Tuesday, February 25, 2020

Umoja wa Ulaya upo tayari kwa mazungumzo magumu na Uingereza

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wanasema umoja huo uko tayari kwa mazungumzo juu ya mahuasiano ya baadaye na Uingereza, ikiwa ni kuanzia biashara hadi usalama, lakini mchakato huo utakuwa mgumu sana na unaweza kushindwa iwapo Uingereza haitatatua mzozo kuhusu mpaka wa Ireland kama ilivyokubaliwa awali.

Uingereza ilijitoa kutoka Umoja wa Ulaya hapo Januari 31, baada ya zaidi ya miaka mitatu ya mazungumzo ya talaka, ambayo yaliingia katika utata kutokana na suala hilo nyeti la mpaka wa Ireland ambao una historia ya machafuko, mpaka pekee wa nchi kavu katika kundi hilo la mataifa na Uingereza kwa sasa.

Wakati pande zote zikitoa matamshi makali kabla ya majadiliano hayo ambayo yanatarajiwa kuanza wiki ijayo, Ireland imeonya kuwa hata makubaliano ya msingi ya biashara hayatawezekana ifikapo mwishoni mwa mwaka huu iwapo Uingereza haitakubaliana na majukumu ya mpaka kama ilivyokubaliwa katika makubaliano ya kujitoa.
Source

SIMBA SC YAING’OA KWA MATUTA STAND UNITED CCM KAMBARAGE



MABINGWA wa soka Tanzania, Simba SC wamefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa penalti 3-2 kufuatia sare ya 1-1 na wenyeji, Stand United jioni ya leo Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere alikosa penalti ya pili katika mchezo wa pili mfululizo leo baada ya mkwaju wake kupanguliwa na kipa wa Stand United, Murtala Hamad ambao ndio ulifungua ngwe ya matuta leo.

Kagere alikosa penalti pia kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, ingawa Simba SC iliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Biashara United naye akifunga bao la pili siku hiyo.
Waliofunga penalti za Simba SC leo ni viungo, Mzambia Clatous Chama, Mkongo Deogratius Kanda na mzawa, Hassan Dilunga, wakati Ibrahim Ajibu shuti lake liligonga mwamba wa juu na kupotelea nje.

Kwa upade wa Stand United penalti zao zilifungwa na Fakhi Juma na Brown Raphael, huku Miraj Saleh akigongesha mwamba, Majid Kimbondile akipiga juu kabisa na Maulid Fadhil akagongesha mwamba wa kulia mpira kwenda nje.

Awali Simba walitangulia kwa bao la mkwaju wa penalti wa Dilunga dakika ya 51, kufuatia beki wa Stand United, Antidius Ishengoma kuunawa mpira kwenye boski, kabla ya wenyeji kusawazisha kupitia kwa Miraj Saleh dakika ya 67.

Stand United ilimaliza pungufu mchezo huo, baada ya mchezaji wake, Abdi Mwite kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 75 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kujiangusha.

Kikosi cha Stand United kilikuwa; Murtala Hamad, Severine Charles, Antidius Ishengoma, Yela Mboma, Majid Kimbondile, Fakhi Juma, Amri Msenda, Abdi Mwete, MIraj Saleh, Maulid Fadhil na Zamogoni Pangapanga/Brown Raphael. 

Simba SC; Benno Kakolanya, Haruna Shamte, Gardiel Michael, Tairone Santos, Kennedy Juma, Gerson Fraga 'Viera', Hassan Dilunga, Sharaf Eldin Shiboub/chama, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu na Shiza Kichuya/kanda. 

Mechi nyingine za 16 Bora leo, Sahare All Stars iliungana na Simba kutinga Robo Fainali baada ya kuwachapa Panama FC 5-2 Jijini Dar es Salaam, Namungo FC nayo ikaichapa 2-1 Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wakati Ndanda SC ikashinda 2-1 dhidi ya Kitayosa FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Hatua ya 16 Bora itakamilishwa kesho kwa mechi nyingine nne, Yanga wakiwakaribisha Gwambina FC Uwanja wa Uhuru, JKT Tanzania na Alliance FC, Dar es Salaam, Kagera Sugar na KMC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Ihefu FC dhidi ya mabingwa watetezi, Azam FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Sunday, February 23, 2020

Serikali yajipanga kutokomeza magonjwa ya mifugo nchini

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema serikali itahakikisha inaendelea kutoa dawa za ruzuku za kuogeshea mifugo nchini ikiwa na lengo la kutokomeza kabisa magonjwa ya mifugo.

Naibu Waziri Ulega amesema hayo (22.02.2020) wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika mnada wa mifugo wa Ndelema uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Handeni Mkoani Tanga ambapo amewataka wafugaji kutoacha kuosha mifugo yao kwani kwa kufanya hivyo mifugo itakuwa na afya njema na hatimaye kupata bei nzuri ya soko.


"Mwaka jana tulipata pesa kutoka kwa mheshimiwa rais zaidi ya Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kununua dawa na kugawa kwa majosho 1,400 nchi nzima, mwaka huu wametuongeza tumepata zaidi ya Shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kununua dawa na kusambaza katika majosho 1,700 tutaendelea na zoezi hilo la kutoa dawa za ruzuku bila kuacha ili kuhakikisha tunapiga kabisa vita magonjwa ya mifugo." Amesema Mhe. Ulega

Aidha kuhusu wafugaji wa Wilaya ya Handeni kuingiza mifugo yao katika misitu ya serikali Naibu Waziri Ulega akizungumza moja kwa moja kwa njia ya simu katika mkutano huo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo amemtaka kuweka alama katika misitu hiyo ili wafugaji waweze kutambua misitu ya serikali na kutoingiza mifugo yao kwa bila kukusudia.

Prof. Silayo amemuahidi Naibu Waziri Ulega katika mkutano huo kuwa atawatuma wataalamu siku ya Jumatatu ili kuanza utekelezaji huo mara moja na kuondoa migogoro ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika misitu ya serikali.

Katika mkutano huo pia naibu waziri huyo ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni kuhakikisha unatua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo ikiwemo ya miundombinu katika mnada huo pamoja na barabara ili waweze kusafirisha mifugo yao kwa urahisi zaidi.

Nao baadhi ya wafugaji waliopatiwa nafasi kuuliza maswali na kutoa maoni yao juu ya sekta ya mifugo, wameipongeza serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikihakikisha inawaboreshea mazingira ya shughuli zao huku wakiomba wazidi kupatiwa elimu zaidi ya masuala mbalimbali ili wafanye shughuli zao bila kukiuka sheria za nchi.

Awali akitembelea bwawa la asili katika Kijiji cha Kweingoma kilichopo Wilaya ya Handeni Vijijini Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi katika bwawa hilo lenye urefu wa Kilometa Nne kujiunga katika ushirika ili serikali iweze kuwasaidia katika maeneo mbalimbali huku akiahidi kutoa mashine kwa ajili ya mtumbwi utakaotengenezwa na uongozi wa wilaya hiyo ili kurahisisha shughuli za uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemaliza ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Tanga ambapo amepita pia katika Wilaya za Muheza, Pangani, Mkinga na Halmashauri ya Jiji la Tanga na kuzungumza na wafugaji na wavuvi ili kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo.

Saturday, February 22, 2020

Aina 8 za watu ambazo ni sumu unatakiwa kuwaepuka maishani mwako

Watu wasiofaa wapo kila mahali, kwa hakika wanakwaza na kurudisha maendeleo ya watu nyuma. Ukiwa kama mjasiriamali au mtu mwingine yeyote unatakiwa kufanya bidii kufikia malengo yako bila kuruhusu aina za watu wasiofaa kukuvuruga.

Inawezekana unawafahamu watu ambao ni sumu; yawezekana wanafanya kazi na wewe, ni marafiki zako au unaishi nao. Kadri unavyowaepuka katika maisha au kazi yako ndivyo mambo yatakavyozidi kuwa mazuri.

Fuatana nami katika makala hii nikushirikishe aina 8 za watu ambazo ni sumu unazotakiwa kuziepuka katika maisha yako.

1. Watu wanaohoji kila kitu
Watu wanaohoji kila kitu hutafuta njia ya kupinga na kukosoa kila unachokifanya. Utatumia muda mwingi kuwaelewesha lakini watasikia kwa sikio moja na swala hilo kutokea sikio la pili. Kujaribu kutafuta msaada na ushauri kutoka kwa watu wa aina hii ni kupoteza muda.

Watu hawa huwa na maswali kama vile kwanini unafanya hivi? Unapoteza muda; si jambo zuri; la fulani liliharibika; nani kakuambia ufanye; nitapata nini mimi? hauwezi kufanikiwa kwenye hili labda tafuta jingine; linahitaji fedha nyingi mno n.k.

2. Wenye wivu
Safari ya mafanikio ina milima na mabonde, hivyo ni vyema kuwa na watu ambao watakuinua na kukutia moyo unapopita katika changamoto. Watu wenye wivu huamini kuwa kila kitu kizuri kinatakiwa kitokee kwao tu.

Watu hawa watafurahia unapopata matatizo tu, wala hawatakusaidia wakati wa changamoto. Hivyo ni vyema ukajiepusha na aina hii ya watu ili uweze kufanikiwa katika maisha yako.

3. Wajuaji
Wajuaji hawako tayari kuambiwa au kuelekezwa kitu chochote, kulingana na wao wanajua kila kitu na wanajua njia bora ya kufanya kila kitu. Si kwamba watu hawa hawahitajiki katika maisha ya mtu binafsi pekee, bali hata katika mazingira ya kazi.

Katika maisha upo usemi unaosema kuwa "wapishi wengi huharibu mchuzi". Hivyo basi, kwa kuwa wajuaji hujifanya wanajua kila kitu na  hawako tayari kupokea maelekezo, basi ni vyema ukawaepuka wasije wakakukwamisha.

4. Wenye kiburi
Watu wenye kiburi wamejaa katika jamii inayotuzunguka. Watu wenye kiburi hawaambiliki wala kushaurika, wao hufikiri ni bora kuliko kila mmoja anayewazunguka.

Unapofanya kazi na mtu mwenye kiburi ni vigumu kukaa naye pamoja mkapanga majukumu na yakatekelezwa; hivyo ni bora kuwaepuka.

5. Watu wenye visingizio na walalamikaji
Watu wa aina hii huwa hawaishiwi sababu, wao hulaumu kila kitu na kila mtu. Watu hawa hawakubali kupokea majukumu bali huwanyoshea wengine vidole; pia hawako tayari kuwajibika kutokana na makosa yao.

Mara nyingi watu hawa husingizia kitu au mtu mwingine kwa kila kosa wanalolifanya. Waondoe kwenye maisha, biashara au ofisi yako sasa ili uishi kwa amani na kuwa na mafanikio.

6. Wale wenye mawazo hasi au wapinzani
Mtu mwenye mawazo hasi atakausha nguvu zako za mawazo chanya. Watu hawa kila mara hujitahidi kukuvuta chini ili ufanane nao na kuamini kile wanachokiamini. Kamwe huwezi kupokea neno la hamasa kutoka kwao.

Watapuuza kila wazo jema ulilo nalo, watatafuta kila njia ya kukuonyesha jinsi utakavyoshindwa katika wazo lako kuliko utakavyofanikiwa. Hivyo ni vyema ukachukua hatua mapema ya kuwaepuka watu hawa.

7. Watu waongo
Ili kufanikiwa katika maisha unahitaji kuwa na watu ambao wanaaminika na kutegemewa. Unapokuwa na watu waongo ni vigumu kufanikiwa kwani utaamani mambo au taarifa fulani kumbe hazina ukweli wowote.

Hebu fikiri unafanya kazi na mhasibu mwongo; ataiba pesa au kupoteza taarifa kisha atakudanganya kuwa hajafanya hivyo; je unajua nini kitatokea? Utapata hasara; hivyo basi jitahidi kujiweka katikati ya watu wakweli.

8. Wambea
Aina hii ya watu ipo kila mahali, ofisini, nyumbani, shuleni n.k. Watu wambea hawawezi kutofautisha uzushi au uvumi na ukweli.

Watu wambea husambaza taarifa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine; kwa ufupi mtu anayekuambia taarifa za mwingine ndiye yeye huwaambia wengine taarifa zako. Wambea hutengeneza mazingira mabaya ya kazi yenye chuki na ugomvi. Hivyo ni vyema kuwaondoa watu hawa katika maisha, biashara au ofisini kwako.

Nakukumbusha usemi usemao "ukikaa na waridi pia utanukia"; hivyo ukikaa na watu wabaya pia watakuwa na athari mbaya katika maisha yako. Jitahidi kujiweka katika mazingira yenye watu wanaopenda kufanikwa na wenye mawazo chanya.

Thursday, February 20, 2020

Msanii ROSA Ree Amkana Mwanamuziki TIMMY Dat Live...


Ukaribu wa Msanii Rosa Ree na Timmy Dat kutoka kenya unaonekana kupungua toka Video aliyoshirikishwa ya Vitamin U iwaletee Shida ya Rosa Ree Kufungiwa na Kulipa Faini ya Milioni mbili Basata

Ukaribu wao ulisababisha watu kufikiria kuwa wana mahusiano ya kimepenzi japo wenyewe wamekuwa wakikataa kuhusu hili, Baada ya ile Video Rosa Ree Alifuta picha zote za jamaa na kuacha kumpost kama tulivyozoea .

Sasa leo huko Instagram Rosa amepost picha yenye Caption 'Niulize Chochote Nitakujibu"

Katika Maswali aliyoulizwa Wengi wanauliza kama yupo kwenye uhusiano na Timmy Dat lakini Rosa Ree yote amejibu "NO" kuonesha kuwa ni hapana Hawana Mahusiano




Wednesday, February 19, 2020

Urusi na Ukraine Zarushiana Makombora

Ukraine imesema mwanajeshi wake mmoja ameuawa na wengine kadhaa wamepata majeraha, katika makabaliano na vikosi vya Urusi ambavyo Ukraine imesema viliingia kwenye ardhi yake.

Tangazo la wizara ya ulinzi limesema kuwa mapigano hayo yalitokea katika mikoa minne ya mashariki mwa Ukraine ambayo ina wakaazi wachache.

Wizara hiyo imesema imeweza kujibu mapigo ya iliyemtaja kuwa adui yake, na kuweza kudhibiti hali ya mambo katika mkoa wa Luhansk.

Aidha, kulingana na tangazo hilo, mwanajeshi mmoja wa upande wa wanamgambo wanaoungwa mkono na Urusi ameuawa pia.

Kila upande unaushutumu mwingine kuvunja makubaliano yaliyosainiwa, yakihimiza kuondolewa kwa silaha nzito nzito.

Wiki iliyopita, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alifanya mazungumzo na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kwa njia ya simu, ambapo walikumbushana makubaliano mapya ya amani yaliyotiwa saini mjini Paris miezi miwili iliyopita.


Friday, February 14, 2020

Kenya Yawatimua Wachina Wanne Kwa Kosa la Kumchapa Viboko Mkenya Aliyechelewa Kazini

Raia wanne wa china waliokamatwa na Mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) wanatarajiwa kurudishwa kwao baada ya amri iliyotolewa na Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Fred Matiang'i.

Agizo hilo lilisainiwa na Matiang'i Jumatano baada ya mahakama kuruhusu polisi kuwashikilia wachina wanne kwa siku 15 huku uchunguzi ukiendelea juu ya tukio la kumchapa viboko raia wa Kenya aliyekua akifanya kazi katika mgahawa ulioendeshwa na Wachina hao mjini Nairobi.

Raia hao wa china waliotambuliwa kwa majina; Ou Qiang, Deng Hailan, Chang Yueping, na Yu-Ling; walitiwa nguvuni Jumapili baada ya video iliyoonyesha mmoja wa wahudumu wa mgahawa wa wachina akipigwa viboko na mmoja wao katika mgahawa wao kueneo kwenye mitandao ya kijamii.

Katika video hiyo mwanaume wa Kichina alionekana akimpiga viboko Mkenya aliyekua akifanya kazi katika mgahawa unaouza vyakula vya kichina Chez Wou Restaurant katika eneo la Kileleshwa jijini Nairobi.

Iliripotiwa kuwa Mkenya, Simon Oseko, alikua akichapwa viboko kwa kosa la kuchelewa kufika kazini.

Alipigwa viboko viwili na meneja huku wafanyakazi wenzake wakishuhudia kwa mbali.

Oseko aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi. Iliripotiwa kuwa mpishi wa Kichina katika mgahawa huo pia aliwatisha wafanyakazi wengine raia wa Kenya ili wasizungumzie kuhusu mateso wanayopitia katika mgahawa.

Walikamatwa kwa kumiliki vibali vilivyopitwa na wakati vya kuishi nchini Kenya na kufanya kazi nchini humo bila kuwa na vibali vya kazi. Baadhi walikua na vibali vya kutembea Kenya
-BBC



Wednesday, February 12, 2020

Adebayor afikisha klabu ya 10 katika soka, Club Olimpia watangaza kumpa kandarasi



Emmanuel Adebayor amejiunga na Club Olimpia ya nchini Paraguay akiwa mchezaji huru na kutangazwa siku ya Jumanne ya wiki hii.

Emmanuel Adebayor has signed for Paraguayan side Olimpia on a free transfer

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal, Manchester City na Tottenham, Emmanuel Adebayor hii inakuwa klabu yake ya 10 katika ulimwengu wa soka baada ya kumaliza kuitumikia klabu ya Kayserispor ya nchini Uturuki kwa miezi mitatu hadi mwezi Disemba.

Nyota huyo raia wa Togo kwa sasa ana umri wa miaka 35, na kwa muda alihusishwa kujiunga na miamba hiyo ya soka ya nchini Paraguay baada ya rais wa timu hiyo, Marco Trovato kuahidi kumsajili mchezaji huyo.

Un nuevo mensaje de @E_Adebayor para todos los hinchas de #Olimpia.

¡Estamos listos, Adeba! 🇹🇬#SeamosLeyenda pic.twitter.com/1T9IinrZpK

— Club Olimpia (@elClubOlimpia) February 11, 2020

Olimpia kwa sasa ipo kwenye nafasi ya tano kwenye ligi kuu ya nchi hiyo maarufu kama Apertura ambapo kwa sasa  Adebayor atakuwa pamoja na mshambuliaji wa zamani wa Manchester City, Roque Santa Cruz. Kwa upande wake, Santa Cruz alijiunga na club Olimpia mwaka 2016.

Adebayor will reunite with former Manchester City strike partner Roque Santa Cruz (right)

Klabu 10 alizo zitumikia Adebayor kabla ya kujiunga na Olimpia.

Anajumla ya michezo 446 aliyocheza kwenye ligi mbalimbali, za nchi nne tofauti, Adebayor akifunga jumla ya magoli 161 na 'assists'52.

2001–2003 Metz, 2003–2006 Monaco, 2006–2009 Arsenal, 2009–2012 Manchester City,  2011 → Real Madrid (loan),  2011–2012 → Tottenham (loan),  2012–2015 Tottenham Hotspur,  2016 Crystal Palace, 2017–2019 Istanbul BaSakSehir,  2019 Kayserispor,  2020– Olimpia


OMAR AL BASHIR KUPELEKWA MAHAKAMA YA ICC

Baraza la mpito Nchini Sudani limekubali kumkabidhi rais wa zamani Omar al Bashir kwa mahakama ya kimataifa ya ICC.


Omar al Bashir alikuwa akitafutwa kutokana na makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu.

Mwezi Desemba kiongozi huyo wa zamani aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi mwezi Aprili, alihukumiwa kifungo cha miaka miwili kwa makosa ya rushwa.



Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...