Friday, April 26, 2019

Picha : WARSHA YA MAMA RIKA YAFUNGWA MWANZA...'TUNATAKA WATOTO WAZALIWE BILA VVU' - AGPAHI

Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona akizungumza wakati wa kufunga warsha ya MAMA RIKA mkoa wa Mwanza Aprili 25,2019.
*****

Tunataka Taifa la Tanzania liwe na watoto wanaozaliwa bila kuwa na Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU)! 

Haya ni maneno ya Cecilia Yona ambaye ni Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii wa asasi ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) inayojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI na UKIMWI, wakati akifunga warsha kwa MAMA RIKA mkoa wa Mwanza iliyolenga kuwajengea uwezo kuhusu masuala mbalimbali ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. 




MAMA RIKA ni Waelimishaji wa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanaoishi na VVU ambao wanapata huduma za tiba na matunzo katika kliniki ya mama,baba na mtoto (RCH) ili kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto. 

Warsha hiyo ya siku mbili imemalizika Alhamis Aprili 25,2019 jijini Mwanza na kuhudhuriwa na MAMA RIKA 70,wauguzi, waratibu wa huduma ya afya ya uzazi,waratibu wa huduma za VVU na UKIMWI katika jamii mkoa wa Mwanza. 

Afisa Miradi huyo wa Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona alisema ili kuwa na watoto wanaozaliwa bila maambukizi ya VVU katika taifa la Tanzania ni lazima akina mama wanaoishi na VVU wapewe elimu ya kutosha kuhusu namna ya kuzuia maambukizi wakati wa ujauzito, kujifungua na wakati wa kunyonyesha. 

"Hatuwezi kupata watoto ambao ni Free From HIV (watoto wasio na HIV),bila akina mama kuwa na elimu,ndiyo maana AGPAHI tumewakutanisha MAMA RIKA ili tuwajengee uwezo juu ya masuala ya VVU na UKIMWI na namna ya kusaidiana kupitia uzoefu kutoka ujauzito mpaka watoto wanapopata kipimo cha mwisho cha uhakiki",alieleza Yona. 

"Lengo la kuwa na MAMA RIKA kwenye vikundi ni kusaidia kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,hivyo tunaamini mama akielewa vizuri,akipata elimu ya kutosha na akafuatilia yale aliyoelekezwa mtoto hatapata maambukizi ya VVU",alisema. 

"AGPAHI iko bega kwa bega kufanya kazi na  MAMA RIKA,tunaamini kwamba huyu mama akijengewa uwezo vizuri kwa njia ya wataalamu na kufundishana wao kwa wao,wanapata nafasi kubwa ya kujifunza wenyewe kwa wenyewe kwa kutumia uzoefu walionao,yule ambaye ameshajifungua atamfundisha mjamzito, yule amemaliza kunyonyesha atamfundisha anayeanza kunyonyesha, kwa hiyo wanafundishana kwa njia ya uzoefu na elimu hiyo inakuwa sehemu ya maisha yao na kuwasaidia akina mama wengine",aliongeza Yona. 

Yona alitoa wito kwa washiriki wa warsha hiyo kuwa mabalozi na wasimamizi kwa akina mama wengine ili watakaporudi wakawasaidie akina mama waliopo katika kitengo cha kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. 

Hata hivyo MAMA RIKA walioshiriki warsha hiyo walisema hivi sasa suala la ubaguzi na unyanyapaa limepungua kutokana na watu wengi kupata elimu kuhusu VVU na UKIMWI na wengi kujiweka wazi wakibainisha kuwa kupata maambukizi siyo mwisho wa maisha. 

Aidha walishauri elimu iendelee kutolewa zaidi kwa akina mama wajawazito wahudhurie kwenye vituo vya afya wafundishwe mambo muhimu badala ya kufuata maneno mtaani na kujinyanyapaa matokeo yake wanajifungua watoto wenye maambukizi.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Afisa Miradi huyo wa Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona akifunga warsha ya siku mbili ya MAMA RIKA mkoa wa Mwanza iliyofanyika katika ukumbi wa Gold Crest Hotel jijini Mwanza -Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Cecilia Yona akiwasisitiza washiriki wa warsha hiyo kuwa mabalozi kwa akina mama wengine wawape elimu ya kutosha kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI ili wazaliwe watoto wasio na maambukizi ya VVU.
Washiriki wa warsha wakiwa ukumbini.
Cecilia Yona akionesha kitabu cha mwongozo wa kuendesha vikundi vya akina mama wanaoishi na VVU wenye ujauzito na wanaonyonyesha kutoka kitengo cha kuzuia maambukizi ya toka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT).
MAMA RIKA,wauguzi, waratibu wa huduma ya afya ya uzazi na waratibu wa huduma za VVU na UKIMWI katika jamii  wakionesha vitabu vya mwongozo  wa kuendesha vikundi vya akina mama (PMTCT) baada ya kugawiwa wakati wa warsha hiyo. Kushoto ni Mwezeshaji wa kitaifa wa masuala ya Vijana,VVU na UKIMWI, Dkt. Happiness Wimile Mbeyela.
Washiriki wa warsha hiyo wakiwa ukumbini.
Awali,Mwezeshaji wa kitaifa wa masuala ya Vijana,VVU na UKIMWI, Dkt. Happiness Wimile Mbeyela akitoa mada kuhusu unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU.
Dkt. Happiness Wimile Mbeyela akisikiliza swali kutoka mmoja wa washiriki wa warsha hiyo.
Mwezeshaji katika warsha hiyo, Edwiga Zumba akitoa mada ukumbini.
Mwezeshaji katika warsha hiyo,Yahaya Isangula akiwasisitiza akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wenye maambukizi ya VVU kuendelea kuwa wafuasi wazuri wa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs).
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo akiuliza swali.
Mratibu wa huduma ya afya ya uzazi halmashauri ya wilaya ya Ilemela,Grace Kusaya akiwahamasisha MAMA RIKA kuwapa elimu akina wajawazito na wanaonyesha ili watoto wasipate maambukizi ya VVU.
Mratibu wa huduma ya afya ya uzazi halmashauri ya wilaya ya Misungwi, Flora Kuzenza akichangia hoja.
Kaimu mratibu wa huduma ya afya ya uzazi halmashauri ya wilaya ya Ukerewe, Laurencia Damas akizungumza ukumbini.
Picha ya pamoja washiriki wa warsha.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Soma pia : AGPAHI YAENDESHA WARSHA KWA MAMA RIKA MKOA WA MWANZA

Picha : MAKAMPUNI,MASHIRIKA YAUNGANA NA LA PRINCE PUB KUTOA ZAWADI KWA WAGONJWA HOSPITALI YA MKOA WA SHINYANGA

Wadau wa Maendeleo mkoa wa Shinyanga wakiongozwa na Kampuni ya La Prince Pub inayojihusisha na biashara ya uuzaji vinywaji na chakula Mjini Shinyanga wamesherehekea Sikukuu ya Miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kutembelea na kuwapatia misaada mbalimbali wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Miongoni mwa zawadi zilizotolewa kwa akina mama na watoto ni pamoja na sabuni,mafuta ya kujipaka juisi,poda, miswaki,dawa za meno,matunda, toilet papers,biskuti,maji na zawadi zingine.

Wadau walioungana na wafanyakazi wa La Prince Pub kutembelea na kutoa misaada kwa wagonjwa leo Aprili 26,2019 ni pamoja na Kampuni ya Lulekia,Jambo Food Products Co. Ltd,Astro Secure Co. Ltd,Uptown Holdings Co.Ltd,Msirikale Microfinance,24 Security Tanzania,Ommy Fashion, Gvenwear,Shirika la TVMC,Dellah Car Traders,Luxury Pub,Friends of Bhoke na Malunde 1 blog.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo,Mkurugenzi wa Kampuni ya La Prince, Athanas William alisema wameamua kuungana na wadau wa maendeleo mkoa wa Shinyanga ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii inayowazunguka.

Alisema zawadi hizo kwa wagonjwa zimetolewa kupitia Mpango maalumu ulioanzishwa na La Prince Pub unaojulikana kwa jina la 'La Prince Charity Movement' kwa lengo la kuisaidia jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali,makampuni na wafanyabiashara mbalimbali. 

"Tumefika hapa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kutoa pole kwa wagonjwa na kuwapa misaada mbalimbali,tumejumuika sisi wafanyakazi wa La Prince na wadau wengine wa maendeleo wakiwemo kutoka kwenye mashirika na makampuni ambao tumeungana kuja kurudi kurudisha fadhila kwa jamii kwa kutoa misaada kwa wagonjwa katika wodi za akina mama na watoto",alisema.

"Tukiwa sehemu ya jamii tumeona ni busara zaidi katika siku hii ya kuadhimisha miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo hatufanyi sherehe za kitaifa,sisi tumeona tufanye sherehe ndogo ya kuwapa pole wanaoumwa na wenye mahitaji maalumu",aliongeza William.

"Kilichotusukuma sisi ni moyo wa upendo,sisi tuna mpango maalumu unaitwa La Prince Movement ambapo kila mwezi tumeamua kuunganisha wadau mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga kutoa misaada mbalimbali katika kada mbalimbali, leo tumeanza na hospitali na hivi karibuni tutambelea magereza",alieleza Mkurugenzi wa La Prince Pub.

ANGALIA PICHA HAPA
Mkurugenzi wa Kampuni ya La Prince, Athanas William akizungumza katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga wakati wadau mbalimbali wa maendeleo walipotembelea wagonjwa na kuwapatia zawadi akina mama na watoto waliolazwa katika hospitali hiyo leo Aprili 26,2019 ikiwa ni siku ya maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mmoja wa wafanyakazi wa La Prince Pub akiweka sawa zawadi mbalimbali zilizotolewa na wadau wa maendeleo mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya akina mama na watoto waliolazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Baadhi ya wafanyakazi wa La Prince Pub wakiwa wamebeba zawadi mbalimbali.
Wadau wa maendeleo wakiwa na zawadi zao wakijiandaa kuingia katika wodi mbalimbali katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kugawa zawadi hizo kwa wagonjwa.
Safari ya kuelekea wodini..
Wadau wa maendeleo wakielekea katika wodi za watoto.
Mkurugenzi wa Kampuni ya La Prince, Athanas William akizungumza katika moja ya wodi akielezea lengo la wadau kufika katika hospitali hiyo.
Wadau wa maendeleo wakiwa wodini na zawadi zao kabla ya kuanza kuzigawa.
Mkurugenzi wa Kampuni ya La Prince, Athanas William akisalimiana na mmoja wa Madaktari katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga aliyekutwa wodini.
Wadau wakitoa zawadi kwa mama aliyelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.

Gvenwear akitoa zawadi ya poda
Zoezi la ugawaji zawadi likiendelea
Twendeni kwenye wodi nyingine...
Mkurugenzi wa Kampuni ya La Prince, Athanas William akizungumza katika moja ya wodi za akina mama.
Wafanyakazi wa Ommy Fashion wakitoa zawadi kwa mgonjwa.
Mfanyakazi wa Lulekia akikabidhi zawadi ya mafuta ya kujipaka.
Wafanyakazi wa La Prince Pub wakitoa zawadi katika wodi ya watoto.
Mkurugenzi wa Kampuni ya La Prince, Athanas William akisalimia akina mama katika wodi ya watoto.
Utoaji zawadi ukiendelea katika wodi ya akina mama waliojifungua. katikati ni Bhoke Wambura, muanzilishi wa Friends of Bhoke.
Wadau wakiongozwa na Mkurugenzi wa shirika la TVMC,Musa Jonas Ngangala (katikati) wakikabidhi zawadi ya ndoo ya sabuni na zawadi zingine kwa mama aliyejifungua watoto mapacha wa kiume.
Wafanyakazi wa La Prince wakiwa nje ya wodi ya wanawake.
Wafanyakazi wa La Prince wakimsalimia na kumpa pole pamoja na zawadi mama wa mmoja mfanyakazi mwenzao aliyelazwa katika wodi ya wanawake.
Wadau wa maendeleo wakiwa nje ya wodi ya wanawake.
Wadau wa maendeleo wakipiga picha ya kumbukumbu
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...