Monday, November 4, 2019

Kijana Aliyemtishia Mwenzake Kwa Bastola Afikishwa Mahakamani

Kijana Shaban Hamisi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni akikabiliwa na kosa la kumtishia silaha  Dereva wa lori la mchanga Venance John ikiwa ni siku chache baada ya kusambaa mitandaoni video ya tukio.

Amesomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mkunde Mshanga mbele ya Hakimu Mfawidhi, Frenk Moshi, ambapo inadaiwa tukio hilo amelitenda Oktoba 30, 2019 maeneo ya Mbezi Mabwepande.

Inadaiwa alikutwa na Pistol aina ya Berreta yenye namba za usajili 102969 ambapo kwa makusudi alimtishia Venance John huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria, baada ya kusomewa shtaka alikana ambapo pia upande wa mashitaka umesema hauna pingamizi na dhamana.

Baada ya kueleza hayo, Hamisi ambae pia ni Mume wa Mtangazaji Zamaradi Mketema ameachiwa kwa dhamana ya Wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho vya Taifa na wamesaini Bondi ya Sh.Mil 2 kwa kila mmoja, kesi imeahirishwa hadi November 13, 2019, mshitakiwa yupo nje kwa dhamana.


Thursday, October 31, 2019

Jiji La Dodoma Latozwa Faini Kutokana Na Uchafu Wa Machinjio

Na Lulu Mussa
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) hii leo imefunga machinjio ndogo ya Msalato kwa muda usiojulikana na kupiga faini kwa kosa la kukithiri kwa uchafu wa mazingira na miundombinu chakavu.
 
Hatua hiyo imefikiwa mara baada ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kufanya ziara ya kushtukiza katika eneo hilo na kujionea Mazingira yasiyoridhisha kwa usalama wa afya za binadamu. 
 
Katika ziara hiyo, wabunge wamejionea mazingira yasiyoridhisha na kuhatarisha afya za watumiaji wa nyama inayochinjwa machinjioni hapo ikiwa ni pamoja na kurundikana kwa samadi, kukithiri kwa harufu kali na kukosekana kwa maji safi.
 
Bw. Gratius Mwesiga, Afisa Mifugo wa Jiji la Dodoma ameieleza Kamati hiyo kuwa ukarabati katika eneo hilo umeanza na unaendelea kwa awamu, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa mifumo ya maji taka.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Sima amesema lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa manufaa ya afya za walaji. "Sisi watu wa Mazingira afya za binadamu ni kipaumbele namba moja, hali hii haikubaliki" Sima alisisitiza. 
 
Waziri Sima amemuagiza Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka kufanya tathmini ya haraka na kina na kuhakikisha kuwa machinjio yanazingatia taratibu zilizopo katika Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira Kanali Mstaafu Masoud Ali amesema hali ya usafi katika machinjio hiyo haidhirishi na kuwataka NEMC kuchukua hatua. "NEMC msingechukua hatua, sisi Kamati tungechukua, haiwezekani hali hii haikubaliki" Alisisitiza Mhe. Masoud Ali.
 
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC amelitoza faini Jiji la Dodoma ya kiasi cha Shilingi Milioni tano (5) kwa mujibu wa kifungu namba 194 cha sheria ya usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kutakiwa kuilipa ndani ya wiki mbili.


Treni Yawaka Moto, 62 Wafariki Dunia...Kisa Mtungi wa Gesi Kulipuka


WATU 16 wamefariki baada ya treni ya mwendokasi kuwaka moto na wengine 13 wamejeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea mapema leo huko Liaqatpur karibu na mji wa Rahim Yar Khan.



Waziri wa Masuala ya Usafirishaji wa reli, Sheikh Rashid Ahmad amesema moto umesababishwa na jiko la gesi lililopuka wakati abiria wakipika chai, jambo ambalo ni kinyume na sheria.





Treni hiyo ilikuwa inatokea Lahore kwenda Karachi. Majeruhi wamekimbizwa katika hospitali ya karibu huku shughuli za uokoaji zikiendelea.

Viongozi Ubungo Wananenepeana' - Paul Makonda



Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amewaonea huruma wakazi wa Ubungo kwa kile alichokieleza kuwa hawakuchagua viongozi sahihi, ambao wangeweza kutatua kero zao hii ni baada ya kufika katika eneo maalumu lililotengwa kwaajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya, bila kuwaona wabunge,


Hayo ameyabainisha leo Oktoba 29, 2019, alipotembelea eneo ambalo litajengwa hospitali hiyo inayotarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu, ujenzi utakaosimamiwa na Jeshi la kujenga Taifa (JKT), utakaogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 1.5.

''Kama nilivyosema juzi, Ubungo hatujapata viongozi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, tumepata kwa ajili ya matumbo yao na ndio maana nimefika hapa nikawa nawatafuta, Meya, Mbunge wa Kibamba na Ubungo yuko wapi, hayupo,sasa niwasihi wakati mwingine msiwaonee haya walafi na wanaonenepa kupitia pesa zenu, wakati wao wameshindwa hata kupaza sauti ili ninyi muweze kupata huduma bora, nafahamu kuna baadhi ya maeneo Ubungo yana changamoto ya barabara, lakini wabunge wenu wala Meya wenu hawana chochote cha kuongea lakini utawakuta wamehamia twitter'' amesema Makonda.

Kufuatia hali hiyo Makonda amewaomba wakazi wa Ubungo, katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wahakikishe wanachagua viongozi wanaojitambua na watakaoweza kuwasilisha vyema kero zao ngazi za juu.

Oktoba 26, 2019, wakati wa upokeaji wa ndege mpya Dreamline ya pili, Makonda aliwasilisha ombi la kutengewa fedha hizo, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, aliridhia ombi hilo na kuagiza zitengwe shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Source

Wednesday, October 30, 2019

PICHA YA RAIS MAGUFULI YAMPONZA IDRIS SULTAN ....MAKONDA AMTAKA AJISALIMISHE POLISI...KIGWANGALLA KUWEKA DHAMANA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amemtaka mchekeshaji na muigizaji hapa nchini, Idris Sultan, kuripoti katika kituo chochote cha polisi, hii ni baada ya msanii huyo ku 'post' picha katika ukurasa wake wa Instagram, akiwa amehariri picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na kuweka sura yake.

Makonda ametoa agizo hilo leo Oktoba 30, 2019, kupitia ukurasa wake wa Instagramu.

"Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha Polisi, uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako" ameandika Makonda.

Idris aliweka picha hizo ikiwa ni siku moja tu imepita tangu Rais Magufuli, atimize umri wa miaka 60, ambapo msanii huyo aliandika kuwa.

 "Kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy birthday yake kwa amani".

Makonda amesema, "nimesema kweli aende polisi sina utani na watu wa aina hiyo."

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema atamuwekea dhamana mchekeshaji Idris Sultan ikiwa ataripoti polisi na kukamatwa baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

 Dk Kigwangalla aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, "nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi."

"Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake. Wameonesha upendo."

Monday, October 28, 2019

MZEE SOMBI : VIJANA WANAOGOPA KUOA KWA SABABU HAWANA KAZI....HAWATAKI USUMBUFU



Mzee James Makungu Sombi (85) akizungumza na Malunde1 blog leo Jumatatu Oktoba 28,2019 

Wimbi la vijana kutooa ama kuolewa limekuwa likiongezeka kila kukicha kutokana na vijana kutofanya kazi za kuwaingizia kipato hivyo kuona jambo la kuwa na familia ni mzigo na usumbufu katika maisha yao.

Hayo yamesemwa na Mzee maarufu wa Kabila la Kisukuma James Makungu Sombi (85) mkazi wa Kisesa mkoani Mwanza wakati akizungumza na Malunde1 blog ambapo amesema kutokana na vijana kuwa wazembe,kutaka kula tu na kuzurura ndiyo maana suala la kuoa au kuolewa linakuwa gumu. 

"Msichana hana kazi,mvulana hana kazi unadhani wakianza kuishi pamoja nyumba itakalika?.Kijana hana kazi atamlisha nini mke wake?,pesa za kumvalisha zitatoka wapi?,ndiyo maana vijana hawaoi ili kukwepa majukumu ya familia kwani akioa atakosa raha akiwaza atapata wapi pesa za kutunza familia",amesema Mzee Sombi. 

"Zamani kilimo ndiyo ilikuwa ngao nzuri ya kumuweka mtu katika maisha mazuri,lakini siku hizi vijana hawataki kulima,hata kufanya kazi nzito nzito hawataki,ukimwambia kijana akalime unakuwa kama umemfukuza, wanakimbilia mjini,wao wanataka kula na kuzurura tu,sasa mtu wa namna hiyo ataoa kweli?",alihoji Mzee Sombi. 

"Zamani huku kwetu tulikuwa na Shikome,hii ilikuwa kama ofisi ya mambo mbalimbali,wazazi walitumia shikome kuongea na vijana wao,lakini siku hizi hakuna shikome,wazazi hawana muda wa kuzungumza na watoto wao na watoto nao hawataki kushauriwa na wazazi, matokeo yake tunakuwa na vijana wa hovyo kweli kweli",amesema. 

Anasema tofauti na sasa zamani wazazi walikuwa wanawatafutia vijana wachumba wa kuoa kisha kijana anaenda kuhakikisha kama mchumba anafaa ndipo anaoa lakini siku hizi vijana wanajiamulia wao wenyewe ndiyo maana hata ndoa hazidumu. 

"Kijana kajiamulia mwenyewe kuoa,msichana kakubali kuolewa,msichana yupo ndani ya ndoa akiona kijana huyo hana kazi anafikiri ataishije,mwisho wa siku kwa kuwa naye hana kazi anaamua kuondoka kwenda kutafuta pesa mahali pengine, na kama walibahatika kuzaa basi mtoto anajikuta analelewa na mzazi mmoja na mara nyingi mtoto atakuwa hana maadili na huo ndiyo mwendelezo wa kuwa na vijana wasio na maadili",ameelza 

Mzee Sombi anasema zamani wanandoa walikuwa wanavumiliana kwa sababu hawakuwa na tamaa ya kupata pesa wao nia yao ilikuwa ni kupata familia na kuzaa na kulea watoto wao. 

"Wasichana wetu siku hizi wakiona wamepata mtoto wanawaza kwamba huyu mtoto atamlisha nini ndiyo maana wengine wanaamua kuwatupa ili wapate nafasi ya kwenda kutafuta pesa kwa wanaume wengine,nawashauri wanawake wawe wanajishughulisha ili wapate kipato badala ya kutegemea wanaume ambao mara nyingi wamekuwa wakiwakimbia na kujikuta tunakuwa na Single Mother wengi 'familia ya mama na mtoto'",alisema Mzee Sombi.

Mzee James Makungu Sombi ambaye ni mkazi wa Kisesa Mwanza Manju Mstaafu wa ngoma za Kisukuma na ni miongoni mwa waanzilishi wa Makumbusho ya Kisukuma ya Bujora yaliyopo Kisesa jijini Mwanza

Mzee Sombi ni Mtaalamu wa Masuala ya Utamaduni wa Kabila la Kisukuma,Wasiliana naye kwa namba 0755903972

KUFANYA SANA MAPENZI KUNAPUNGUZA SIKU ZA KUISHI....BABU WA MIAKA 85 ATOA USHAURI

Mkutano wa kuvutia uwekezaji SADC kutoka China wafunguliwa

Mkutano wa kuvutia uwekezaji katika nchi za SADC kutoka Jimbo la Jiangsu umefunguliwa leo jijini Nanjing na Naibu Gavana wa Jimbo hilo Ndugu Ma Qiulin.

Mkutano huo umehudhuriwa na Mabalozi 11 wa nchi za SADC na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa SADC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Miundombinu wa Sekretariat ua SADC, Mapolao Mokoena.

Katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo Balozi wa Tanzania Mbelwa Kairuki alitoa hotuba kwa niaba ya Jumuiya ya Mabalozi wa Nchi za SADC nchini China ambapo pamoja na mambo mengine aliyakaribisha makampuni ya SADC kuchangamkia fursa za uwekezaji katika nchi za SADC kutokana na fursa za soko kubwa lenye idadi ya watu milioni 345 na uchumi wa GDP 600 Billioni.
Source

RC MNYETI : WANANCHI DONGOBESH WAPOKEENI WAFANYAKAZI WA HALMASHAURI YA MBULU


Na Beatrice Mosses - Malunde 1 blog 
WANANCHI wa kata ya Dongobesh wilaya ya Mbulu mkoani Manyara wametakiwa kuwapokea na kuwakaribisha wafanyakazi wa halmashauri hiyo ambapo wanatarajia kuhamishia makao makuu ya halmashauri hiyo ndani ya wiki hii.

Kauli hiyo imetolewa juzi na mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alipotembelea na kukagua jengo jipya la halmashauri ya wilaya ya Mbulu linalojengwa kwenye kata hiyo. 

Mnyeti alisema  ujio wa watumishi hao wa halmashauri kwenye kata ya Dongobesh utaleta mabadiliko ya haraka lakini pia mji utachangamka na maendeleo yataonekana kwa haraka zaidi. 

"Sasa nikuombe Mwenyekiti  uwahamasishe wananchi wa Dongobesh wawapokea watumishi kwa sababu tunaambiwa hapa kuna Ka Ukoo fulani ambako ndiko kana dominate kila kitu sasa kama mkifanya hivyo shauri yenu. 

"Lakini mkitaka maendeleo muwapokee watumishi, msiwafanye watumishi usiku wamelala wanaamka  wanajikuta wapo barabarani maana tunasikia kwamba hapa Dongobesh ni wataalamu sana wa sekta hiyo. 

"Niwaombe muwapokee watumishi na kuwafanya kama watoto wenu, sio tukileta hapa watumishi halafu mkawa mnawafanyia mambo ya namna hiyo tutawaondoa, tutajenga nyumba za halmashauri maeneo mengine watakuwa wanakuja kufanya kazi wanaondoka", Alieleza Mnyeti. 

Hata hivyo Mnyeti alishauri kwamba pindi watumishi wa halmashauri hiyo watakapohamia kwenye eneo hilo uitishwe mkutano wa wazee wa kimila wawapokee na kuwapa ulinzi wa kimila asidhurike mtu hata mmoja. 

Pamoja na hayo Mnyeti alipongeza kazi ya ujenzi unaoendelea kwenye jengo la halmashauri hiyo ambalo linajengwa na kampuni ya kijeshi ya Mzinga ambapo alidai kuwa fedha iliyotolewa inaendana na kazi inayofanyika. 

"Ingelikuwa tumetoa pesa halafu hakuna kinachofanyika tungesikitika sana, mwanzoni nilipita hapa nilimkuta mzee mmoja  tu na hapakuwa na mtu mwingine, nilisikitika sana   kwa sababu Mzinga tunaowaamini ni makampuni ya kijeshi ambayo tunaamini kwamba kazi zao zinakwenda kijeshi tulitoa mawazo yetu,  tulitoa ushauri na mmetekeleza tunawapongeza sana. 

"Sasa mlichonishawishi ni kitu kimoja tu kikubwa kwenda kuwatafutia pesa ili ije pesa nyingine muweze kuendelea na ujenzi huu na kwa spidi hii kwa kweli mmetufurahisha kwani hakuna kitu kibaya kama kuletewa pesa halafu miradi inakuwa haiendi",alisema.  

Kwa upande wake Mwenyekiti  wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu Joseph Mandoo alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli kwa kusimamia fedha za watanzania kutokana na huko nyuma kutokuwa na historia nzuri. 

"Sisi wana Mbulu niseme ametupendelea sana kwa sababu ametupa miradi mikubwa ya maendeleo kwenye shule za sekondari na msingi lakini kubwa zaidi ni kutuletea fedha bilioni mbili na milioni Mia tano kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri ya wilaya katika mji wa Dongobesh lakini pia ametuletea fedha zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya", alieleza Mandoo. 

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MKAKATI WA AJIRA NA UWEZESHAJI VIKUNDI VYA VIJANA


Na; Mwandishi Wetu
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mikakati iliyoweka katika kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na uwezeshwaji kiuchumi kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana "Youth Development Fund" na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya vijana katika Mkoa wa Morogoro, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga ameipongeza Serikali kwa mikakati iliyokuja nayo katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwajengea mazingira wezeshi na yanayowahamasisha kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.

"Matokeo ya utekelezaji wa mikakati hiyo tumeona kwa kiasi kikubwa imewawezesha vijana kutambua taratibu rasmi za kupata mikopo yenye riba nafuu na ambayo imewasaidia kuazisha miradi ya kiuchumi," alisema Mheshimiwa Giga.

Aliongeza kuwa Serikali iendelee kutenga bajeti zaidi ya uwezeshwaji wa vikundi vya vijana kwa kuwa vina tija na vinapunguza tatizo la ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa.

Sambamba na hayo Kamati hiyo iliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutoa maelekezo katika halmashauri zote kuelimisha vijana zaidi ili waweze kutambua taratibu za kupata mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana na asilimia 10 ya mikopo ambayo utolewa kwa Vijana 4%, Wanawake 4% na Wenye Ulemavu 2% kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.

Akitoa maelezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde ameihakikishia Kamati ya Bunge kwamba Serikali itaendelea kuviwezesha kiuchumi vikundi vya vijana katika mkakati wa kuhamasisha vijana kujiajiri lakini pia kuwajengea uwezo wa kiuchumi vijana ili nao pia washiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa uchumi wa viwanda ambapo matarajio ni kwamba ifikapo mwaka 2025 zaidi ya asilimia 40 ya nguvukazi iwe imeajiriwa kwenye sekta ya viwanda.

"Serikali iliazisha mfuko wa maendeleo ya vijana na programu mbalimbali ili kuwawezesha wananchi hususan vijana kuweza kupata mahitaji ya mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazo waingizia kipato," alisema Mavunde

Akitolea mfano mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vijana kutumia teknolojia ya kitalu nyumba ni mkakati mzuri ambao Serikali imekuja nao katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo.

Aidha, Naibu Waziri Mavunde aliwahamasisha vijana kuandaa maandiko ambayo yataelezea shughuli zenye tija wanazotaka kuzifanya katika kujileta maendeleo ili waweze kupata mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri itakayowasaidia kuendesha shughuli zao. 

Kwa nyakati tofauti vijana wa Mkoa wa Morogoro wameishukuru Serikali kwa uwezeshaji kupitia Mfuko wa maendeleo ya vijana na kuomba kuwezeshwa zaidi ili kukidhi matarajio yao ya uanzishwaji wa viwanda katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tano katika uchumi wa viwanda.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...