Wednesday, May 6, 2026

Picha : SIMANZI SHINYANGA, MAMIA WAJITOKEZA KUMZIKA VICTORY SENGE, AZIKWA KWA HESHIMA KUBWA

Mume wa marehemu Victory Emmanuel Senge, Bw. Victor, akishiriki kushusha jeneza lenye mwili wa mkewe wakati wa mazishi yaliyofanyika Mjini Shinyanga. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mume wa marehemu Victory Emmanuel Senge, Bw. Victor, akiweka udongo katika kaburi la mkewe wakati wa maziko yaliyofanyika Mjini Shinyanga.
Mume wa marehemu Victory Emmanuel Senge, Bw. Victor, akiweka shada la maua katika kaburi la mkewe wakati wa mazishi yaliyofanyika Mjini Shinyanga.
Baba mzazi wa marehemu Victory Emmanuel Senge, Mchungaji Emmanuel Senge, akizungumza wakati wa ibada ya mazishi ya binti yake iliyofanyika Mjini Shinyanga.
Baba mzazi wa marehemu Victory Emmanuel Senge, Mchungaji Emmanuel Senge, akizungumza wakati wa ibada ya mazishi ya binti yake iliyofanyika Mjini Shinyanga.
Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa marehemu Victory Emmanuel Senge wakati wa shughuli za mazishi zilizofanyika Mjini Shinyanga.
Victory Emmanuel Senge enzi za uhai wake
Victory Emmanuel Senge enzi za uhai wake
Victory Emmanuel Senge enzi za uhai wake

****
Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kushiriki mazishi ya marehemu Victory Emmanuel Senge (35) yaliyofanyika Mjini Shinyanga, kufuatia kifo chake kilichotokea Jumamosi Mei 2, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya changamoto za uzazi.

Ndugu, jamaa, marafiki, wafanyakazi wenzake pamoja na wakazi wa Shinyanga wamejitokeza kwa wingi katika eneo la Bushushu, Mwalugoye, leo Jumatano Mei 6, 2026  kushiriki ibada ya kumuaga na safari ya mwisho ya marehemu ambaye alikuwa akiheshimika kwa wengi kutokana na utu wake na mchango wake kwa jamii.

Marehemu Victory alikuwa Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, ambapo alihudumu kwa weledi mkubwa na kujenga mahusiano mazuri na wateja pamoja na jamii kwa ujumla.

Mbali na kazi yake serikalini, marehemu pia alikuwa mfanyabiashara aliyefanikiwa na mmiliki wa maduka ya nguo ya Victorious yaliyopo Ngokolo Mjini Shinyanga, jambo lililomfanya kugusa maisha ya watu wengi kupitia ajira na huduma zake.

Ibada ya kuaga mwili ilianza nyumbani Mwalugoye kabla ya kuendelea katika Kanisa la TAG PCC Bushushu, ambako waombolezaji walipata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho na kumuombea marehemu.

Baada ya ibada hiyo, mwili wa marehemu ulisindikizwa kwenda makaburini Bushushu yaliyopo Barabara ya Shy Park ambako ulizikwa huku simanzi na huzuni vikitawala kwa waombolezaji wengi waliohudhuria.

Wengi waliomfahamu wameeleza kushtushwa na kifo chake, wakimtaja kuwa alikuwa mtu mwenye upendo, mchapakazi, mwenye moyo wa kusaidia na aliyekuwa karibu na jamii.

Kifo cha Victory Senge kimeacha pengo kubwa kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na jamii ya Shinyanga kwa ujumla, huku akikumbukwa kwa uchapakazi wake, moyo wa kujituma na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii.
Mwili wa Victory Emmanuel Senge ukiwa nyumbani kwake Bushushu Mjini Shinyanga
Mwili wa Victory Emmanuel Senge ukitolewa nyumbani kwake Bushushu Mjini Shinyanga kwa ajili ya kupelekwa Kanisani
Mwili wa Victory Emmanuel Senge ukiwasili Kanisani
Mwili wa Victory Emmanuel Senge ukiwa Kanisani



Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

SAMIA: CHEO NI SADAKA YA KUMTUMIKIA MWANANCHI, SIO KUJIKWEZA


Na mwandishi wetu, Dodoma

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amewaambia watendaji wa Serikali kuwa vyeo ni dhamana, akisema ni dhambi kubwa mtu kupata cheo kisha kuvimba mabega.

Ametoa rai hiyo leo Jumatano wakati akiwaapisha wateuliwe mbalimbali alioteua wiki iliyopita. Hafla hiyo imefanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Mkuu huyo wa nchi, amesisitiza kuwa cheo ni dhamana na dhambi kubwa ukapata cheo, ukavimbisha mabega, ukawa untouchable ‘usiyegusika’ we unanijua mi nani who are you?

Katika msisitizo wake, Dkt Samia amesema, “Narudia tena wewe nani? Wewe ni kiumbe kama wengine, ila Mungu ameamua kushika hapo. 

“Amekupa hapo ili uwatumikie watu, kama ni sadaka yako ukiwa duniani,” amesema.

Kwa mujibu wa Rais Dkt Samia kama hutumikii vyema watu, Mungu anajua na ana adhabu zake na kwamba Serikali inapitia tu, lakini mambo yote ni Mungu.

Tuesday, May 5, 2026

ROSTAM AZIZI : KENYA -TANZANIA NA KENYA ZIWE NA MFUMO MMOJA WA KIBIASHARA KUPATA MAFANIKIO ZAIDI YA BIASHARA


Mfanyabiashara mashuhuri na Mwenyekiti wa Taifa Group, Rostam Azizi akiongea katika kongamano hilo
Mwenyekiti wa Taifa Group, Rostam Azizi katika banda la maonesho la kampuni hiyo kwenye kongamano la biashara kati ya Kenya na Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo Taifa Group ambayo ni kampuni mama ya Taifa Gas ilkuwa mdhamini mkuu wa kongamano hilo.
Mwenyekiti wa Taifa Group,Rostam Azizi katika picha ya pamoja na Maofisa Waandamizi wa Taifa group na Taifa Gas kwenye banda la maonesho la kampuni hiyo kwenye kongamano la biashara kati ya Kenya na Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo Taifa Group ambayo ni kampuni mama ya Taifa Gas ilikuwa mdhamini mkuu wa kongamano hilo.
Muonekano wa banda la maonesho la kampuni ya Taifa Group kwenye kongamano la biashara kati ya Kenya na Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo Taifa Group ambayo ni kampuni mama ya Taifa Gas ilkuwa mdhamini mkuu wa kongamano hilo.
#Watanzania wasiwaogope Wakenya katika masuala ya biashara na ajira na Wakenya waache kushabikia matatizo na majanga yanayotokea Tanzania.

 **

Mfanyabiashara mashuhuri na Mwenyekiti wa Taifa Group, Rostam Azizi. ametoa wito wa kuanzishwa kwa mfumo mmoja wa kibiashara ili kuharakisha mtiririko wa uwekezaji, kuhamasisha mitaji, na kufungua fursa zilizopo za biashara kati ya Kenya na Tanzania.

Akizungumza katika Kongamano la biashara kati ya Kenya na Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais William Ruto—Azizi alizihimiza jumuiya za wafanyabiashara wa nchi hizi mbili kuharakisha mchakato wa ujumuishaji wa kiuchumi ili kuimarisha biashara na kuvutia uwekezaji mkubwa na wa kati.

Kampuni ya Taifa Group,kampuni mama ya kampuni kinara ya usambazaji wa nishati ya gesi ya Taifa Gas ndiyo ilikuwa mdhamini mkuu wa kongamano hili kubwa la kihistoria.

“Tunapaswa sasa kutia mkazo kwenye ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kujenga mfumo mmoja wa kibiashara utakaofungua njia ya kuvutia uwekezaji mkubwa kati ya Kenya na Tanzania,” alisema.

Pia alihimiza Watanzania kuondokana na hofu ya kuwaogopa Wakenya katika masuala ya ajira ya biashara vilevile Wakenya kuacha kushabikia matatizo na majanga yakitokea nchini Tanzania.

Azizi alibainisha kwamba sekta binafsi ina jukumu muhimu katika kuhamasisha mitaji, kufungua fursa mpya za masoko, na kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani katika nchi zote mbili. 

Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi ujumuishaji wa makusudi na wa kina kiuchumi.

“Tuunganishe sekta binafsi za nchi zetu mbili kupitia miradi ya pamoja, tukifungua fursa za manufaa ya pande zote na kupanua upatikanaji wa masoko ya kimataifa,” aliongeza.

Rostam Azizi alizungumzia fursa hizo wakati wa mjadala wa jopo kuhusu nafasi ya sekta binafsi katika kufungua uwezo wa kiuchumi na kuharakisha utendaji wakati wa kongamano. Tukio hilo lilihudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mgeni wake Rais wa Kenya William Ruto.

Katika ziara hiyo ya siku mbili, Rais Ruto alieleza matumaini ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya Kenya na Tanzania kupitia mikataba ya biashara na uwekezaji yenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 500. Hatua hiyo inaashiria msukumo mpya wa kuimarisha mojawapo ya njia muhimu zaidi za kiuchumi katika Afrika Mashariki.

Mikataba hiyo inatarajiwa kuibuka kutoka Kongamano la Biashara kati ya Kenya na Tanzania 2026, ikijumuisha sekta muhimu kama nishati, usafiri, TEHAMA, na kilimo. Zaidi ya mikutano 200 ya biashara baina ya wafanyabiashara (B2B) imepangwa ili kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi kati ya uchumi hizo mbili.

Wachambuzi wanaona ushirikiano huu kama mwelekeo mpya kuelekea diplomasia ya kiuchumi inayolenga utekelezaji katika Afrika Mashariki.

Biashara kati ya Kenya na Tanzania imekua kwa kasi kwa miaka mingi, ikionyesha uhusiano imara wa kiuchumi kati ya nchi jirani. Kama wanachama muhimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), mataifa haya yanafaidika na kupunguzwa kwa vikwazo vya biashara na kuboreshwa kwa ujumuishaji wa kikanda, hali inayochochea kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa bidhaa na huduma.

Kenya inaendelea kuwa miongoni mwa wabia wakubwa wa biashara wa Tanzania, ikisafirisha bidhaa za viwandani kama vyakula vilivyosindikwa, saruji, plastiki, na mashine. 

Kwa upande wake, Tanzania husambaza Kenya bidhaa za kilimo, madini, na malighafi, ikiwa ni pamoja na mahindi, mchele, na dhahabu. Uhusiano huu wa kibiashara unaokamilishana umechangia ongezeko la mara kwa mara la kiwango cha biashara kati ya nchi hizi mbili.

Katika miaka ya hivi karibuni, biashara kati ya Kenya na Tanzania imefikia mabilioni ya dola kila mwaka, ikichochewa na uboreshaji wa miundombinu kama barabara zilizoboreshwa, vituo vya mipakani vilivyoboreshwa, na bandari zilizoimarishwa. 

Kuanzishwa kwa vituo vya mpaka wa pamoja (one-stop border posts)—hasa Namanga na Holili/Taveta—kumepunguza ucheleweshaji na kuongeza ufanisi, hivyo kufanya biashara ya mpakani kuwa ya haraka na yenye kutabirika zaidi.

Licha ya mafanikio hayo, changamoto bado zipo. Migogoro ya mara kwa mara ya biashara, tofauti za kanuni, na vikwazo visivyo vya ushuru wakati mwingine vimeathiri mtiririko wa bidhaa. Hata hivyo, mazungumzo yanayoendelea ndani ya mfumo wa EAC yanaendelea kushughulikia masuala haya na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Kwa mtazamo wa baadaye, matarajio ya biashara kati ya Kenya na Tanzania yanaendelea kuwa mazuri. Uwekezaji endelevu katika miundombinu, uratibu wa sera za biashara, na upanuzi katika sekta zinazoibukia kama biashara ya kidijitali na huduma vinaweka msingi imara wa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi.

Kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Kenya kimeonyesha ukuaji wa mara kwa mara. Mwaka 2024, mauzo ya nje ya Kenya kwenda Tanzania yalifikia Sh67.20 bilioni, yakionyesha mwelekeo wa juu licha ya kushuka kidogo mwaka 2020. Uagizaji wa bidhaa ulikuwa Sh58.72 bilioni, na kusababisha ziada ya biashara ya Sh8.48 bilioni.

Kupungua kwa pengo la biashara kunaashiria haja kwa Kenya kuongeza ushindani na kubadilisha wigo wa bidhaa zake za kuuza nje. Hata hivyo, nchi zote mbili zinaendelea kujitolea katika mikataba ya kibiashara ya kikanda inayosaidia ukuaji wa uchumi na ujumuishaji.

Biashara ya pande mbili tayari imevuka $1 bilioni, ikisisitiza umuhimu wa kimkakati wa Kenya na Tanzania kama nguvu kuu katika uchumi wa Afrika Mashariki.

MBUNGE MWAKIOJA ATANGAZA NEEMA YA SOKA WILAYA MKINGA





>Agawa vifaa vya michezo kwa timu zote zinazoshiriki Ligi ya wilaya ya Mkinga


Na Oscar Assenga, MKINGA

Mbunge wa Jimbo la Mkinga mkoani Tanga, Twaha Mwakioja, ameahidi kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo kuinua kiwango cha soka wilayani humo kwa kuwekeza katika elimu na maendeleo ya waamuzi pamoja na makocha.

Akizungumza wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii uliokwenda sambamba na uzinduzi wa Ligi ya Wilaya ya Mkinga, uliofanyika katika Uwanja wa Chamazi, Kata ya Matamba, Mwakioja alisema lengo lao ni kuwekeza katika michezo kwa vijana ili kuwapatia ajira, kuboresha afya zao, pamoja na kuimarisha amani, mahusiano mema na ushirikiano miongoni mwao.

Alieleza kuwa dhamira yao ni kuwashika mkono vijana ili waweze kupiga hatua kutoka ngazi ya wilaya, kwenda mkoa, kanda na hatimaye ligi za juu, huku yeye akiwa bega kwa bega nao kuhakikisha wanafikia malengo yao.

Mbunge huyo alibainisha kuwa wamepata taarifa ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa makocha na waamuzi wenye sifa. Hivyo, wamejipanga kuwekeza katika mafunzo ya makocha ili kila kata iwe na angalau kocha mmoja mwenye ujuzi na mafunzo rasmi, pamoja na kuandaa waamuzi wenye vyeti ili kuboresha usimamizi wa michezo.

Alisisitiza kuwa uwekezaji huo utaenda sambamba na ushirikiano na Chama cha Soka Wilaya ya Mkinga katika kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana.

Aidha, alisema mpango wao ni kuhakikisha kila kata na kijiji kinakuwa na timu ya mpira wa miguu inayoshiriki ligi ya wilaya. Aliongeza kuwa watawekeza zaidi ili kuibua timu imara zitakazoweza kushiriki ligi za ngazi ya mkoa, kanda na hatimaye Ligi Kuu, hatua itakayosaidia kuitangaza Mkinga katika ramani ya soka nchini.

Katika kuonyesha dhamira hiyo, Mwakioja alikabidhi jezi na mipira kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha na kusaidia maendeleo ya michezo wilayani humo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Mkinga, Fadhili Habibu, alisema ratiba ya ligi hiyo imeanza Mei 4 katika kituo cha Mkinga, huku kituo cha Maramba kikitarajiwa kuanza Mei 6 (Jumatano), ambapo kutakuwa na vituo vinne vitakavyochezwa katika Kijiji cha Maramba, ikiwa ni pamoja na mechi kati ya Viva Dynamo na Maramba FC.

Habibu alisema lengo la ligi hiyo ni kusimamia na kuibua vipaji vya vijana, pamoja na kuwapa mwelekeo wa maendeleo yao kisoka. Alimshukuru mbunge kwa kujitoa na kushirikiana nao katika kufanikisha malengo hayo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Mkinga, Hassan Zumo, alimpongeza mbunge kwa juhudi zake za kuendeleza michezo wilayani humo, akieleza kuwa hatua hiyo imeongeza hamasa na matarajio ya ushindani mkubwa katika ligi hiyo, hasa baada ya timu kukabidhiwa vifaa.

Zumo aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2008, wamekuwa wakipeleka vilabu katika mashindano ya ngazi ya mkoa lakini wamekuwa wakikwama kutokana na changamoto za kifedha. Hata hivyo, alisema kupitia uongozi wa Mbunge Mwakioja, wana matumaini ya kupata timu itakayoweza kufika hadi Ligi Kuu.

Aidha, timu zinazoshiriki mashindano hayo zimeahidi kujituma na kupambana kwa juhudi zote ili kuhakikisha ligi hiyo inaleta mafanikio na tija kwa vijana wa Wilaya ya Mkinga.

Monday, May 4, 2026

RAIS RUTO AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA KUUNDA TUME YA JAJI CHANDE



Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuunda Tume ya Jaji Othman Chande kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Ruto ametoa pongezi hizo alipowasili nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya uongozi makini na wenye kuwajibika katika kushughulikia changamoto za kitaifa kwa njia ya kisheria na kiutawala.

Amesema kuundwa kwa tume hiyo kunaonesha dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kutafuta ukweli wa kilichotokea na kuhakikisha masuala yote yanayohusu amani na utulivu yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu ndani ya mipaka ya nchi.

Kwa mujibu wa Rais Ruto, juhudi hizo zinaungwa mkono na nchi za Afrika Mashariki, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kikanda kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa ukanda huo.

Ameongeza kuwa kutokana na uzoefu wa Kenya katika nyakati kama hizo, ana imani Tanzania itaweza kupitia kipindi hicho na kuibuka imara zaidi, huku akiahidi ushirikiano na nia njema katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.

Tume ya Jaji Othman Chande iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaDkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuimarisha utawala bora na kudumisha amani nchini.

MCHENGERWA: BIMA YA AFYA KWA WOTE IWE KIPAUMBELE BAJETI YA 2026/27

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesisitiza kwamba bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 inapaswa kutoa mwelekeo wa Taifa katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Mchengerwa amesema hayo Jumapili Mei 03, 2026 wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya kilichofanyika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza.

"Lazima tujiandae kikamilifu kwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Hili si suala la kadi pekee bali lazima kuwe na utayari wa miundombinu, mifumo, dawa na rasilimali watu imara" alisema Mchengerwa.

Mchengerwa alisisitiza kwamba lazima mifumo ya TEHAMA iwe imara, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba uimarishwe huku akiweka mkazo kwa buzalishaji wa ndani kupewa kipaumbele na Wizara ya Afya.

"Lazima mifumo ya manunuzi itoe kipaumbele kwa wazalishaji wa ndani. Katibu Mkuu nakuagiza usimamie hilo, ununuzi kupitia MSD na mifumo yetu ya manunuzi lazima izingatie hilo lakini kwa kuzingatia ubora" ameongeza.

Mchengerwa aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kupiga hatua ikiwemo kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu kufikia wastani wa asilimia 73 kwa mwezi Februari, 2026.

"Pia tumeendelea kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kupitia uwekezaji katika vituo vya afya, hospitali za wilaya, vifaa tiba na rasilimali watu. Haya ni mafanikio ya pamoja chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan" alisema Mchengerwa.

Pia alitoa wito kwa kila mtumishi, kuanzia makao makuu hadi hospitali za rufaa, kutoka idara hadi kituo cha afya, kuhakikisha wanatoa huduma kwa weledi na huruma kwa wananchi.

"Hatutavumilia ucheleweshaji wa huduma usio na sababu. Hatutavumilia upendeleo unaodhalilisha haki za mwananchi" alisisitiza Mchengerwa huku akiagiza Katibu Mkuu kufanyia kazi malalamiko ya wagonjwa kukaa muda mrefu bila kupata huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Seif Shekalaghe alisema kikao hicho kimelenga kujadili na kupitisha mwelekeo wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 yenye lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi pamoja na ustawi wa watumishi.

Naye Katibu wa Baraza hilo, Vivian Joseph ambaye ni Afisa Tawala Mkuu Wizara ya Afya alisema kupitia kikao hicho kitasaidia upatikanaji wa bajeti ambayo ni shirikishi kutekelezwa na watumishi wa wizara hiyo baada ya kupitishwa na bunge.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe akizungumza kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo kilicholenga kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka 2026/27.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe akizungumza kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi Wizara ya Afya kilichoketi jijini Mwanza.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.

Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...