Tuesday, April 29, 2025

Airtel yazindua teknolojia ya Akili Mnemba kupambana na utapeli


Airtel Tanzania imezindua huduma maalum ya kutoa taarifa kuhusu utapeli kupitia Akili Mnemba ya ambayo imetengenezwa mahususi kwa ajili ya kuwatahadharisha wateja dhidi ya ulaghai na utapeli ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza hatua za kupambana na uwepo wa utapeli kwa njia ya simu nchini Tanzania. 

Kuanzishwa kwa huduma ya Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli nchini Tanzania inafuatia mafanikio ya uzinduzi wa teknolojia hiyo ya Akili Mnemba nchini Nigeria na Uganda wakati kampuni hiyo ya mtandao wa simu inavyoendelea kuboresha uzoefu wa wateja kwa kuwa huduma hiyo itakuwa inapatikana kwenye simu janja na simu za kawaida zote kwa ajili ya jumbe zinazoshukiwa kuwa za kitapeli. Haihitaji kupakua aplikesheni kwa kuwa inapatikana kwa wateja wote wa Airtel. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa aliipongeza Airtel kwa kutengeneza teknolojia ya kibunifu nchini akiongeza kuwa huduma hiyo ya kimapinduzi ya Airtel Spam Alert Service-Kataa Matapeli itakuwa na mchango muhimu katika kuunga mkono jitihada za serikali kutatua utapeli nchini Tanzania.

"Huduma ya Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli, inayotumia Akili Bandia kugundua ulaghai mtandaoni, inaendana moja kwa moja na juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na wanaweza kuepuka matapeli wa simu kwa haraka zaidi," alisema.

Waziri Silaa alisisitiza kuwa hatua iliyochukuliwa na kampuni ya simu inaendana na kampeni inayoendelea ya kitaifa dhidi ya udanganyifu wa simu za mkononi iitwayo #Sitapeliki, inayolenga kuelimisha umma na kuwawezesha kutambua na kuepuka matapeli wa simu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema kuwa suluhisho hili la kisasa la AI ni uthibitisho wa dhamira ya Airtel kuwawezesha wateja wake dhidi ya vitisho vinavyotokana na matapeli wa simu za mkononi, na kwamba huduma ya Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli inapatikana kwa watumiaji wote wa simu janja na simu za kawaida.

"Huduma ya Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli tayari inapatikana kwa wateja wote wanaotumia simu janja au simu ya kawaida, na muhimu zaidi, wateja wetu hawatahitajika kupakua programu yoyote au kufuata hatua za kuiwasha. Hii si tu tangazo la teknolojia kuhusu hatua muhimu ya kulinda wateja, bali ni tamko kwamba Airtel Tanzania si mtandao wako tu, bali pia ni mlezi wako wa kidijitali. Tumejitoa kikamilifu kuwawezesha wateja wetu kuwa makini na kuwapa imani ya kufurahia manufaa ya mawasiliano ya kidijitali," alisema.

Kamoto pia alitoa wito kwa wadau wa sekta ya mawasiliano kuunga mkono juhudi zinazolenga kukabiliana na udanganyifu wa simu katika jamii.

Monday, April 28, 2025

MKURUGENZI JAMII AFRICA : UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NI HAKI, SI HISANI...ATAHADHALISHA MATUMIZI MAKUBWA YA AKILI MNEMBA WAKATI WA UCHAGUZI


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo amesema uhuru wa vyombo vya habari si hisani bali ni haki ya msingi ambayo kila mwananchi anapaswa kuipata na kuitetea akisisitiza kuwa dunia ya leo inahitaji zaidi uwezo wa kuchambua, kutathmini na kuelewa taarifa kwa undani, kuliko wakati mwingine wowote.

Akizungumza leo Aprili 28, 2025 katika mjadala maalum kuhusu Athari za Akili Mnemba (AI) katika Mustakabali wa Uandishi wa Habari wakati maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayoendelea katika hoteli ya Gran Melia jijini Arusha, Melo amesema mapambano ya kulinda uhuru wa habari hayawezi kuachiwa waandishi peke yao bali ni jukumu la jamii nzima.

"Uhuru wa habari hauwezi kuonekana kama zawadi inayotolewa kwa neema. Ni haki yetu ya kuzaliwa kama binadamu huru. Katika enzi ya taarifa nyingi, akili mnemba ndiyo silaha kuu ya kulinda uhuru huu," amesisitiza Melo.

Mageuzi ya Vyombo vya Habari

Melo ameelezea kuwa tasnia ya habari imepiga hatua kubwa, kutoka kwenye magazeti, redio na televisheni hadi kwa watengeneza maudhui wa kidijitali kama wanablogu, vloggers na podcasters.

Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo

Katika hali hii mpya, amesema, uhuru wa habari haupaswi kulindwa kwa vyombo vya habari vikuu pekee, bali kwa wote wanaoshiriki kusambaza taarifa kwa umma.

"Kila mmoja anayeshiriki katika mnyororo wa mawasiliano ya kisasa waandishi huru, wapiga picha, vloggers , anapaswa kuheshimiwa na kulindwa chini ya kanuni za uhuru wa habari," amesema.

Umuhimu wa Akili Mnemba

Kaulimbiu ya mwaka huu, "Uhabarishaji katika Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba kwenye Uhuru wa Vyombo vya Habari", inaangazia hitaji la kutumia akili mnemba kuchuja taarifa za kweli dhidi ya propaganda na habari potofu.

Kwa mujibu wa ripoti ya UNESCO ya mwaka 2023, uwezo wa kupima ubora wa taarifa umetajwa kama "ujuzi muhimu zaidi katika karne ya 21".

Melo amesisitiza kuwa bila akili mnemba miongoni mwa wanahabari na wananchi, tasnia ya habari iko katika hatari ya kudhibitiwa na taarifa za kupotosha zinazochochewa na maendeleo ya teknolojia kama AI.

Athari za AI katika Mustakabali wa Uandishi wa Habari

Mkurugenzi huyo wa JamiiAfrica ameonya kuwa tunapokaribia Uchaguzi Mkuu wa 2025, matumizi ya teknolojia ya kidijitali na Akili Bandia (AI) yatashika kasi kubwa kuliko wakati mwingine wowote nchini.

Amesema tayari katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, matumizi ya AI yalishuhudiwa na sasa JamiiAfrica kwa kushirikiana na wadau kama Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) inaendelea kuwajengea uwezo wadau wa siasa kutumia teknolojia kwa njia salama na yenye uwajibikaji.

"Tunapopokea fursa ya teknolojia mpya, lazima tuwe na uelewa wa kina kuhusu athari zake kwa uhuru wa kujieleza. AI inaweza kutumiwa kuharakisha kazi za habari, lakini pia inaweza kuwa chombo cha kusambaza taarifa za uongo ikiwa haitasimamiwa kwa makini," ameonya Melo.

Uhuru wa Vyombo vya Habari Katika Kipindi cha Uchaguzi

Akizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu, Melo ametoa wito kwa vyama vya siasa, mamlaka na jamii kulinda mazingira ya kazi za waandishi wa habari.

"Ni kipindi kama hiki ambapo uhuru wa vyombo vya habari hupimwa kwa vitendo si maneno. Lazima tuheshimu haki ya kila mwananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati," amesema.

 Hatua Tunazopaswa Kuchukua

Katika dunia inayoongozwa na data na teknolojia za kisasa, ujumbe wa Maxence Melo unaacha somo muhimu: uhuru wa habari hautegemei huruma ya watawala au mitandao ya kijamii, bali unalindwa kwa uwezo wetu wa kufikiri kwa kina, kuchambua kwa makini, na kusimamia ukweli bila woga.

"Akili mnemba ndiyo silaha yetu dhidi ya taarifa za uongo. Na uhuru wa habari si zawadi — ni haki yetu ya kuzaliwa," amesema Melo.

Ushirikiano wa Kimataifa

Katika maadhimisho hayo, viongozi wengine akiwemo Balozi wa Sweden nchini Tanzania, H.E. Charlotta Ozaki Macias, na mwakilishi wa UNESCO, Michael Toto, wameelezea umuhimu wa kulinda uhuru wa habari katika enzi ya teknolojia mpya kama AI.

 
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, H.E. Charlotta Ozaki Macias

Balozi Macias amekumbusha kuwa maendeleo ya AI yanapaswa kudhibitiwa kwa misingi ya kulinda faragha, kupambana na upendeleo, na kuimarisha usawa, huku akitoa mfano wa juhudi za Sweden katika kuhakikisha AI inatumikia binadamu.

Kwa upande wake, mwakilishi wa UNESCO, Michael Toto, amekumbusha kuwa mwaka 2024 pekee, zaidi ya waandishi 90 waliuawa ulimwenguni kote kwa ajili ya kuhabarisha ukweli. Alisisitiza kuwa uandishi wa habari ni nguzo ya demokrasia, uwajibikaji na amani duniani.

Maadhimisho haya ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2025 yanaendelea Arusha hadi Aprili 30, yakiratibiwa na JamiiAfrica kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, UNESCO, na wadau mbalimbali wa habari ikiwemo MISA Tanzania.

Wazungumzaji wakijadili kuhusu Athari za Akili Mnemba(AI) katika Mustakabali wa Uandishi wa Habari​ - Picha na Kadama Malunde




Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...