo ya mwili wake; hivyo kudumaza maendeleo ya ukuaji wake kwa ujumla.

Takwimu za utafiti wa kitaifa za mwaka 2018 juu ya hali ya lishe mkoani Singida zinaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia 5 ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo.

Kadhalika, utafiti huo unabainisha kuwa asilimia 27.9 tu ya watoto hao ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na asilimia 3 tu ya watoto walio chini ya miaka miwili ndio angalau hupata mlo unaokubalika katika tafsiri ya lishe bora. 

Friday, December 20, 2019

Mwanamke bora katika maisha ya ndoa hujengwa na mambo haya

Maisha halisi ya mwanamke anayetarajia kuwa mke/ mke tayari hii ni kumaanisha kuwa wanawake mashujaa tunapaswa kuishi maisha ambayo yanatutambulisha kama mfano wa kuigwa ili tunapozungumza na kufundisha mabadiliko tuwe tunazungumza uhalisia wa maisha yetu ambao unajengwa na haya yafuatayo;

Uvumilivu
Kuwa mvumilivu katika maisha yake ya kila siku hasa ukizingatia kuwa tunakutana na mambo mbali mbali yasiyotuvutia katika mahusiano yetu, mengine ni magumu na yanayokwenda kinyume kabisa na matakwa yetu au mazoea yetu ya binafsi. Ifahamike kwamba wewe kama mwanamke shujaa inapotokea umekutana na mambo kama haya hupaswi kuonyesha hasira zako wazi wazi kama vile; chuki, kulaumu, ugomvi, vurugu, malalamiko, manung'uniko, machafuko, kulipa kisasi au aina yoyote ya uharibifu kutokea kwako au ndani mwako. Hivyo mwanamke shujaa huwa ni heri kila anapokuwa kwani hutunza amani ya eneo alipo.

Upendo wa dhati
Maisha ya upendo wa halisi na sio wa kinafki kwa jamii inayomzunguka. Tabia ya upendo wa halisi ina thamani kubwa sana kuliko mali nyingi, pesa, elimu ya juu n.k. Wewe unaweza kabisa kuwa na elimu ya juu sana na pesa nyingi sana lakini pasipo upendo wa halisi ni sawa na kusema kopo zuri kwa nje na ndani hamna kitu. Nguzo kuu ya maisha ya mwanamke shujaa ni upendo wa dhati na uhalisia.

Utii kwa jamii
Maisha halisi ya utii katika jamii inayokuzunguka  ili kuweza kuyafanyia kazi yale yote uliyojifunza na pia kuyatenda kwa ufasaha pasipo kupita kona yoyote. Utii  kwa jamii ni ufunguo mmoja wapo utakaokusaidia kufanikisha mambo yako na malengo yako kama mwanamke shujaa.

Uaminifu katika jamii
Kuishi maisha ya uaminifu wa kweli na uhalisia katika jamii inayomzunguka. Uaminifu wa kweli huonekana nyakati zote na siyo tu wakati mtu anapokuwa mbele za watu wanaomjua bali hata wale wasiomjua na hata anapokuwa mahali peke yake aweze kutunza uaminifu wake kwa faida ya jamii nzima. Mwanamke shujaa hujitahidi sana kutunza uaminifu wake katika sekta zote.

Unyenyekevu wa kweli
Kuishi maisha halisi kabisa ya unyenyekevu kwa jamii inayomzunguka, unyenyekevu ni kinyume kabisa na kiburi, majivuno, kujigamba, kujikweza, kujiinua, kujiona,na hata kjitanguliza mbele kwa kila jambo. Mwanamke shujaa huwa ni mnyenyekevu wakati wote na hana makuu daima.

Uwajibikaji wa dhati
Maisha halisi ya uwajibikaji akiangalia majukumu yake yote yanayomkabili na kuhakikisha anafanya kwa moyo bila kuwa na tabia ya kusaidiwa majukumu yake. Mwanamke shujaa ni mfano wa kuigwa kutokana na uwajibikaji wake.

Ushirikiano wa dhati
Ushirikiano katika jamii inayomzunguka. Sisi wanawake mashujaa yatupasa kujua dhahiri kuwa kazi ya kubadili tabia na kufanya wengine wabadilike kwa lengo la kupata familia bora ni lazima kuwa na ushirikiano wa kweli ambao utajenga tabia ya kuaminiana na kunai mamoja katika harakati hizi za kuandaa/ kujenga familia bora.

Utaratibu wa kazi/mpangilio
Katika utaratibu wa maisha yake, pamoja na mpangilio mzuri wa mambo yanayomzunguka hii itakusaidia kuwa na muda mzuri wa kufanya shughuli zako na pia kutekeleza majukumu yako ya kila siku kama mwanamke shujaa. Hakuna njia yoyote ya kukuwezesha kukua na kuendelea katika maisha yako bila kuwa na utaratibu na mpangilio wa mambo yako.

Thursday, December 19, 2019

TRUMP APIGIWA KURA NYINGI ZA MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA


Baraza la Wawakilishi la Marekani limepiga kura kuridhia kushtakiwa kwa Rais Donald Trump kwa kutumia vibaya madaraka yake na kuingilia uchunguzi wa Bunge.



Mchakato wa mwisho wa kura utalihusisha baraza la Seneti ambalo litakuwa na mamlaka ya kuamua kama anaweza kuondolewa madarakani au la

Matokeo ya mchakato huo ni kama ulikuwa ukijulikana mapema kutokana na baraza hilo kuwa na wingi wa wabunge wa chama cha Democratic.  


Baada ya majadiliano ya masaa 10, wabunge walipigia kura vifungu viwili vya sheria; Shtaka la kwanza likiwa ni kutumia vibaya mamlaka aliyonayo lililotokana na madai ya kwamba Trump alijaribu kuishinikiza Ukraine kutangaza uchunguzi dhidi ya hasimu wake wa kisiasa na mgombea urais kupitia chama cha Democrats, Joe Biden.

Shtakala pili lilikua ni kuzuia shughuli za bunge la Kongresi kwasababu rais anadaiwa kukataa kutoa ushirikiano katika uchunguzi dhidi yake, kwa kukataa kutoa nyaraka za ushahidi na kuwazuwia wasaidizi wake kutoa ushahidi katika uchunguzi huo.

Kura katika kipengele cha kwanza cha uchunguzi, cha kutumia vibaya mamlaka zilikuwa 230 ndiyo na 197 hapana na kipengele cha pili cha kuzuia utendaji wa Kongresi zikawa 229 ndiyo na 198 hapana.

Baraza la wawakilishi lina nguvu ya kumshitaki rais kwa wingi mdogo wa kura, lakini baraza la Seneti litahitaji wingi wa theluthi mbili kumuondoa rais madarakani, hatua ambayo sio rahisi kufanyika. 

Rekodi zinaonesha kuwa hatua hiyo ni ya mara ya tatu kwa rais wa Marekani kushitakiwa.




MBOWE ADAI KUANZIA MWAKA 2020 CHADEMA HAITATEGEMEA TENA RUZUKU KUJIENDESHA


Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, kimezindua mfumo wake mpya wa Kidigitali wa uendeshaji wa Chama hicho ambapo kitakuwa kikikusanya ada za Uanachama wa wanachama wake na kukifanya kujitegemea.


Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Chama  hicho uliofanyika leo jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe, amesema mfumo utawasaidia kukusanya karibia Bilioni 15 kwa mwaka.

Mbowe amesema programu hiyo iliyozinduliwa leo Jumatano Desemba 18, 2019 inahusisha uandikishaji wa wanachama kidigitali, kufanya mikutano kidijitali pamoja na kampeni.

"Kila mwaka mwanachama anatakiwa alipie Sh1,000 ya ada, kwenye vikao hivi tunapendekeza iwe Sh2,500 kwa mwaka. Maana yake ni nini? Leo hii chama kinapata ruzuku ya Sh3 bilioni kwa mwaka. Gharama ya kufanya mkutano wa baraza kuu ni zaidi ya Sh1 bilioni kwa hiyo ruzuku peke yake haitoshi."

"Kupitia Chadema Digital tuna digital fund raising, tumekubaliana kuchangia Sh2,500. Asilimia 90 wana Chadema wana simu za mkononi, kila mwanachama akilipa kwa simu tutapata Sh15 bilioni kwa mwaka."

Amesema kupitia vikao vyao wataibadilisha katiba ya Chadema ili kuruhusu mfumo huo ufanye kazi vizuri, "tunahitaji kujenga chama cha kujitegemea na hili msajili usikie, maana yake kuna watu wanafikiri chama kinategemea sana ruzuku."

Amesema kutokaa na mfumo huo, chama hicho sasa hakihitaji tena kufanya mikutano ya hadhara ili kupata wanachama wapya.


Wednesday, December 18, 2019

Mambo 5 ya kuficha unapokuwa kwenye ndoa yako


Yafuatayo ndiyo mambo matano ya kuficha unapokuwa kwenye maisha ya ndoa;

Tendo 
Maisha yenu ya mahusiano ya kimwili  (sex) na mwenzako ni marufuku kumwambia mtu yeyote kwa gharama yoyote. Funga mdomo; iwe ni nzuri au mbaya. Ni mwiko kuwambia watu! (watu ni pamoja na mama yako, ndugu, marafiki, viongozi wa dini, n.k.)

Utamaduni 
Utaratibu wenu wa kufanya mambo na mtindo wa maisha. Kwa mfano, sio lazima kuwaambia watu mambo yenu ya ndani ikiwemo mipango yenu ya baadae ya kifamilia au biashara, mambo ya watoto wenu, n.k. Ikibidi kusema, basi iwe ni kwa sababu maalumu sana ya kujenga watu wengine na kufundisha wengine sio kuanika tu maisha yenu hovyo; hasa mtandaoni. Ni muhimu kuchagua kwa makini kitu cha kuweka hadharani kwa maana ukitoa jambo hutaweza kulirudisha wala kulizuia lisisambae; litaenda hadi usikotaka, litaendea tu!

Ugomvi 
Hakuna faida yoyote ya kusema magomvi yenu ya kwenye ndoa. Mara nyingi, tabia ya kusema magomvi yenu itawapunguzia heshima mbele ya jamii. Mara chache sana tabia hiyo ina faida, ila kila palipo na faida ya kusema magomvi, hasara ni kubwa zaidi kuliko faida. Chagua mwenyewe!

Pesa 
Kipato chenu na pesa zenu ni siri. Wacheni watu waone kazi zenu na jinsi mnavyowasaidia wengine sio kujisifia pesa!

Siri 
Ni mwiko kutoa siri za ndoa! Kama mwenzako kasema, "hii ni siri" au "usimwambie mtu!" Au "nimekwambia wewe tu!", n.k. Hakikisha husemi kwa gharama yoyote, la sivyo hatakuamini tena! Na hasara yake ni kwamba, hatakuamini hata katika mambo mengine mengi tu! Tabia ya kutoa siri ni mbaya na inaweka ufa usiozibika kwa urahisi.

Tuesday, December 17, 2019

Mbinu muhimu za kuzingatia ili kufanikiwa katika biashara


Biashara nyingi zinazoanzishwa haziwezi kufikisha miaka mitano, na hata zinazofikisha huwa hazina maendeleo mazuri.

Hii ni kutokana na sababu biashara nyingi huanzishwa kiholela, kienyeji, kimazoea, ukosefu wa mipango na mikakati ya biashara. Pia, ukosefu wa utafiti wa masoko na kukosa utaalamu na ujuzi mbalimbali katika biashara.

Katika kuanzisha biashara yako unatakiwa kujifunza mbinu na ujuzi mbalimbali kadri unavyozidi kuifanya ili iweze kufanikiwa. Kuna hatua ambazo ukizifuata biashara yako itafanikiwa.

Fanya utafiti
Ukishakuwa na wazo la biashara unayotaka kufanya, kinachofuata ni kuangalia uhalisia, jiulize je, wazo lako lina uwezekano wa kufanikiwa? Unahitaji kuendeleza wazo lako huku ukiendelea kufanya utafiti wa kina ili kupata uhalisia wa wazo lako kabla hujasonga mbele.

Ili biashara ndogo ifanikiwe lazima ilenge kutatua tatizo, kukidhi mahitaji au itoe kitu ambacho soko linahitaji au kuongeza thamani katika biashara husikKuna njia kadhaa zinazoweza kukusaidia kutambua mahitaji hayo, hasa kufanya utafiti na kujaribu.

Kadri unavyotafiti soko, kuna baadhi ya maswali ambayo lazima huyajibu; kuna uhitaji wa bidhaa/huduma yako?; Nani anahitaji?; Kuna mtu au kampuni zinatoa bidhaa/huduma sawa?; Ushindani ukoje? Na namna gani biashara yako itaingia sokoni?

Tengeneza mpango wa biashara
Ili biashara yako iweze kufanikiwa huna budi kuwa na mpango wa biashara wa namna ya kulifanyia kazi wazo lako. Mpango wa biashara ni muongozo utakaokuongoza katika biashara yako kuanzia hatua ya awali hadi inavyokua.

Mpango wa biashara unaweza kukupa dira sahihi ya kile unachotegemea kufanikiwa katika biashara yako na namna gani umepanga kufanya kitu hicho kiuhalisia, unaweza pia kutengeneza mpango kazi katika daftari lako na ukaendelea kuboresha kadri mda unavyosonga mbele.

Pangilia matumizi fedha
Kuanzisha biashara ndogo hakuhitaji fedha nyingi sana, lakini itakuhitaji kufanya baadhi ya uwekezaji muhimu wa mwanzo kama vile ufahamu wa biashara husika na uwezo wa kugharimia kadri unavyoendelea kabla hujaanza kupata faida.

Weka pamoja daftari linaloonyesha makadirio ya gharama ya kuanzisha na kuendeleza biashara yako kama vile vibali, leseni, ada, ushuru, bima, vifaa, utafiti wa soko, matangazo, mshahara wa wewe binafsi na wasaidizi wako, gharama ya pango, uzalishaji, gharama za usafirishaji na usambazaji.

Chagua mfumo wako wa uhasibu
Biashara ndogo zinaendeshwa vyema na kwa mafanikio zaidi ikiwa kuna mifumo rasmi ya kifedha, mapato na matumizi ikifanya kazi kwa weledi na kibunifu. Moja ya mifumo muhimu zaidi katika biashara ndogo ni pamoja na mfumo imara wa uhasibu.

Mfumo wako wa uhasibu ni muhimu ili kuunda na kuongoza bajeti yako, kupanga viwango na bei, kufanya biashara na wengine pamoja na kodi.

Tengeneza eneo la biashara
Kuandaa eneo lako la biashara ni muhimu sana katika uendeshaji wa biashara yako iwe ni kwenye ofisi yako nyumbani, ofisi binafsi ya biashara au eneo lolote biashara yako inafanyika.

Inakubidi ufikirie kwa kina kuhusu eneo, vitendea kazi na mengineyo yote yanayohusika katika biashara yako, hakikisha eneo la biashara yako linafaa kwa aina ya biashara utakayokuwa unafanya.

Andaa timu yako
Ikiwa utakuwa unaajiri watu mbalimbali wa kukusaidia katika biashara yako, basi ni wajibu wako sasa kuanza kutengeneza timu yako.

Hakikisha unapata muda wa kutosha kuainisha nafasi, wajibu na sifa unazozihitaji katika kila kitengo cha biashara yako. Utawala wa biashara ndogo una muongozo rahisi katika kuajiri watu kitu ambacho ni muhimu kwa mwenye biashara ndogo kukua na kufanikiwa.

Tangaza biashara yako
Ikiwa biashara yako tayari imeanza huna budi kuanza kuvuta wateja katika huduma/bidhaa yako. Utahitajika kuanza na mbinu na mikakati ya kimasoko na mauzo ya kipekee sana ili kuweza kufikia wateja.

Hamisi wa Bongo Star Search uwezo wake mdogo



Leo niliangalia marudio ya Bongo Star Search ya Jumapili nimeona kabisa huyo Hamisi uwezo wake wa kuimba ni mdogo sana wakati wenzake uwezo wao ni mkubwa. Na amshukuru Mungu kufika hatua ya 10 Bora, hakustahili kufika hatua hiyo.

Ifike kipindi watanzania tuache unafiki pale Bongo Star Search wanaangalia kipaji na si mtu kutia huruma na washiriki wote wameenda kwa ajili ya kutafuta nafasi ya kuonekana na pia kutafuta maisha kupitia vipaji vyao.

Hitimisho: kiukwel Bongo Star Search ya mwaka huu ndio yenye vipaji vikubwa kuliko Bongo Star Search zote kwa mtazamo wangu

By Innocent Dependent/JF

Saturday, December 14, 2019

Aliyeachiwa kwa msamaha wa Rais azua taharuki stand ya Bukoba auwa mmoja ajeruhi watano



Na Clavery Christian Bukoba Kagera.

Jeshi la polisi mkoani Kagera linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya watu wawili na majeruhi watano baada ya mtu mmoja anayesadikika kuwa ni mmoja kati ya wafungwa waliotoka jera kwa msamaha wa Rais kuwavamia na kuwashambulia kwa kuwachoma visu katika maeneo mbalimbali ya mwili katika eneo la stand kuu ya mabasi bukoba na kusababisha taharuki kubwa kwa raia.

Majeruhi watano ambao ni wananchi wa kawaida waliojeruhiwa na mtu huyo katika tukio hilo watatu wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa - Bukoba na hali zao zinaendelea vizuri japo kuwa mmoja kati yao alipata majeraha makubwa.

Kwa mujibu wa mashuhuda wanaeleza kwamba jana tarehe 13/12/2019 majira ya saa 03:00 usiku maeneo ya stand kuu ya mabasi Bukoba ghafla mtu mmoja asiyefahamika majina yake majina yake mwenye kati ya umri wa miaka 30-35 jinsia mwanaume alivamia watu waliokuwa hapo stand na kuanza kuwachoma watu visu na mtu wa kwanza kuanza kumchoma alikuwa Godfrey Gobadi miaka 30-35 ni mhaya dereva wa bajaji ambaye alimchoma kisu tumboni na kumsababishia kifo papo hapo.

Aidha mtu huyo alizidi kusababisha hofu na taharuki kubwa kwa watu wa eneo hilo alipoendelea kuwavamia na kuwachoma visu watu wengine na kujeruhi watu watano.

Baada ya mtuhumiwa kufanya vitendo hivyo wananchi wenye hasira kali walimvamia na kuanza kumshambulia na kumuumiza vibaya na baadae askari polisi waliokuwa doria waliweza kufika katika eneo hilo na kufanikiwa kumuokoa mtuhumiwa asiendelee kushambuliwa lakini alifariki wakati akipelekwa hospitalini.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amesema kuwa chanzo cha tukio hilo hakijafahamika na uchunguzi bado unaendelea.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...